Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Iran yafanya mashambulizi mapya, ndege za Marekani zaanguka Kuwait

Wakati huo huo nchini Lebanon, mshambulizi ya Israel yamewauwa takriban watu 31, wizara ya afya inasema. Israel inasema ilikuwa ikijibu mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na roketi kutoka kwa Hezbollah.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Asha Juma

  1. Watu 153 wameripotiwa kuuawa katika shambulio la shule, Jeshi la Israel lasema “halijui” kuhusu operesheni katika eneo hilo

    Afisa mmoja wa Iran amesema kuwa watu 153 wamefariki baada ya shule ya wasichana katika mji wa Minab kushambuliwa katika mashambulizi ya jana, kulingana na Mizan News Agency inayohusishwa na mahakama ya Iran.

    Afisa mwingine wa Iran alikuwa amesema awali kuwa shule hiyo, iliyoko takribani mita 600 kutoka kituo cha Islamic Revolutionary Guard Corps, ilikuwa imelengwa kwa mashambulizi matatu ya makombora.

    BBC imethibitisha video za tukio hilo, zikionesha moshi ukipaa kutoka kwenye jengo huku umati wa watu ukikusanyika karibu na eneo hilo na sauti za watu wakipiga mayowe kwa hofu zikisikika.

    Hata hivyo, idadi ya waliokufa haijaweza kuthibitishwa kwa uhuru, kwani mara nyingi mashirika ya kimataifa ya habari hukataliwa kuingia Iran, jambo linalozuia kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kukusanya taarifa huko.

    Msemaji wa Israel Defense Forces amesema “hafahamu” operesheni yoyote katika eneo hilo. Ameongeza kuwa pia ameona taarifa kutoka kwa maafisa wa Marekani wakisema wanachunguza tukio hilo.

  2. Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, aonekana kwenye televisheni ya taifa na kusema kuwa nchi hiyo “inaharibu kambi za maadui”

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ameonekana kwenye televisheni ya taifa katika video ambayo inaonekana kuwa ilirekodiwa awali.

    Ametoa pole zake kufuatia kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, na amesema kuwa baraza la uongozi wa muda limeanza kazi yake.

    Kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Iran, Pezeshkian mwenyewe ni sehemu ya kamati ya muda ya watu watatu ambayo imechukua nafasi ili kuepuka mapengo ya uongozi wakati mwili wa viongozi wa kidini wa Iran unapoamua kiongozi mkuu mpya.

    Ripoti zinaonesha kuwa anafanya kazi pamoja na Mohseni Ejehei, kiongozi wa mahakama na Ayatollah Ali Reza Arafi.

    Pezeshkian pia amesema kuwa majeshi ya nchi hiyo yatawapoteza maadui, na kwa sasa wanadondosha "vituo vya maadui".

    Nusu saa kabla ya kuzungumza na taifa, aliandika chapisho kwenye X ambapo alisema kuwa shambulio la hivi karibuni "halitaleta mgawanyiko katika azma ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu kutimiza majukumu yake".

    Pia alisema kuwa "majonzi" kutokana na kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran yataendelea "kubaki katika akili za watu" kwa "muda mrefu".

    Unaweza kusoma;

  3. Nchi za Ghuba zazuilia wimbi jipya la mashambulizi ya Iran

    Bahrain: Mifumo ya ulinzi wa anga ya Bahrain imefanikiwa kudungua na kuharibu wimbi jipya la makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani kutoka Iran, kulingana na vyombo vya habari vya serikali.

    Maafisa waliiambia Shirika la Habari la Bahrain kwamba mabaki machache yalianguka katika maeneo kadhaa.

    Kuwait: Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti kuwa ulinzi wa anga wa Kuwait ulizuia “idadi ya mashambulizi ya anga ” Jumapili asubuhi. Wizara ya ulinzi ya nchi hiyo makombora yalidunguliwa kusini mwa nchi na hakuna vifo vilivyoripotiwa.

