'Sina ujasiri alio nao Lissu': Mke wa Lissu aelezea gharama ya mapambano ya kisiasa ya Tanzania kwa familia

    • Author, Beryl Munoko
    • Author, Valerie Cardi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Alicia Lissu hajazungumza wala kumuona mumewe Tundu Lissu kwa mwaka mmoja sasa. Lissu ambaye ni kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, anakabiliwa na kesi ya uhaini.

Amekuwa akifuatilia kesi hiyo akiwa uhamishoni nchini Ubelgiji kwa kupitia taarifa mtandaoni, mawakili wa mumewe au shemeji yake.

"Miezi mitatu ya kwanza ilikuwa migumu sana, nilisongwa na mawazo," Alicia ameimbia BBC Africa Eye.

Lissu, mwenye umri wa miaka 58, alikamatwa mwezi Aprili 2025 wakati akifanya kampeni chini ya kaulimbiu ya chama chake Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), "Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi."

Mamlaka zilielezea kuwa kampeni hiyo ilikuwa ikichochea umma kupinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

"Nilipatwa na hofu kubwa," anasema. "Lissu alikuwa amekamatwa mara kadhaa hapo awali, lakini safari hii lilikuwa shtaka kubwa zaidi."

Kiongozi huyo hawezi kuachiliwa kwa dhamana, mawasiliano ni finyu na shtaka analokabiliwa nalo linaweza kupelekea hukumu ya kifo chini ya sheria za Tanzania.

Serikali inakanusha madai kwamba uhuru wa kisiasa unazidi kubanwa.

Serikali ya Tanzania iliambia BBC mwezi Januari 2026 kwamba: "Chini ya uongozi wa Rais Samia, nafasi ya kiraia imepanuliwa kwa kuruhusu wanasiasa na wananchi kushiriki mikutano na kampeni za kisiasa. Tanzania sasa inaongoza nchi zilizoko Afrika Mashariki kwa uhuru wa vyombo vya habari."

Serikali pia iliongeza kuwa sheria lazima izingatiwe, "Rais Samia alimwalika Tundu Lissu, aliyekuwa uhamishoni, kurejea Tanzania ili kuendelea na shughuli za kisiasa. Hata hivyo, hakuna aliye juu ya sheria. Kesi ya Tundu Lissu haiwezi kujadiliwa kwa kuwa suala hilo liko mahakamani."

Baada ya kupata taarifa za kukamatwa kwa mumewe, Alicia hakurejea Tanzania. Badala yake alifunga safari kutoka Brussels alikoishi tangu mwaka 2018 na kuelekea Marekani, ambako wanawe walikuwa wakisoma.

Mmoja wa watoto wao alikuwa akijiandaa kwa mitihani ya chuo kikuu, na aliogopa kuwa taarifa hizo zingewaathiri sana kisaikolojia.

"Walikuwa na maswali mengi. Walitaka kujua ni kwa nini nilikuwa na uhakika kwamba baba yao angeachiwa huru."

Ghafla, jukumu lake likawa ni kuhakikisha familia inabaki imara.

"Niliwaelezea wanangu kuwa baba yao ana hadhi ambayo wengi wetu hatuna. Mimi sina ujasiri wala vipaji alivyo navyo. Tunapaswa kujivunia yeye."

Ijapokuwa aliwatia moyo wanawe, Alicia alikabiliana na hali mpya ambayo hakuwahi tarajia atakumbana nayo.

"Kwa mara ya kwanza kabisa, nilijikuta kuwa sina msaada wowote kutoka kwa Lissu," anasema. "Hakuwepo na pia hakuna msaada wa kifedha. Ninalazimika kujitunza pamoja na kuwalea watoto wetu."

Dalili za mwanaharakati wa haki za binadamu

Mara ya kwanza Alicia Lissu aliona namna mumewe alikuwa tayari kupigania haki kwa vyovyote vile, alikuwa mwanafunzi wa sheria akiwakimbia polisi.

Ilikuwa miaka ya tisini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alicia alikuwa chumbani mwake aliposikia mlango ukibishwa kwa nguvu.

"Tundu alikuwa akihema," anakumbuka. "Aliniambia, 'Nahitaji sehemu ya kujificha'."

Kulikuwa na maandamano ya wanafunzi chuoni, na polisi walikuwa wameitwa kuzima vurugu. Maafisa walikuwa wameleta mbwa.

"Nilivutiwa na ujasiri wake na namna alitaka kujihusisha na siasa za chuo kikuu," anasema.

