Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Iran yafanya mashambulizi mapya, ndege za Marekani zaanguka Kuwait

Wakati huo huo nchini Lebanon, mshambulizi ya Israel yamewauwa takriban watu 31, wizara ya afya inasema. Israel inasema ilikuwa ikijibu mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na roketi kutoka kwa Hezbollah.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Asha Juma

  1. Iran yasema watu 40 wameuawa katika shambulio dhidi ya shule ya wasichana – ripoti

    Afisa mmoja ameliambia Shirika la Habari la Taifa la Iran (IRNA) kuwa watu 40 wameuawa kufuatia shambulio la Israel dhidi ya shule ya msingi ya wasichana katika kaunti ya Minab, mkoa wa Hormozgan kusini mwa Iran, tarehe 28 Februari.

    Gavana Mohammad Radmehr amesema watu wengine 48 walijeruhiwa, na kwamba idadi ya vifo kutokana na shambulio hilo katika Shule ya Wasichana ya Shajareh Tayyebeh inaendelea kuongezeka.

    BBC haijaweza kuthibitisha taarifa hizi kwa njia huru, kwani mara nyingi mashirika ya habari ya kimataifa hukataliwa viza za kuingia Iran, hali inayopunguza uwezo wao wa kukusanya taarifa kuhusu matukio yanayoendelea ndani ya nchi hiyo.

    Kando na hilo, Iran inakabiliwa na kukatika kwa huduma ya intaneti, sambamba na taarifa za awali za shambulio la kimtandao.

    Soma zaidi:

  2. Umoja wa Ulaya waeleza wasiwasi wao kufuatia mashambulizi yanayoendelea dhidi ya Iran

    Katika kujibu mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, Umoja wa Ulaya uliyataja matukio hayo kuwa "hatari" na kutoa wito wa kulindwa kwa raia.

    Haya yanajiri baada ya Iran kuanza mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya washirika wakuu wa Marekani.

    Kambi ya kijeshi ya Marekani iliyoko Qatar imeshambuliwa pamoja na Bahrain na UAE.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Qatar yalaani shambulizi la Iran kwenye anga yake

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imelaani katika taarifa yake "ukiukaji wa wazi" wa anga yake uliofanywa na Iran katika shambulio la kombora.

    Taarifa hiyo ilisema kuwa Qatar "inahifadhi haki ya kujibu."

    Hapo awali, ripoti zilichapishwa kuhusu shambulio la Iran kwenye kambi ya Kijeshi ya Marekani huko Doha.

    Soma Pia:

  4. Waziri Mkuu wa Australia: Tunaunga mkono hatua za Marekani dhidi ya Iran

    Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese ametangaza kwamba nchi yake inaunga mkono hatua za Marekani dhidi ya Iran, kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi yaTehran.

    Bwana Albanese aliandika katika ujumbe kwenye mtandao wa X: "Imejulikana kwa muda mrefu kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa."

    Ameongeza kuwa: "Tunaunga mkono hatua ya Marekani ya kuizuia Iran kupata silaha ya nyuklia na pia kuzuia kuendelea vitisho vya Iran kwa amani na usalama wa kimataifa."

  5. Ofisi ya Kiongozi Mkuu wa Iran yaripotiwa kushambuliwa

    Milipuko kadhaa imeripotiwa kusikika katika mji mkuu wa Tehran na katika miji mingine kadhaa nchini Iran, huku taarifa zikieleza kuwa maeneo nyeti ya serikali na kijeshi yameshambuliwa.

    Kwa mujibu wa duru za habari, ofisi ya Kiongozi Mkuu wa Iran pamoja na ofisi ya rais mjini Tehran ni miongoni mwa maeneo yaliyoripotiwa kushambuliwa. Hata hivyo, mamlaka za Iran hazijatoa taarifa rasmi kuhusu kiwango cha uharibifu au majeruhi.

    Mashambulizi pia yameripotiwa katika maeneo ya kijeshi ya Kermanshah, Qum, Isfahan, Tabriz na Karaj, pamoja na vituo vya majini vya Iran vilivyoko Kenarak, kusini mwa nchi.

    Video kutoka mji wa Kamyaran katika eneo la Wakurdi zinaonyesha kile kinachoelezwa kuwa kambi ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ikishambuliwa.

