Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Iran yasema inapendelea mazungumzo, lakini iko tayari kwa vita pia

Mpatanishi mkuu wa upande wa Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ameeleza katika mahojiano na televisheni ya taifa ya nchi hiyo kuwa Tehran haitaacha kujilinda iwapo mazungumzo na Marekani hayatatoa matokeo.

Moja kwa moja

Mariam Mjahid na Lizzy Masinga

  1. Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kuwa kama 'eneo la vita' kwa angalau siku nane zijazo

    Vyama vya wafanyakazi wa meli na makampuni ya usafirishaji vimetangaza leo kwamba Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kuainishwa kama “eneo la operesheni za vita”, uamuzi uliotokana na mashambulizi dhidi ya meli mbili, licha ya kuwepo kwa usitishaji wa mapigano kati ya Iran na Marekani.

    Shirikisho la Kimataifa la Wafanyakazi wa Usafirishaji (International Transport Workers' Federation) na ujumbe wa mazungumzo ya pamoja wa wamiliki wa meli walisema katika taarifa ya pamoja kwamba uamuzi huo unaonesha “hatari kubwa na inayoendelea kwa maisha ya binadamu pamoja na hali inayobadilika kwa kasi katika eneo hilo.”

    Chanzo kilichofahamu mazungumzo hayo kiliiambia AFP kwamba kama meli mbili hazingeshambuliwa katika siku tofauti tangu Alhamisi iliyopita na usafirishaji ungeendelea bila usumbufu, huenda uainishaji huo ungebadilishwa wiki hii.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kuwa “eneo la operesheni za vita” hadi angalau Julai 9, na hali hiyo itapitiwa upya kila wiki.

    Mlango huo uliwekwa rasmi katika hadhi hiyo kwa mara ya kwanza Machi 5, baada ya mashambulizi dhidi ya meli zilizokuwa zikijaribu kupita katika njia hiyo muhimu ya nishati.

    Hali hii inahusu meli zote zilizo chini ya mikataba ya kazi ya International Bargaining Forum, ambazo ni takriban meli 15,000 duniani kote.

    Unaweza kusoma;

  2. Watu watatu wafariki wakati wa sherehe za Kombe la Dunia mjini Mexico City

    Msichana mwenye umri wa miaka 19 ni miongoni mwa watu watatu waliofariki dunia kutokana na kukosa hewa wakati wa sherehe za ushindi katika michuano ya Kombe la Dunia Mexico City siku ya Jumanne.

    Mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka 48 na mwanaume wa miaka 44 pia walifariki baada ya umati mkubwa wa watu kujitokeza mitaani kufuatia ushindi wa Mexico wa mabao 2-0 dhidi ya Ecuador, kwa mujibu wa mamlaka za afya ya mji huo iliyotoa taarifa Jumatano.

    Serikali ya jiji ilisema zaidi ya watu milioni moja walijitokeza mitaani, hasa karibu na mnara wa Angel of Independence katikati mwa jiji, kusherehekea ushindi wa kwanza wa Mexico katika hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia tangu mwaka 1986.

    Meya wa jiji hilo, Clara Brugada, alitoa salamu zake za rambirambi kwa familia za waliofariki na kuahidi kuwapa msaada katika siku zijazo.

    Mamlaka ya afya ilisema wahudumu wa dharura waliwahudumia watu watatu waliokuwa wamepoteza fahamu katika maeneo tofauti kandokando ya barabara ya Paseo de la Reforma kabla ya kuwapeleka hospitalini.

    "Mara baada ya kutoa huduma ya kwanza na kufanya mbinu za kufufua moyo na mapafu (CPR), wagonjwa hao walihamishiwa hospitalini kwa matibabu maalumu," ilisema taarifa ya mamlaka ya afya ya jiji.

    Hata hivyo, watu hao watatu walithibitishwa kufariki dunia kutokana na kukosa hewa, na baadaye walitambuliwa na familia zao.

    Baada ya vifo hivyo kutangazwa, Meya Clara Brugada aliwataka mashabiki kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii "kusherehekea kwa uwajibikaji, tahadhari na kujali wengine kila wakati."