    Qatar: Wizara ya ulinzi ya Qatar imesema ndege zake za kivita pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga zilifanikiwa kukabiliana na ndege zisizo na rubani na makombora yaliyorushwa na Iran kuelekea anga ya nchi hiyo, kulingana na Shirika la Habari la Qatar.

    United Arab Emirates: Mwanamke na mtoto walipata majeraha madogo baada ya mabaki ya ndege isiyo na rubani iliyodunguliwa kuanguka kwenye sehemu ya nje ya jengo moja katika Etihad Towers, kulingana na Ofisi ya Habari ya Abu Dhabi.

    Unaweza kusoma;

  4. Nani ni kiongozi mkuu wa kijeshi wa Iran kwa sasa?

    Baada ya vifo vya makamanda kadhaa wakuu wa kijeshi wa Iran katika mashambulizi yaliyofanywa na Marekani na Israel, swali linalojitokeza sasa ni nani anayeshikilia nafasi muhimu ya kijeshi nchini Iran.

    Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Iran, Meja Jenerali Ali Abdollahi. Kwa sasa yeye ni kamanda wa Khatam al-Anbiya, ambayo inaratibu ulinzi wa taifa kati ya jeshi la kawaida na Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC), kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambacho hivi karibuni kilimteua kamanda mpya.

    Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Iran, Abdollahi alikuwa miongoni mwa waliohudhuria maombolezo ya kifo cha Ayatollah Ali Khamenei mjini Tehran leo.

    Amesema kuwa Iran “itajibu vitisho vya maadui kwenye uwanja wa vita” na pia akaeleza “utayari wa majeshi ya ulinzi uko juu zaidi kuliko wakati wowote.”

    Abdollahi aliwekewa vikwazo na Marekani mwezi Januari 2020 pamoja na makamanda wengine wa kijeshi kufuatia mashambulizi ya makombora ya Iran dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq.

    Unaweza kusoma;

  5. Watu wasiopungua tisa wamefariki katika maandamano ya wanaoiunga mkono Iran

    Daktari mmoja mwandamizi katika Hospitali ya umma Karachi aliiambia BBC News kwamba miili tisa na takribani watu 32 waliojeruhiwa walipelekwa hospitalini baada ya mapigano makali na polisi karibu na ofisi ya kibalozi ya Marekani mjini Karachi.

    Mamia ya waandamanaji wanaoiunga mkono Iran waliingia barabarani katika miji ya Karachi, Lahore na Islamabad kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Afisa wa Edhi Foundation, huduma binafsi ya uokoaji, pia alithibitisha kuwa walipeleka miili tisa ya watu waliokufa na makumi ya waliojeruhiwa hospitalini.

    Mapigano yalianza wakati polisi walipojaribu kuwazuia waandamanaji kuingia katika eneo la ubalozi huo. Polisi bado hawajatoa taarifa rasmi kuhusu hali hiyo.

    Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, aliiambia BBC News kwamba ofisi ya Umoja wa Mataifa ilichomwa moto huko Gilgit, katika eneo la Gilgit-Baltistan linalosimamiwa na Pakistan.

    Polisi walithibitisha kuwa amri ya kutotoka nje iliwekwa katika eneo hilo baada ya mamia ya watu kuanza maandamano.

    Mashirika ya Washia yalikuwa yametangaza maandamano katika miji kadhaa, ikiwemo Islamabad.

    Unaweza kusoma;

  6. Milipuko yaripotiwa Doha wakati Iran ikiendelea na mashambulizi ya kulipiza kisasi katika Ghuba ya Kiarabu

    Iran imeanza tena mashambulizi yake ya anga dhidi ya nchi za Ghuba ya Kiarabu, ikilenga makambi ya Marekani kote katika eneo hilo. Tumesikia mlipuko mkubwa asubuhi ya leo huko Doha na moshi mwingi unaonekana kutoka mjini humo.