    Jeshi la Israel lilitoa onyo kwa raia wa Iran kuondoka katika maeneo yaliyo karibu na vituo na miundombinu ya kijeshi kabla ya kutekelezwa kwa mashambulizi hayo.

    Wakati huohuo, picha kutoka Tehran zinaonyesha makazi katika kitongoji cha Narmak, ambako anaishi rais wa zamani Mahmoud Ahmadinejad, yameathirika. Haijathibitishwa iwapo kiongozi huyo wa zamani amejeruhiwa.

    Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imesema vikosi vya usalama vimewekwa katika hali ya utayari ili kudhibiti hali ya usalama, huku hospitali kadhaa kote nchini zikiwa katika hali ya tahadhari kupokea majeruhi iwapo watakuwepo.

    Soma pia:

  6. Shirika la ndege la Kenya Airways lasitisha safari za UAE kwa muda kufuatia kufungwa kwa anga

    Shirika la Ndege la Kenya Airways limetangaza kusitisha kwa muda safari zake kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kutokana na kufungwa kwa anga ya nchi hiyo.

    Katika taarifa kwa wateja iliyotolewa Februari 28, 2026, shirika hilo limesema limeahirisha safari za kwenda Dubai na Sharjah hadi itakapotolewa taarifa nyingine.

    Kwa mujibu wa notisi iliyosomwa na BBC, inaeleza kuwa ''Kutokana na hatua hiyo, na kwa kuzingatia usalama wa abiria na wahudumu wa ndege, Kenya Airways imefuta safari nambari KQ310, KQ305 pamoja na safari za mizigo (freighter flights)''.

    Shirika hilo limeomba radhi kwa usumbufu wowote uliosababishwa na kuahidi kuwasiliana moja kwa moja na wateja walioathirika ili kuwapatia msaada unaohitajika.

    Kenya Airways imesema itaendelea kutoa taarifa kadri hali inavyoendelea kubadilika na imewahimiza wateja kufuatilia masasisho ya safari kupitia tovuti yake, programu ya simu au kuwasiliana na Kitengo cha Huduma kwa Wateja.

    Hatua hiyo inafuatia mashambulizi yanayoendelea nchini Iran yaliyopelekea kufungwa kwa anga ya UAE.

    Soma pia:

  7. Iran yasema ilijua mapema kuhusu mipango ya mashambulizi ya Marekani na Israel

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema katika taarifa yake kuwa, ingawa Tehran ilikuwa inafahamu kuhusu “nia” ya Marekani na Israel kutekeleza mashambulizi hayo, iliendelea kushiriki mazungumzo ya kidiplomasia bila kujali hali hiyo.

    Taarifa hiyo ilikiri kuwa mashambulizi hayo yalifanyika “wakati ambapo Iran na Marekani zilikuwa katika mchakato wa kidiplomasia.”

    Duru ya tatu ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia kati ya Iran na Marekani ilifanyika siku mbili zilizopita, Februari 26, mjini Geneva, bila kufikia mafanikio yoyote.

    Tangu Mei mwaka jana, Iran na Marekani zimefanya pia duru tano za mazungumzo bila mafanikio.

    Duru ya sita iliyokuwa imepangwa kufanyika Juni 2025 ilisitishwa baada ya Israel kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya maeneo ya Iran, jambo lililosababisha mzozo wa siku 12 ambapo Marekani ilishambulia vituo vitatu vya nyuklia ndani ya Iran.

    Soma pia:

  8. Iran yashambulia kambi za jeshi la Marekani Mashariki ya kati

    Kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran asubuhi ya Jumamosi, Tehran imejibu kipigo kwa kulenga washirika wa Marekani.

    Milipuko na ving'ora vya mashambulizi ya anga vimesikika katika mji mkuu wa Qatar, Doha.

    Wizara ya ulinzi ya Qatar ilisema "imefanikiwa kukabiliana na mashambulizi kadhaa yaliyolenga eneo la nchi hiyo", kulingana na vyombo vya habari vya serikali.

    Afisa mmoja wa Qatar ameliambia shirika la habari la AFP kwamba betri ya Patriot iliyotengenezwa Marekani ilinasa kombora la Iran.