"Nilimuambia, 'Tundu, unapaswa kuwa mwangalifu. Watu wanaweza kukudhuru'."

Hiyo haikuwa mara ya mwisho Alicia kujikuta akihofia usalama wa Lissu.

Zaidi ya miongo mitatu baadaye, anazungumza akiwa nchini Ubelgiji. Maisha ya uhamishoni hayakuwa sehemu ya mipango yao. Vivyo hivyo, kukamatwa mara kwa mara, kushambuliwa kwa risasi 16 katika jaribio la kumuua, na sasa kukabiliwa na shtaka la uhaini.

Hata hivyo, anapotafakari maisha yao pamoja, kinachojitokeza si simulizi ya mwanasiasa aliyekuwa tayari kupoteza uhuru wake kwa ajili ya imani zake za kisiasa. Pia ni simulizi ya mke aliyeshuhudia gharama za kitaaluma na ya kibinafsi ya kuolewa na mwanamageuzi.

"Nilivutiwa na Lissu kwa sababu alikuwa mwerevu sana," Alicia Lissu anasema.

Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza wakati wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, kabla ya kukutana tena walipojiunga na shule ya sheria Chuo Kikuu.

Walisoma pamoja mara kwa mara katika maktaba na wakawa marafiki wa karibu kabla ya kuwa wanandoa.

"Nilianza kuelewa mtazamo wake kuhusu kila jambo aliloliona kuwa si la haki."

Anaamini mtazamo huo ulitokana na malezi yake na pia kutoka kwa baba ambaye, "alichukia aina yoyote ya unyanyasaji au dhuluma kwa watu wengine".

Aligombea ubunge mwaka wa 1995 lakini hakufanikiwa.

Hata hivyo walipofunga ndoa mwaka wa 1997, Alicia tayari alijua siasa zingekuwa na sehemu muhimu katika maisha yao.

Mwaka 2008, Lissu alianza kuzungumza kuhusu kurejea kwenye siasa na kugombea tena ubunge.

Alicia anakumbuka kuwa hakuwa na hofu sana kuhusu uchaguzi, bali kuhusu kulea watoto.

"Kulea watoto wakati mume wako ni mwanasiasa si jambo rahisi," anasema.

Na kweli alikuwa sahihi.

Kutokuwepo nyumbani kwa muda mrefu kuligeuka kuwa jambo la kawaida huku Lissu akisafiri kote nchini Tanzania kutafuta uungwaji mkono kwa chama chake, Chadema.

"Mwaka mpya wa kwanza tuliouadhimisha tukiwa hatuko pamoja kama familia ulikuwa mwaka wa 2008," anasema.

Kadri mafanikio ya Lissu ya kisiasa yalivyoongezeka, familia ilimuona mara chache zaidi.

Kamata kamata ikaanza

Lissu alichaguliwa kuwa mbunge wa Singida Mashariki mwaka 2010 na akajijengea sifa kama mmoja wa wanasiasa wa upinzani wenye msimamo thabiti.

Lakini Alicia anasema hali ilibadilika baada ya hayati Rais John Magufuli kuwa rais mwaka 2015.

Kadiri Lissu alivyoendelea kuikosoa serikali na kupinga sera za rais hadharani, kukamatwa kwake kukawa jambo la kawaida.

"Mwaka 2016 ulikuwa mgumu sana kwa familia yangu."

Alikamatwa mara kwa mara na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi. Mojawapo ya mashtaka hayo lilitokana na madai yake kwamba ndege ya serikali ilikuwa imezuiliwa nchini Canada kutokana na deni ambalo halikulipwa.

Alicia anakumbuka miezi iliyotawaliwa na safari za vituo vya polisi, kufika mahakamani, kusikilizwa kwa maombi ya dhamana na maandalizi ya kisheria.

"Sikufanya kazi mwaka 2016," anasema. "Ilikuwa ni kukamatwa baada ya kukamatwa."

Mwaka 2017 hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Lissu kumweleza kuwa alikuwa akifuatiliwa.

Licha ya Lissu kuwakabili watu waliokuwa ndani ya gari lililokuwa likimfuatilia na hata kutoa wito hadharani wa kutaka uchunguzi ufanyike, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

"Nilijawa na hofu," anasema Alicia. "Nilihofia maisha yake yapo hatarini."

Lakini Lissu alisimama imara; alisema, "Sitawacha. Sitakoma kutoa maoni yangu kuhusu kile ninachoamini kuwa ni sahihi."

