Kwa nini nchi hii hujikuta kitovu cha vita mara kwa mara?

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Ukitaja neno Beirut mbele ya Mkenya, huenda jambo la kwanza linalomjia akilini si vita, bali ni jina la mkahawa.

Kutoka katikati ya jiji la Nairobi hadi miji mingine ya Afrika Mashariki, ni rahisi kukutana na migahawa inayobeba jina hilo. Kwa wengi, Beirut ni jina linalohusishwa na chakula kitamu, burudani na mahali pa kukutana na marafiki.

Lakini ni nini kuhusu mji huu wa Mashariki ya Kati ambao umeufanya usafiri maelfu ya kilomita na kujipenyeza katika maisha ya kila siku ya Afrika Mashariki?

Karibu kila mtu aliyewahi kutembelea Beirut husimulia hadithi inayofanana. Husema ni mji wenye chakula cha kipekee, maisha ya usiku yasiyolala na nguvu ya ajabu inayoufanya uendelee kupumua hata baada ya maafa makubwa. Beirut ni mji unaokataa kutambulishwa kwa vita pekee, licha ya kuishi kwa miongo mingi chini ya kivuli cha migogoro.

Nimekuwa nikitamani kwenda mji huu. Siyo tu kwa sababu ya uzuri wake wa Bahari ya Shamu au mchanganyiko wake wa tamaduni, dini na historia, bali pia kwa sababu Beirut ni mahali pa nadra duniani ambapo furaha na huzuni huonekana kutembea bega kwa bega.

Lakini kwa sasa, siwezi kwenda. Kisa? Historia imejirudia tena.

Baada ya mivutano kati ya Marekani na Iran kuongezeka miezi michache iliyopita, Lebanon nayo ilijikuta tena katikati ya dhoruba. Makombora yalivuka mipaka, Hezbollah na Israel wakarushiana mashambulizi, na milipuko ikafika Beirut, mji ambao haujaacha kuhesabu majeraha yake tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe, uvamizi wa kigeni na migogoro ya kikanda.

Ni kana kwamba kila kipindi Mashariki ya Kati inapowaka moto, Beirut hulazimika kubeba sehemu ya majivu yake.

Hivyo basi, swali lisiloepukika ni hili,Kwa nini Lebanon, hujikuta ikivutwa mara kwa mara katika vita ambavyo mara nyingi huanza nje ya mipaka yake?

Jiografia yake ni changamoto yenyewe

Ukiangalia ramani utaona kuwa Lebanon ni nchi ndogo sana. Unaweza kuisafiri kutoka upande mmoja hadi mwingine kwa chini ya saa mbili kwa gari.

Iko kwenye pwani ya Bahari ya Shamu, jambo ambalo limeifanya kuwa kitovu muhimu cha biashara kwa karne nyingi. Pia imekuwa lango la kuingia katika ulimwengu wa Kiarabu kwa yeyote aliyekuwa akitaka ushawishi katika eneo hilo.

Kaskazini na mashariki mwa Lebanon kuna Syria. Kusini kuna Israel.

Kwa hali hiyo, hakuna mpaka ambao ni rahisi au usio na migogoro.

Makombora yanaporushwa kutoka kusini mwa Lebanon yanaweza kufika katika miji ya kaskazini mwa Israel ndani ya dakika chache. Na Israel inapojibu kwa mashambulizi ya anga au ya ardhini, Lebanon haina maeneo ya ndani yaliyo mbali vya kutosha kutoa usalama.

Nchi nzima huwa katika hatari.

Lakini jiografia pekee haiwezi kueleza tatizo hilo.

Mfumo wa kisiasa wenye migawanyiko ya kidini

Mwaka 1920, Ufaransa iliunda Lebanon kutoka eneo lililokuwa sehemu ya Syria chini ya Milki ya Ottoman.

Mipaka iliwekwa kwa namna iliyojumuisha makundi mengi ya kidini, yakiwemo Wakristo wa Maronite, Waislamu wa Sunni, Waislamu wa Shia, Wadruze, Wakristo wa Orthodox ya Ugiriki na jumuiya nyingine nyingi za kidini zinazotambuliwa rasmi.

Lebanon ilipopata uhuru mwaka 1943, viongozi wake walikubaliana kugawana madaraka kwa misingi ya dini.

Rais alipaswa kuwa Mkristo wa Maronite. Waziri Mkuu alipaswa kuwa Mwislamu wa Sunni. Spika wa Bunge alipaswa kuwa Muislamu wa Shia.

Tatizo lilikuwa kwamba mgawanyo huo ulitegemea sensa ya watu ya mwaka 1932. Kadiri idadi ya watu ilivyobadilika kwa miaka iliyofuata, mfumo haukubadilishwa.