    Unaweza kusoma;

  3. Chris Brown aamriwa kumlipa mfanyakazi wake wa nyumbani dola milioni 13 baada ya kushambuliwa na mbwa

    Mwimbaji wa Marekani Chris Brown amepatikana na hatia na kutakiwa kuwajibika kisheria kwa shambulio la mbwa lililomjeruhi vibaya na kumwacha mfanyakazi wake wa nyumbani akiwa na ulemavu wa kudumu nyumbani kwake mwaka 2020.

    Baada ya kesi iliyodumu kwa wiki mbili mjini Los Angeles, jopo la majaji lilitoa uamuzi kwa manufaa ya Maria Avila, ambaye alishambuliwa na mbwa aina ya Caucasian Shepherd mwenye uzito wa takriban kilo 90, anayemilikiwa na Brown, alipokuwa akimwaga taka nyumbani kwake eneo la Tarzana.

    Brown pamoja na kampuni yake, Black Pyramid LLC, sasa wanatakiwa kumlipa Avila fidia ya dola za Marekani milioni 12.9 kutokana na uzembe, kwa mujibu wa chapisho la Marekani Billboard.

    BBC News imewasiliana na wawakilishi wa Brown ili kupata maoni yao kuhusu uamuzi huo.

    Avila alisema mbwa huyo, anayeitwa Hades, alimnyofoa vipande vikubwa vya ngozi yake, jambo lililosababisha uharibifu wa kudumu wa uso, makovu, kupoteza uwezo wa kuona kwa kiwango fulani na kuharibika kwa mishipa ya fahamu.

    Brown alidai kuwa mbwa huyo alikuwa akifugwa kwa madhumuni ya ulinzi wa nyumba na hakuwa mnyama wake wa kufugwa binafsi.

    Wakati wa kesi hiyo, mahakama ilisikia ushahidi ulioonesha kuwa badala ya kupiga simu kwa huduma za dharura au kumsaidia Avila mwenyewe baada ya shambulio, Brown aliondoka eneo la tukio, kwa mujibu wa Rolling Stone.

    Majaji pia walielezwa kuwa Brown aliwaacha wafanyakazi wake wamuhudumie Avila, akisema aliogopa kuwapo kwake au sauti yake kusikika kwenye simu ya dharura ya 911 kungesababisha "msisimko mkubwa wa vyombo vya habari" polisi walipowasili.

    Chris Brown alisema alikuwa anajiandaa kuoga alipomsikia mbwa akinguruma, ndipo akashuka chini na kumkuta Maria Avila akiwa amelala bila kutikisika na akiwa ametapakaa damu nyingi.

    "Kuona damu nyingi kulinishtua sana," alisema, akiongeza kuwa alikuwa katika hali ya mshtuko alipoamua kufuata ushauri wa meneja wake wa kuondoka eneo la tukio kabla ya wahudumu wa dharura kufika.

    Brown alikiri kuwa alikuwa na sehemu ya kuwajibika kabla ya kesi kuanza, lakini alipinga kiwango cha majeraha aliyopata Avila na kudai kuwa Avila pia alikuwa na mchango katika kutokea kwa tukio hilo.

    Mwimbaji huyo alisema alikuwa amewaonya dada hao wawili waliokuwa wafanyakazi wa nyumbani kuwa mbwa hao "hawakuwa kabisa wa kirafiki", na aliwaambia watoke nje ya nyumba tu pale walinzi walipokuwa wamefika.

    Hata hivyo, wafanyakazi hao wawili walikanusha kuwa kuliwahi kufanyika mazungumzo kati yao na Brown, wakisema pia kuwa tofauti ya lugha ilifanya mazungumzo ya aina hiyo kuwa kutofanyika kwa urahisi.

  4. Amnesty International yasema RSF ilitenda uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini Sudan

    Kundi la kutetea haki za binadamu limesema kuwa wanamgambo wa Sudan walifanya uhalifu dhidi ya ubinadamu na utakasaji wa kikabila wakati wa kampeni yao ya kuuteka mji wa El-Fasher mwaka jana.

    Kuzingirwa na kutekwa kwa mji huo ulioko katika eneo la magharibi la Darfur kulikuwa miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya umwagaji damu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, vinavyopiganwa kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha Rapid Support Forces (RSF).