    Qatar ni mwenyeji wa kambi ya kijeshi ya Al Udeid, kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani katika eneo hilo la mashariki ya kati.

    Vile vile, Iran haikukomea hapo, ililipua kambi za jeshi la Marekani nchini Bahrain, UAE na Kuwait.

    Kambi hizo ni kama vile kambi ya Al Salem, Al Dhafra, Al Udeid na pia Makao ya Kikosi cha 5 cha Jeshi la Wanamaji la Marekani yashambuliwa nchini Bahrain.

    Mashambulizi yanaendelea na hayajulikani muafaka utaafikiwa lini.

    Soma Zaidi:

  9. Uingereza yatahadharisha dhidi ya vita vya kikanda baada ya mashambulizi dhidi ya Iran

    Msemaji wa serikali ya Uingereza amesema Uingereza “haitaki kuona ongezeko zaidi la mvutano unaoweza kugeuka kuwa mzozo mpana wa kikanda,” kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Akiongezea: “Kipaumbele chetu cha haraka ni usalama wa raia wa Uingereza walioko katika eneo hilo, na tutawapatia msaada wa kibalozi unaopatikana saa 24 kwa siku.”

    Imeelezwa pia kuwa, kama sehemu ya ahadi ya muda mrefu ya Uingereza kwa usalama wa washirika wake katika Mashariki ya Kati, nchi hiyo ina uwezo mbalimbali wa kujihami katika eneo hilo, ambao umeimarishwa hivi karibuni. “Tuko tayari kulinda maslahi yetu,” ilisema taarifa hiyo.

    BBC inaufahamu kuwa Uingereza haikushiriki katika mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, anatarajiwa kuongoza kikao cha dharura cha kamati ya Cobra ya serikali Jumamosi ya tarehe 28 mwezi Februari 2026.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Mtandao wa intaneti Iran wakaribia 'kuminywa' kikamilifu

    Iran kwa sasa inakabiliwa na kukatika kwa huduma ya intaneti kwa mujibu wa NetBlocks, shirika la ufuatiliaji wa mtandao, wakati Marekani na Israel zikiendelea na mashambulizi dhidi ya Iran.

    Hii si mara ya kwanza kwa nchi hiyo kuzima huduma ya intaneti.

    Mwezi uliopita tu, Iran ilikumbwa na kukatika kwa intaneti wakati wa maandamano ya kitaifa yaliyoenea kote nchini na ambayo yalizimwa kwa nguvu na serikali.

    Baadhi ya watu waliweza kwa muda mfupi kupata huduma ya intaneti kwa kutumia mbinu kama huduma ya intaneti ya setilaiti ya Starlink ya kampuni ya SpaceX pamoja na mitandao ya faragha pepe (VPN). Inawezekana kwamba wale watakaoweza kupata huduma watajaribu kutumia mbinu hizo tena.

    BBC Verify inaendelea kufuatilia na kuthibitisha picha na video za mashambulizi hayo katika eneo husika, na taarifa zaidi zitatolewa hivi karibuni.

    Soma Pia:

  11. Habari za hivi punde, Makao ya Kikosi cha 5 cha Jeshi la Wanamaji la Marekani yashambuliwa nchini Bahrain

    Milipuko imeripotiwa katika mji mkuu wa Bahrain.

    Tukio hilo limetokea baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain kutangaza kupitia ujumbe kadhaa kwenye mtandao wa X kuwa ving’ora vya tahadhari ya dharura vilikuwa vimewashwa. Wizara hiyo pia iliwasihi wakazi kubaki watulivu na kuelekea katika maeneo salama yaliyo karibu.

    Kituo cha huduma cha Jeshi la Wanamaji la Marekani nchini Bahrain, kinachohudumia Kikosi cha 5 cha Jeshi la Wanamaji la Marekani, “kimeshambuliwa kwa kombora,” kwa mujibu wa taarifa ya Kituo cha Kitaifa cha Mawasiliano cha Bahrain iliyonukuliwa na Shirika la Habari la Taifa la Bahrain (BNA).

    Taarifa hiyo ilisema: “Maelezo zaidi yatatolewa kwa wakati muafaka,” bila kutaja nchi iliyohusika na shambulio hilo.

    Wananchi wamehimizwa kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika na kupata taarifa kutoka vyanzo rasmi pekee.