Siku ambayo kila kitu kilibadilika

Tarehe 7 Septemba 2017, Lissu alitoka bungeni mjini Dodoma akielekea nyumbani. Watu waliojihami kwa bunduki walimfyatulia risasi. Alipigwa risasi 16 tumboni na mguuni.

Alicia alianza kwa kupokea taarifa hiyo kupitia ujumbe kwenye simu yake. Picha zilipoanza kusambaa zikionyesha nguo za mumewe zikiwa zimelowa damu, alihisi huenda amefariki dunia.

"Nilipiga nduru," anasema, "Lissu amepigwa risasi."

Hata sasa, miaka mingi baadaye, bado anapata ugumu kuelezea yaliyofuata. Aliwaona majirani wakikusanyika kimya kimya nje ya nyumba yake.

"Muonekano wa nyuso zao bado imeniganda akilini," anasema kwa sauti ya chini. "Picha hizo zimesalia akilini mwangu."

Alipelekwa kwa haraka uwanja wa ndege na kusafirishwa hadi hospitali mjini Dodoma, ambapo aliambiwa kuwa mumewe alikuwa hai.

"Nilipomuona, hapo ndipo kwa mara ya kwanza niliamini kuwa Lissu alikuwa amenusurika."

Lakini afueni hiyo haikudumu.

Lissu ilibidi asafirishwe hadi Nairobi kwa matibabu maalum.

Alicia anasema wakati mmoja moyo wake ulisimama na madaktari walipambana.

"Tulikuwa tumesimama tu pale," anakumbuka. "Nilikuwa nikisali kila sala niliyoijua."

Baada ya matibabu zaidi nchini Kenya, alihamishiwa Ubelgiji kwa miaka kadhaa ya upasuaji na matibabu ya kumrejesha afya na uwezo wa kutembea.

Kwa Alicia, baadhi ya majeraha hayajawahi kupona.

"Hakujawahi kufanyika uchunguzi wowote," anasema. "Hilo ndilo linalochangia kuwepo kwa makovu hayo."

Kutoka uhamishoni hadi gerezani

Hatimaye familia hiyo ilihamia Ubelgiji ambapo Lissu alipata matibabu.

"Tulifika mwanzoni mwa msimu wa baridi kali, na kulikuwa na baridi kali sana," anasema.

"Lakini nilihisi afueni kubwa sana."

Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, familia hiyo ilipata hali ya utulivu badala ya misukosuko.

Kufuatia kifo cha Rais John Magufuli mwaka 2021, Samia Suluhu Hassan alichukua madaraka kama Rais wa Tanzania.

Serikali yake ilionyesha nia ya kufungua zaidi mazingira ya kisiasa na kuwahimiza viongozi wa upinzani waliokuwa uhamishoni kurejea nchini.

Mwezi Januari 2023, zaidi ya miaka mitano baada ya kushambuliwa kwa risasi, Lissu alirejea Tanzania.

"Aliniambia, 'Ninahitaji kurudi nyumbani kutoa mchango wangu na maarifa yangu ya sheria kusaidia mchakato wa maridhiano ambao unaweza kufungua njia ya mabadiliko'," Alicia anasimulia.

Alimsaidia mumewe kujiandaa kwa ajili ya safari hiyo ya kurejea Tanzania.

"Nilijua wakati ambao sikupaswa kumshinikiza," anasema.

Kulikuwa na matumanini kwamba ukurasa mpya unafunguliwa. Badala yake, mgongano mwingine na serikali ulikuwa unamsubiri.

Sasa anapozungumzia mumewe, hata wakati kuna sintofahamu kuhusu kesi yake ya uhaini, Alicia bado anamwona yule kijana aliyekuja chumbani kwake chuoni akiwa anahema baada ya kukimbia maandamano ya wanafunzi.

Yule yule aliyeamini kuwa ni wajibu wake kupinga kile alichokiona kuwa si haki.

Kwa Alicia, msimamo huo thabiti ndio chanzo cha fahari yake lakini pia ni chanzo cha maumivu yake.

"Huyu si Lissu mwenye hofu," anasema. "Huyu ni Lissu ambaye huwezi kumpuuza."

Baada ya maombi kadhaa ya kutaka maoni kutoka kwa serikali, Serikali ya Tanzania iliomba tufanye mahojiano ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Spika wa Bunge na Waziri wa Nchi. BBC ilikataa kufanya mahojiano hayo na wote watatu, kwa kuwa yasingeweza kufanyika kwa ufanisi. Baadaye, serikali ilikataa kutoa maoni.