Mvulana wa miaka mitatu aokolewa akiwa hai siku sita baada ya tetemeko la ardhi Venezuela

Chanzo cha picha, Jordan Public Security via Reuters
Mvulana mwenye umri wa miaka mitatu ameokolewa akiwa hai kutoka chini ya vifusi siku sita baada ya matetemeko makubwa ya ardhi yaliyolikumba Venezuela, timu ya uokoaji kutoka Jordan imesema.
Mtoto huyo, aliyetambuliwa kwa jina la Klieber Morán, aliokolewa kutoka kwenye vifusi katika jimbo la La Guaira, kwa mujibu wa Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, ambaye alieleza uokoaji huo kuwa "chanzo cha matumaini kwa watu wetu."
Tukio hilo limejiri huku Umoja wa Mataifa ukionya kwamba makumi ya maelfu ya watu wanahitaji kwa dharura chakula na makazi.
Idadi ya vifo kutokana na matetemeko ya ardhi ya wiki iliyopita, yaliyokuwa na ukubwa wa 7.2 na 7.5, imefikia watu 1,943, huku zaidi ya watu 10,000 wakijeruhiwa na makumi ya maelfu wengine wakiwa hawajulikani waliko.
Kwa mujibu wa tathmini ya awali ya data za satelaiti za NASA, matetemeko hayo huenda yaliharibu au kubomoa majengo 58,870.
Idara ya Ulinzi wa Raia ya Jordan ilisema Klieber alipatiwa huduma ya kwanza, akapelekwa hospitalini na hali yake ilikuwa nzuri. Anaendelea kupatiwa matibabu katika mji mkuu, Caracas.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema upungufu wa chakula umeenea, huduma za msingi zimevurugika na mawasiliano mengi yamekatika katika jimbo la La Guaira.
"Mvutano ndani ya jamii unaongezeka huku upatikanaji wa misaada ukiendelea kuwa mgumu," UNHCR ilisema katika taarifa yake.




