    Bahrain ni makao makuu ya Kikosi cha 5 cha Jeshi la Wanamaji la Marekani, ambacho eneo lake la uwajibikaji linajumuisha Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Shamu, Bahari ya Arabia na sehemu za Bahari ya Hindi.

    Hakukuwa na tamko la haraka kutoka kwa jeshi la Marekani, ingawa ubalozi wa Marekani hapo awali ulikuwa umeonya raia wake kujisitiri ndani kufuatia taarifa za vitisho vya makombora na ndege zisizo na rubani juu ya Bahrain.

    Soma Pia:

  12. Trump awahimiza Wairan: ‘Chukueni mamlaka ya serikali yenu’

    Rais wa Marekani, Donald Trump, katika ujumbe wake wa video uliotangulia, aliwahimiza wananchi wa Iran kutumia mashambulizi makubwa dhidi ya Iran kama fursa ya kuwaondoa madarakani viongozi wa kidini wanaotawala mjini Tehran.

    “Tutakapomaliza, chukueni serikali yenu, ni yenu kuichukua. Huenda hii ikawa fursa pekee ambayo mmekuwa mkiisubiri kwa muda mrefu,” alitangaza.

    Pia aliwaambia wanachama wa vikosi vya usalama vya Iran kuwa watapewa “kinga” iwapo wataweka silaha chini, la sivyo “watakabiliwa vilivyo.”

    Mapema mwezi Januari, Trump alitishia kuishambulia Iran wakati vikosi vya usalama vilipokuwa vikikandamiza maandamano ya kupinga serikali kote nchini, ambayo kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 6,480. Alionya kuwa waliohusika “watalipa gharama kubwa” na kuwaambia waandamanaji kwamba “msaada unakuja.”

    Hata hivyo, siku chache baadaye rais huyo alisema alipokea uhakikisho kutoka kwa serikali ya Iran kwamba “mauaji yalikuwa yamesimama,” na akaeleza kuwa analenga zaidi mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, ambao umekuwa kiini cha mvutano wa muda mrefu kati ya Iran na mataifa ya Magharibi.

    Soma pia:

  13. Reza Pahlavi awataka Wairan kuchukua maamuzi baada ya shambulio

    Mwana Mfalme wa zamani wa Iran, Reza Pahlavi, amesema katika ujumbe wa video kuwa “wakati wa maamuzi uko mbele yetu.”

    Alisema: “Msaada ambao Rais wa Marekani aliyouahidi watu jasiri wa Iran sasa umefika. Huu ni uingiliaji wa kibinadamu, na lengo lake ni Jamhuri ya Kiislamu, vyombo vyake vya ukandamizaji na mashine yake ya mauaji; siyo taifa kubwa na wananchi wa Iran.”

    Reza Pahlavi ameongeza kuwa: “Licha ya kuwasili kwa msaada huu, ushindi wa mwisho utakuwa wetu.”

    Pia alisema: “Wakati wa kurejea mitaani unakaribia.”

    Mwana Mfalme huyo aliwataka wanajeshi na vikosi vya usalama kujiunga na wananchi wa Iran.

    Aidha, alimwomba Rais wa Marekani, Donald Trump, kuchukua tahadhari za hali ya juu ili kulinda maisha ya raia.

    Soma Pia:

  14. Netanyahu: Utawala wa Iran 'haupaswi kumiliki silaha za nyuklia'

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa utawala wa Iran “haupaswi kumiliki silaha za nyuklia” kwa kuwa ni tishio kwa usalama wa Israel na dunia.

    Akihutubia wananchi wa Israel, Netanyahu alisema:

    “Enyi ndugu zangu, raia wa Israel, muda mfupi uliopita, Israel na Marekani zilianza operesheni ya kuondoa tishio la moja kwa moja linalotokana na utawala wa kigaidi wa Iran.”

    Alimshukuru Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa kile alichokiita uongozi wa kihistoria, akisema kwa miaka 47 utawala wa Ayatollah umekuwa ukipaza sauti kauli za “Kifo kwa Israel” na “Kifo kwa Marekani.”