    Katika ripoti ya uchunguzi iliyotolewa Jumatano, Amnesty International ilisema:

    "Uhalifu uliofanywa na RSF ulijumuisha mauaji, kuwahamisha watu kwa nguvu, kuwafunga bila sababu za kisheria, mateso, ubakaji, utumwa wa kingono, aina nyingine za ukatili wa kingono, utumwa, mauaji ya halaiki, na mateso kwa misingi ya utambulisho."

    RSF haijasema chochote kuhusu ripoti hiyo ya Amnesty, lakini hapo awali ilikanusha tuhuma kama hizo.

    Sudan bado imo katika mapambano ya madaraka yaliyodumu kwa miaka mitatu kati ya jeshi la kawaida la nchi hiyo na wanamgambo wa RSF. Vita hivyo vimeua mamia ya maelfu ya watu na kuwalazimisha zaidi ya watu milioni 14 kuyakimbia makazi yao.

    Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ukatili wa kingono dhidi ya wanaume, wanawake na watoto unatumiwa kama silaha ya vita.

    Pande zote mbili, RSF na Sudanese Armed Forces (SAF) zimeshutumiwa kwa kufanya uhalifu wa kivita, ingawa zote zimekanusha tuhuma hizo.

    Baada ya kufukuzwa kutoka mji mkuu, Khartoum, mwezi Machi mwaka jana, RSF ilielekeza nguvu zake katika kuimarisha udhibiti wake wa eneo la magharibi la Darfur kwa kuuteka mji wa El Fasher, pamoja na kupanua ushawishi wake katika majimbo ya Kordofan yaliyoko kusini mwa nchi.

    Unaweza kusoma;

  5. Iran yatangaza likizo ya umma ili kujiandaa kwa mazishi ya Khamenei

    Serikali ya Iran imetangaza Jumanne, Julai 6, kuwa siku ya mapumziko ya umma mjini Tehran.

    Msemaji wa serikali ya Iran, Fatima Mohajerani, amesema hatua hiyo inalenga kuwezesha waombolezaji wa kiongozi wa zamani wa Iran kurejea kutoka mji mkuu.

    Pia amesema siku ya maombolezo ya kitaifa itaadhimishwa nchini Iran siku ya Alhamisi, huku mazishi ya Ali Khamenei yakitarajiwa kufanyika mjini Mashhad Julai 8.

    Kwa mujibu wa ratiba rasmi, sala za mazishi na shughuli za kuaga mwili wa Khamenei zitafanyika kati ya Julai 4 na 8 katika miji ya Tehran, Qom na Mashhad. Hafla za kutoa pole pia zitafanyika katika miji ya Baghdad, Kazmin, Karbala na Najaf nchini Iraq.

    Inakumbukwa kuwa Ali Khamenei aliuawa katika mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyolenga makazi na ofisi yake, maarufu kama Nyumba ya Uongozi, lakini hadi sasa bado hajazikwa.

    Unaweza kusoma;

  6. Mvulana wa miaka mitatu aokolewa akiwa hai siku sita baada ya tetemeko la ardhi Venezuela

    Mvulana mwenye umri wa miaka mitatu ameokolewa akiwa hai kutoka chini ya vifusi siku sita baada ya matetemeko makubwa ya ardhi yaliyolikumba Venezuela, timu ya uokoaji kutoka Jordan imesema.

    Mtoto huyo, aliyetambuliwa kwa jina la Klieber Morán, aliokolewa kutoka kwenye vifusi katika jimbo la La Guaira, kwa mujibu wa Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, ambaye alieleza uokoaji huo kuwa "chanzo cha matumaini kwa watu wetu."

    Tukio hilo limejiri huku Umoja wa Mataifa ukionya kwamba makumi ya maelfu ya watu wanahitaji kwa dharura chakula na makazi.

    Idadi ya vifo kutokana na matetemeko ya ardhi ya wiki iliyopita, yaliyokuwa na ukubwa wa 7.2 na 7.5, imefikia watu 1,943, huku zaidi ya watu 10,000 wakijeruhiwa na makumi ya maelfu wengine wakiwa hawajulikani waliko.

    Kwa mujibu wa tathmini ya awali ya data za satelaiti za NASA, matetemeko hayo huenda yaliharibu au kubomoa majengo 58,870.