    Wizara ya mambo ya ndani ilisema ilikuwa ikizima moto mdogo katika eneo la viwandani uliosababishwa na mabaki ya kombora lililopigwa.

    Katika mkutano na waandishi wa habari karibu saa sita usiku, maafisa wa Qatar walisema Iran ilirusha makombora 65 na ndege zisizo na rubani 12 jana, nyingi zilizuiwa, lakini kulikuwa na uharibifu fulani na watu wanane kujeruhiwa kutokana na mabaki ya mlipuko.

    Mlipuko pia umesikika asubuhi hii Dubai na Manama, na shirika la habari la Oman linaripoti shambulizi la ndege isiyo na rubani katika bandari yake ya kibiashara.

    Oman imekuwa mtu muhimu katika mazungumzo ya Marekani na Iran kwa miaka mingi na hadi sasa haijashambuliwa na Iran.

    Qatar na baadhi ya serikali nyingine za Kiarabu zimekemea vikali mashambulizi haya.

    Nchi za Ghuba zimejaribu kupunguza mvutano na Iran katika miaka ya hivi karibuni, zikifanya juhudi kubwa za kuratibu suluhisho la kidiplomasia kwa mgogoro huu na zimekataza Marekani kurusha mashambulizi kutoka kwenye makambi yake katika nchi zao.

    Lakini hayo hayakutosha kuzuia mashambulizi ya moja kwa moja ya kijeshi katika ardhi yao. Na sasa, baada ya kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, mustakabali unaonekana kuwa haujastawi, si tu kwa Iran, bali pia kwa eneo zima.

    Unaweza kusoma;

  7. Takribani maafisa 40 wa Iran wathibitishwa kuuawa na mashambulizi ya Israel na Marekani

    Maafisa kadhaa waandamizi nchini Iran wanajulikana kuuawa katika mashambulizi ya Jumamosi dhidi ya nchi hiyo.

    Miongoni mwao ni:

    • Ayatollah Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Iran, ambaye aliuawa Jumamosi asubuhi katika ofisi yake.
    • Televisheni ya Iran imeripoti kuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo, Abdolrahim Mousavi, aliuawa katika mashambulizi ya anga.
    • Tehran pia imethibitisha kifo cha kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, Jenerali Mohammad Pakpour.
    • Vyombo vya habari vya serikali pia vimeripoti kuwa binti wa Khamenei, mkwe wake na mjukuu wake waliuawa katika shambulizi hilo.
    • Chanzo cha kijasusi na chanzo cha kijeshi vimeiambia CBS News kuwa kwa jumla maafisa wa Iran takribani 40 waliuawa katika mashambulizi hayo.

    Unaweza kusoma;

  8. Kifo cha kiongozi mkuu ni tukio kubwa na Iran inajibu kwa nguvu

    Kuuawa jana kwa mtu ambaye ameiongoza Iran kwa karibu miaka 40 kulithibitishwa usiku na televisheni ya taifa. Hili ni tukio kubwa sana kwa taifa hilo la Kiislamu.

    Kulikuwa na sherehe katika baadhi ya mitaa ya miji ya Iran kutoka kwa watu waliopinga utawala wake. Hali hiyo itazitia moyo Israel na Marekani, ambazo zimewahimiza Wairani kutumia fursa hii kuamka na kuiondoa serikali.

    Usiku kucha, jeshi la Israel lilifanya wimbi jingine la mashambulizi ya mabomu, likisema lililenga hifadhi na vituo vya kurushia makombora ya masafa marefu ya Iran pamoja na mifumo yake ya ulinzi wa anga.

    Zaidi ya watu 200 wameuawa kote Iran, kulingana na Iranian Red Crescent Society, Shirika la misaada ya kibinadamu nchini Iran.

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran limesema litajibu kifo cha Kiongozi Mkuu kwa operesheni yenye uharibifu mkubwa zaidi katika historia yake.