    Amedai kuwa utawala huo umehusika na umwagaji damu wa Waisraeli, vifo vya Wamarekani na ukandamizaji wa raia wake wenyewe, akiongeza kuwa:

    “Utawala huu wa kigaidi na wauaji haupaswi kupewa silaha za nyuklia ambazo zingeuruhusu kutishia ubinadamu wote.”

    Netanyahu alisema hatua ya pamoja ya Israel na Marekani italeta mazingira yatakayowawezesha wananchi wa Iran “kuchukua hatima yao mikononi mwao.”

    Alitoa wito kwa makundi mbalimbali ya wananchi wa Iran, Waajemi, Wakurdi, Waazeri, Wabaluchi na Waahwazi, kuondokana na kile alichokiita nira ya udikteta na kuijenga Iran huru na yenye amani.

    Kwa wananchi wa Israel, aliwataka kufuata maelekezo ya Kamandi ya Ulinzi wa Ndani, akisema katika siku zijazo za operesheni iliyopewa jina la “Mngurumo wa Simba,” taifa litahitaji uvumilivu na uthabiti.

    “Pamoja tutasimama, pamoja tutapigana, na pamoja tutahakikisha kudumu kwa Israel,” alisema.

    Soma Pia:

  15. Marekani yatoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake wanaoishi Qatar

    Ubalozi wa Marekani mjini Doha, Qatar, umetangaza hatua ya tahadhari ya kujisitiri ndani (shelter-in-place) kwa raia wake wote, huku ukiwashauri raia wa Marekani walioko nchini humo kufanya vivyo hivyo hadi itakapotolewa taarifa nyingine.

    Katika taarifa rasmi kupitia mtandao wa X, ubalozi huo ulisema: "Ubalozi wa Marekani nchini Qatar umeanzisha mpango wa kuhakikisha wafanyikazi wake wote walioko nchini humo wamebaki ndani eneo salama. Tunapendekeza Wamarekani wote wafanye hivyo hadi ilani nyingine itangazwe."

    Raia wa Marekani wametakiwa kutafuta eneo salama ndani ya makazi yao au katika jengo lingine lililo salama, na kuhakikisha wanakuwa na akiba ya chakula, maji, dawa na mahitaji mengine muhimu.

    Pia wamehimizwa kutoshiriki maandamano, kuwa makini na waangalifu wa mazingira yanayowazunguka, na kufuatilia taarifa kadri zinavyochipuka kupitiavyombo vya habari vya ndani.

    Taarifa hiyo imeongeza: “Weka simu yako ikiwa na chaji na udumishe mawasiliano na familia na marafiki ili kuwajulisha hali yako.”

    Aidha, raia wametakiwa kujisajili katika mpango wa Smart Traveler Enrollment Programme (STEP) ili wapokee taarifa za usalama kwa wakati.

    Kwa huduma za dharura nchini Qatar, ubalozi umeelekeza raia kupiga nambari 999.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Katika picha: Hali ilivyokuwa baada ya Iran kushambuliwa asubuhi

    Mashirika ya habari ya Iran yamechapisha picha za milipuko hiyo mjini Tehran.

    Israel na Marekani zazindua mlipuko walioutaja ni wa 'tahadhari' dhidi ya Iran.

  17. Milio ya ving'ora yasikika kote Israel

    Ving'ora vilisikika kote nchini Israel mwendo wa 08:15 saa za ndani (06:15 GMT), kuwatahadharisha watu kuhusu tishio la uwezekano wa shambulio la kombora.

    Mashambulizi ya Israel yanatokea huku kukiwa na juhudi za kidiplomasia kati ya maafisa wa Marekani na Iran kufikia makubaliano ya kukomesha mpango wa nyuklia wa Iran na kuepusha vita, na mazungumzo yalitarajiwa kuendelea wiki ijayo.

    Iran ilifanya makubaliano katika mazungumzo hayo, lakini Rais wa Marekani Donald Trump - ambaye hapo awali alitishia kuishambulia Iran ili kuwashinikiza viongozi wake kukubali makubaliano - alisema jana "hajafurahishwa" na jinsi majadiliano yalivyokuwa yakiendelea.

    Soma pia:

  18. Picha za kwanza zinaonyesha moshi ukifuka mjini Tehran

    BBC imepokea picha za moshi ukifuka mjini Tehran, juu ya Jomhouri Square na Hassan Abad Square