    Idara ya Ulinzi wa Raia ya Jordan ilisema Klieber alipatiwa huduma ya kwanza, akapelekwa hospitalini na hali yake ilikuwa nzuri. Anaendelea kupatiwa matibabu katika mji mkuu, Caracas.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema upungufu wa chakula umeenea, huduma za msingi zimevurugika na mawasiliano mengi yamekatika katika jimbo la La Guaira.

    "Mvutano ndani ya jamii unaongezeka huku upatikanaji wa misaada ukiendelea kuwa mgumu," UNHCR ilisema katika taarifa yake.

    Soma Zaidi:

  7. Bilionea wa China ahukumiwa miaka 30 jela Marekani kwa ulaghai wa dola bilioni moja

    Guo Wengui, ambaye wakati mmoja aliaminika kuwa miongoni mwa watu matajiri zaidi nchini China, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela nchini Marekani kwa kuendesha ulaghai wa zaidi ya dola bilioni moja.

    Bilionea huyo wa zamani wa sekta ya mali isiyohamishika alikimbilia Marekani mwaka 2017, ambako alijijenga upya kama mkosoaji wa Chama cha Kikomunisti cha China na kupata wafuasi wengi mtandaoni.

    Hata hivyo, baadaye alipatikana na hatia ya makosa ya uhalifu wa kupangwa, ulaghai na utakatishaji fedha.

    Jaji wa New York, Analisa Torres, alisema Guo aliwalaghai watu waliokuwa wakitafuta kuleta demokrasia nchini China na kutumia fedha zao kugharimia maisha yake ya anasa.

    Wakili wake, Melinda Sarafa, alisema hukumu hiyo ni kali kupita kiasi na haikuzingatia maelfu ya wawekezaji wake ambao wanasema hawakulaghaiwa.

    Guo amesisitiza kuwa hana hatia na atakata rufaa dhidi ya hukumu na adhabu hiyo.

    Mwanasheria wa serikali ya Marekani, Sean Buckley, amesema:

    "Hukumu ya leo inaonyesha kuwa umaarufu na utajiri haviweki mtu juu ya sheria, na walaghai wanaowaathiri wengine ili kujinufaisha watakabiliwa na madhara makubwa."

    Kabla ya kuondoka China, Guo alijijengea utajiri mkubwa kupitia biashara za mali isiyohamishika na alikuwa na uhusiano mzuri na serikali ya China.

    Hata hivyo, aliomba hifadhi nchini Marekani baada ya kutuhumiwa na maafisa waandamizi wa China kwa ufisadi.

  8. Iran yasema inapendelea mazungumzo, lakini iko tayari kwa vita pia

    Mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Iran na Marekani yanaendelea huku Iran ikisisitiza kuwa, pamoja na kuipa kipaumbele njia ya mazungumzo, bado iko tayari kurejea vitani ikiwa juhudi hizo zitashindwa.

    Hayo yameelezwa na mpatanishi mkuu wa upande wa Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ambaye alisema katika mahojiano na televisheni ya taifa kuwa Tehran haitaacha kujilinda iwapo mazungumzo hayatatoa matokeo.

    "Tunafuata njia ya mazungumzo, lakini ikiwa mazungumzo hayatatekelezwa, pia tuko tayari kwa vita na tutajibu ipasavyo," alisema Ghalibaf.

    Kauli hiyo ilitolewa wakati wajumbe wa Iran na Marekani walipokuwa wakitarajiwa kufanya mazungumzo mengine mjini Doha, yakilenga kupunguza mvutano na kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro uliodumu kwa miezi kadhaa.

    Mvutano huo uliongezeka mwezi Juni 2026, baada ya mashambulizi ya kijeshi kati ya Iran na Israel, yaliyohusisha pia mashambulizi ya Marekani dhidi ya baadhi ya maeneo ya nyuklia ya Iran. Baada ya siku kadhaa za mapigano, pande husika zilikubaliana kusitisha mapigano kwa muda ili kutoa nafasi kwa juhudi za kidiplomasia.

    Ingawa mapigano yamesitishwa kwa sasa, bado hakuna makubaliano ya kudumu yaliyofikiwa.