    Asubuhi hii nchini Israel, ving’ora vya tahadhari ya mashambulizi ya anga vimesikika tena huku Iran ikiendelea kurusha makombora ya masafa marefu. Karibu yote yamedunguliwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel.

    Hata hivyo, baadhi yalipenya: mjiniTel Aviv, shambulizi la kombora lilimuua mwanamke mmoja, ambaye ni kifo cha kwanza cha raia wa Israel katika vita hivi. Huduma ya ambulensi imesema watu wengine 120 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa na majeraha madogo.

    Unaweza kusoma;

  9. Habari za hivi punde, Trump asema atatumia 'nguvu ambayo haijawahi kuonekana' Iran ikiwashambulia washirika wa Marekani

    Rais wa Marekani Donald Trump muda mfupi uliopita ameionya Iran kutodhubutu kukabiliana na Marekani na Israel.

    Katika taarifa kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, aliandika, "Iran hivi punde imesema kwamba itafanya mashambulizi makali ambayo hayaijawahi kuonekana. WASIJARIBU KUFANYA HIVYO KWA SABABU WAKIDHUBUTU, TUTAWAKABILI KWA NGUVU AMBAYO HAIJAWAHI KUONEKANA!"

    Kauli yake inakuja baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuonya kuwa litashambulia kazi majeshi ya Marekani na Israel kulipiza kisasi kifo cha Khamenei.

    "Tutaanza operesheni mbaya zaidi ya katika historia ya vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuelekea maeneo yanayokaliwa kimabavu na vituo vya kigaidi vya Marekani muda mfupi ujao," ilisema saa chache zilizopita.

    Melezo zaidi:

  10. Mauaji ya Khamenei yanaweza 'kubadilisha mwelekeo wa taifa' - Reza Pahlavi

    Reza Pahlavi, mtoto wa shah wa mwisho wa Iran (mfalme) aliye uhamishoni nje ya nchi, ametoa taarifa kukaribisha kuunga mkono kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa Irana Ayatollah Ali Khamenei.

    Katika taarifa iliyochapishwa katika gazeti la Washington Post, Pahlavi amemshukuru Rais wa Marekani Donald Trump kwa tamko lake kwa watu wa Iran kwamba "wakati wa uhuru wenu imekaribia".

    Ameongeza kwamba kwa karibu nusu karne, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa "ikipindua mamlaka ya majirani, ikichochea mizozo kote ulimwenguni, na kutafuta silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu ili kuziokoa".

    Anasema uhalifu mkubwa zaidi wa Iran ulifanywa nyumbani, ikiwa ni pamoja na maelfu ya waandamanaji waliouawa wakati wa msako dhidi ya waandamanaji mwezi Januari.

    Pahlavi anasema kwamba mchakato wa nchi kusonga mbele unapaswa kuhusisha katiba mpya iliyoandikwa na kuidhinishwa kupitia kura ya maoni, ikifuatiwa na uchaguzi huru chini ya "uangalizi wa kimataifa", aliandika.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Katika picha: Hisia mseto nchini Iran huku mashambulizi yakiendelea

    Hizi hapa ni baadhi ya picha kutoka ndani ya Iran tunapokaribia saa 24 tangu Israel na Marekani kuishambulia taifa hilo la Mashariki ya Kati.

  12. Rais na wengine wawili kusimamia kipindi cha mpito - Iran yatangaza

    Iran imetangaza kwamba Rais wake, Mkuu wa mahakama, na mmoja wa Wanasheria wa Baraza la Walinzi - chombo chenye nguvu - watasimamia kipindi cha mpito kufuatia kifo cha Ayatollah Ali Khamenei.

    Jopo la Wataalamu wa Uongozi - baraza la maulama - sasa litageukia linatarajiwa kumteua mrithi wa Khamenei, jambo ambalo katiba inasema lazima lifanyike haraka iwezekanavyo.

