CECAFA: Harambee Starlets wawalaza Malkia wa Kilimanjaro na kubeba taji la 2019

Timu ya soka ya kandanda kwa upande wa akina dada ya Kenya Harambee Starlets ndio washindi wa kombe la CECAFA 2019.
Starlets waliwashinda Kilimanjaro Queens 2-0 siku ya Jumatatu katika fainali iliochezwa katika uwanja wa Chamazi , mjini Dar es Salaam na kubeba taji hilo la eneo hili.

Mshambuliaji wa klabu ya malkia wa Vihiga Jentrix Shikangwa ambaye alinga'ra katika mechi hiyo baada ya kuingia kama mchezaji wa ziada na kufunga magoli mawili katika kipindi cha pili na kuweka idadi yake ya mabao katika michuano hiyo kufikia tisa.
Kilikuwa kisasi kizuri kwa Starlets waliopoteza 2-1 kwa Tanzania mwaka 2016 katika eneo la Gulu, Uganda mbali na wakati mzuri kwa wachezaji hao baada ya kuondolewa katika michuano ya kufuzu kwa mashindano ya Olimpiki ya 2020.

Mchezaji huyo mahiri alifunga kupitia mkwaju wa penalti katika dakika ya 71 kabla ya kuongeza uongozi huo kupitia kombora kali katika dakika ya 87.
Ushindi huo umefanya Kenya kumaliza michuano hiyo bila kushindwa na bila kufungwa goli katika mashindano hayo.

Starlets ilimaliza juu katika kundi B na pointi tisa baada ya ushindi dhidi ya Ethiopia wa 2-0 . ikailaza Djibout 12-0 na Uganda 3-0 kabla ya kuicharaza Burundi 5-0 katika nusu fainali.
Katika kutafuta mshindi wa tatu Uganda iliilaza Burundi 2-0 na kuchukua medali ya shaba.