  9. Kombe la Dunia: Ivory Coast yaaga, Afrika yasalia na timu saba

    Ivory Coast imekuwa timu ya pili ya Afrika kuondolewa katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia baada ya kufungwa mabao 2-1 na Norway, na kuziacha timu saba za bara hilo zikiendelea na harakati za kutinga hatua ya 16 bora.

    Kuondolewa kwa Ivory Coast kunaiunganisha na Afrika Kusini, ambayo iliaga hatua hiyo mapema, huku Tunisia ikiwa ilitolewa katika hatua ya makundi.

    Katika mechi nyingine zilizochezwa usiku wa kuamkia leo, Ufaransa ilitinga hatua ya 16 bora baada ya kuichapa Sweden mabao 3-0, wakati Mexico nayo ilifuzu kwa kuishinda Ecuador mabao 2-0, asubuhi hii.

    Sasa matumaini ya Afrika yapo kwa timu saba zilizobaki kwenye mashindano hayo.

    Usiku wa leo saa moja usiku, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itavaana na England, huku saa tano usiku Senegal ikikabiliana na Ubelgiji kuwania nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora.

    Ratiba ya Ijumaa inaonyesha Algeria ikicheza dhidi ya Uswisi, wakati Misri itavaana na Australia.

    Maelezo zaidi:

  10. Marekani yaombwa kuangalia upya uhusiano wake na Uganda

    Baada ya kufungwa kwa vyombo vya habari Seneta wa Marekani, Jim Risch, ametaka kufanyika kwa mapitio ya uhusiano wa kiusalama kati ya Washington na Uganda.

    Risch, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Marekani inayoshughulikia Masuala ya Nje, amesema Uganda huenda isiwe mshirika anayefaa kufuatia kufungwa kwa baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni kwa agizo lililoidhinishwa na Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Muhoozi Kainerugaba.

    “Marekani inahitaji kupitia upya uhusiano wake wa kiusalama na Uganda. Mashambulizi ya Jenerali Muhoozi Kainerugaba dhidi ya uhuru wa kujieleza, yakiwemo ya kufunga taasisi kubwa za habari mwishoni mwa wiki hii, yanamfanya yeye pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda kuwa washirika wasiofaa.''

    Tunapaswa kushirikiana tu na wale wanaoimarisha usalama wa kikanda, si wanaoudhoofisha,” Risch aliandika kwenye ujumbe wake katika mtandao wa X almaarufu Twitter.

    Soma zaidi:

  11. Trump aingiza zaidi ya dola bilioni moja kutokana na sarafu za kidijitali tangu arejee madarakani

    Rais wa Marekani Donald Trump aliingiza zaidi ya dola bilioni moja kupitia shughuli zinazohusiana na sarafu za kidijitali mwaka jana, kwa mujibu wa ripoti yake ya lazima ya mwaka 2025 ya kutangaza mali zake.

    Katika ripoti hiyo yenye kurasa 927, Trump amesema alipata dola milioni 635 kutokana na mrabaha wa sarafu ya kidijitali ya Trump meme coin, ambayo thamani yake imeshuka kwa kiasi kikubwa tangu ilipozinduliwa siku tatu kabla ya kuapishwa kwake.

    Pia amesema alipata zaidi ya dola milioni 500 kutoka World Liberty Financial, kampuni ya sarafu za kidijitali iliyoanzishwa na wanawe pamoja na watoto wa mjumbe wake maalum wa Mashariki ya Kati, Steve Witkoff.

    Mbali na hilo, Trump alipata mamilioni ya dola kupitia biashara za mali isiyohamishika na bidhaa zinazobeba jina la Trump.

    Hata hivyo, Ikulu ya White House imekanusha kuwa Trump ananufaika kifedha kutokana na urais wake.

    Mapato yaliyoorodheshwa katika ripoti hii mpya ni makubwa zaidi kuliko yale aliyotangaza mwaka 2024, aliposema alikuwa ameingiza zaidi ya dola milioni 600.

    White House pia ilikanusha kuwapo kwa mgongano wa maslahi, ikisema Trump alihamishia biashara zake kwenye mfuko wa amana unaosimamiwa na wanawe.

    Naibu msemaji wa White House, Anna Kelly, amesema rais huyo ameifanya Marekani kuwa "kitovu cha dunia cha sarafu za kidijitali."

  12. Hujambo natumai umzima.