    Kukufanyika kwa haraka kwa shughuli hiyokw wakati Iran inashambuliwa na Marekani na Israel kunaweza kuwa vigumu kutokana na sababu za kiusalama.

    Khamenei mwenyewe aliteuliwa siku hiyo hiyo Ruhollah Ayatollah Khomeini alipokufa.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Ikiwa ndio mwanzo unajiunga nasi...

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimethibitisha kwamba Kiongozi Mkuu Ali Khamenei ameuawa, katika mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran kutoka ambayo yalianza Jumamosi asubuhi (saa za ndani).

    Haya hapa yaliyojiri kwa mukhtasari:

    • Taarifa ya Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa la Iran, iliyosomwa vyombo kadhaa vya habari vya serikali, imethibitisha kuwa Ayatollah Khamenei aliuawa ofisini kwake mapema Jumamosi asubuhi.
    • Mtangazaji mmoja, alisema nchi itaanza siku 40 za maombolezo huku akitokwa na machozi, .
    • Zaidi ya watu 200 wameuawa wakati wa mashambulizi hayo, kulingana na shirika la Red Crescent, huku CBS News, mshirika wa habari wa BBC ikiripoti kuwa maafisa 40 wa Iran wameuawa.
    • Kujibu mashamblizi hayo, Iran ilifanya msururu wa mashambulizi Mashariki ya Kati, hasa dhidi ya mataifa washirika wa Marekani na ambapo Marekani ina kambi za kijeshi, ikiwa ni pamoja na Dubai, Doha, Bahrain, na Kuwait.
    • Uingereza inashiriki katika "operesheni zilizoratibiwa za ulinzi wa kikanda" kulinda raia wa Uingereza na washirika wa kikanda, Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer amesema.
    • Rais Donald Trump hapo awali alisema Khamenei alikuwa "mmoja wa watu waovu zaidi katika historia" na kwamba kifo chake kilikuwa "fursa kubwa zaidi kwa Wairan kurujirudishia nchi yao". Alisema Marekani itaendelea kuishambulia Iran kwa mabomu - huku milipuko ikiendelea kusikika katika mji mkuu wake Tehran.
    • Marekani haiwezi kutangaza vita bila idhini ya bunge - na operesheni hii imegawanya wabunge, kwa kiasi kikubwa kulingana na vyama.
    • Umoja wa Mataifa pia umesema operesheni hiyo ya kijeshi inadhoofisha amani katika eneo hilo.
  14. Habari za hivi punde, Iran yaonya kuhusu 'mashambulizi mabaya'

    Tumepokea taarifa hivi punde kutoka kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ikionya kwamba watashambulia kambi za Marekani na Israel.

    "Tunajiandaa kufanya operesheni mbaya zaidi ya katika historia ya vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran idhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na vituo vya kigaidi vya Marekani muda mfupi ujao," inasema.

  15. Habari za hivi punde, Televisheni ya taifa ya Iran: Khamenei aliuawa ofisini kwake

    Tukiangazia tena maelezo zaidi taarifa ya Baraza Kuu la Usalama la Iran, iliyosomwa kwenye vituo vya Televisheni vya serikali hapo awali.

    Baraza hilo limesema kuwa Ayatollah Khamenei aliuawa mapema Jumamosi asubuhi katika ofisi yake "alipokuwa akitekeleza majukumu yake".

    Kwa kutumia picha za satelaiti, BBC Verify hapo awali ilithibitisha uharibifu mkubwa wa sehemu za Jumba la Uongozi, ambalo ni ofisi ya Khamenei mjini Tehran.

    Shirika la Habari la Tasnim linalohusiana na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema kwamba kifo cha Khamenei ofisini mwake ni dhibitisho kwamba ripoti kwamba alikuwa akijificha zilikuwa "vita vya kisaikolojia vya adui".

    Soma pia:

  16. Mrithi wa Khamenei hakutajwa kwenye tangazo la kifo chake

    Taarifa kutoka Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, vyombo kadhaa vya habari vya serikali nchini Iran vimethibitisha kifo cha Ayatollah Khamenei.

    Rais wa Marekani Donald Trump saa chache zilizopita alisema Kiongozi Mkuu huyo aliuawa wakati wa shambulio la pamoja na Israel katika maeneo kadhaa kote Iran.

    Katika taarifa hiyo, haikutajwa ni jinsi gani Khamenei mwenye umri wa miaka 86 alivyofariki, au ni nani anayeweza kuchukua nafasi ya kiongozi.

    Jamaa wa Khamenei pia wameuawa katika mashambulizi hayo

    Hapo awali, vyombo vya habari vya serikali vilisema kwamba binti wa Khamenei, mkwewe na mjukuu wake pia waliuawa katika mashambulizi hayo.

    Kulingana na Shirika la Habari la Fars, ambalo lina uhusiano na Kikosi cha Revolutionary Guard, kuna ripoti kwamba mmoja wa mabinti wa Khamenei ameuawa pia.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Habari za hivi punde, Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei ameuawa, televisheni ya serikali imesema

    Televisheni ya taifa ya Iran imethibitisha kuwa Ayatollah Ali Khamenei ameuawa.

    Siku arobaini za maombolezo zatangazwa nchini Iran

    Katika hotuba ya machozi, mtangazaji wa televisheni ya serikali ametangaza kifo cha Khamenei na kusema nchi itaingia katika siku 40 za maombolezo.

    Jamaa za Khamenei pia waliuawa katika mashambullizi hayo.

    Kulingana na Shirika la Habari la Fars ambalo lina mafungamano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kuna ripoti kwamba binti mmoja wa Khamenei ameuawa pia.

    Soma zaidi:

  18. CBS yasema maafisa 40 wa Iran wauawa katika shambulizi

    Chanzo cha habari cha kijasusi na chanzo cha kijeshi kimeambia mshirika wa vyombo vya habari wa BBC, CBS News, kwamba takriban maafisa 40 wa Iran wameuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Haijulikani wazi kama maafisa hao walikuwa katika eneo moja au tofauti.

    Walidai kwamba kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei, alikuwa miongoni mwa waliofariki, pamoja na kamanda wa Kikosi cha Revolutionary na waziri wa ulinzi.

    Iran bado haijathibitisha ripoti zilizoenea kuhusu kifo cha Khamenei.

  19. UAE yalaani shambulio la Iran

    Umoja wa Falme za Kiarabu umelaani mashambulizi ya Iran dhidi ya eneo lake, ukiita ni "ukiukaji wa uhuru wa kitaifa na sheria za kimataifa".

    Katika chapisho kwenye mtandao wa X, UAE inaita hatua ya kulipiza kisasi ya Iran kuwa kuongeza hatari na "kitendo cha uwoga" kinachotishia usalama wa raia na kudhoofisha utulivu.

    Wizara yake ya ulinzi inasema iko " katika tahadhari ya juu" na tayari kukabiliana na vitisho vyovyote.

    Inaongeza kuwa vikosi vyake vya ulinzi vimezuia makombora 137 ya balestiki na ndege zisizo na rubani 209 zilizorushwa kuelekea nchini.

    Kumi na nne kati ya ndege zisizo na rubani zilizoanguka ndani ya maeneo na maji ya nchi hiyo zilisababisha "uharibifu fulani", inasema.

    Pia unaweza kusoma:

  20. Ziara ya Rubio kwenda Israel yafutwa

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio hatasafiri tena kwenda Israel siku ya Jumatatu "kutokana na hali ilivyo kwa sasa", ofisi yake imesema.

    Wizara ya mambo ya nje ilisema jana Rubio alikuwa amepangiwa kwenda Israel kujadili mada mbalimbali, ikiwemo Iran.

    "Kutokana na hali ilivyo kwa sasa, Waziri Rubio hatasafiri tena kwenda Israeli mnamo Machi 2," msemaji anasema.