Kufikia miaka ya 1970, jamii ya Washia iliaminika kuwa kubwa zaidi nchini, lakini bado haikuwa na nguvu kubwa kisiasa.

Hakukuwa na utaratibu rahisi wa kurekebisha mfumo huo bila kuibua migogoro mipya.

Mfumo huo ulijulikana kama confessionalism yaani ni mfumo wa kisiasa au wa kugawana madaraka ambapo nyadhifa za serikali na uwakilishi wa kisiasa hugawanywa kulingana na makundi ya dini au madhehebu ya kidini yaliyopo nchini.

Kutokana na mgawanyiko huo wa ndani, mataifa ya nje hayakuhitaji kuivamia Lebanon moja kwa moja ili kupata ushawishi.

Yalihitaji tu kupata kundi la ndani ambalo lingekuwa mshirika wao.

Kwa sababu kila kundi lilikuwa likitafuta msaada wa kulinda maslahi yake, mara nyingi kulikuwa na washirika wa kupatikana.

Israel na Hezbollah

Ili kuelewa Lebanon ya leo, ni vigumu kutenganisha historia ya Israel na Hezbollah.

Baada ya kuanzishwa kwa Israel mwaka 1948 na vita vilivyofuata, takribani wakimbizi wa Kipalestina 100,000 walikimbilia Lebanon. Wengi wao waliishi katika kambi kusini mwa nchi.

Mwaka 1970, baada ya kuondolewa Jordan, Shirika la Ukombozi wa Palestina (PLO), ilihamishia shughuli zake za kijeshi kusini mwa Lebanon. Hilo lilifanya Israel kuona tishio jipya kwenye mpaka wake wa kaskazini.

Mwaka 1978 na tena mwaka 1982, Israel ilivamia Lebanon.

Uvamizi wa mwaka 1982 ulifika hadi Beirut, na baadaye Israel ilidhibiti kusini mwa Lebanon kwa takribani miaka 18.

Katika kipindi hicho, ndani ya vijiji vya Washia kusini mwa nchi, harakati mpya ilizaliwa.

Harakati hiyo iliitwa Hezbollah, yaani "Chama cha Mungu".

Hezbollah ilianzaje?

Baada ya uvamizi wa Israel mwaka 1982, Iran ilituma wanamgambo wa Kikosi cha Mapinduzi ya Kiislamu katika Bonde la Beqaa nchini Lebanon.

Walipata uungwaji mkono kutoka kwa Washia waliokuwa wamehamishwa makwao na waliojiona kutengwa kisiasa.

Iran ilitoa fedha, mafunzo, silaha na itikadi ya mapambano ya Kiislamu.

Lakini Hezbollah haikuwa tu kundi la kijeshi.

Ilijenga shule, hospitali na mifumo ya ustawi wa jamii katika maeneo ambayo serikali ya Lebanon ilikuwa haijatoa huduma za kutosha.

Ndiyo sababu sehemu ya Washia wa Lebanon bado wanaendelea kuiunga mkono.

Mwaka 2000, Hezbollah ilisaidia kushinikiza kuondoka kwa majeshi ya Israel kutoka kusini mwa Lebanon.

Mwaka 2006, ilipigana tena na Israel katika vita vya siku 33 vilivyosababisha uharibifu mkubwa lakini havikuzaa ushindi wa wazi kwa upande wa Israel.

Kwa baadhi ya Walebanon, huo ulikuwa ushahidi kwamba kulikuwa na nguvu iliyokuwa tayari kuwalinda.

Lebanon ya leo

Katika miaka ya karibuni, mapigano kati ya Israel na Hezbollah yameendelea mara kwa mara.

Kuanzia mwaka 2024, mashambulizi yaliongezeka. Viongozi wa Hezbollah waliuawa, maelfu ya watu walijeruhiwa au kuuawa, na mamia ya maelfu walilazimika kuhama makazi yao.

Makubaliano mbalimbali ya kusitisha mapigano yalifikiwa, lakini masuala makubwa kama uwepo wa Hezbollah, usalama wa mpaka na uondoaji wa majeshi kutoka maeneo yenye migogoro yaliendelea kuwa chanzo cha mvutano.

Lakini kwa nini Lebanon huendelea kuathirika na vita?

Jibu fupi ni kwamba Lebanon iko katikati ya migogoro mingi inayokutana mahali pamoja.

Ni nchi ndogo yenye mipaka nyeti

Ina mfumo wa kisiasa unaotegemea usawa wa makundi ya kidini.

Imekuwa uwanja wa ushindani wa kikanda kati ya Iran, Israel, Saudi Arabia na mataifa mengine.

Imepokea mamilioni ya wakimbizi kwa vipindi tofauti. Na migogoro ya ndani haijawahi kutatuliwa kikamilifu.

Kwa sababu hiyo, kila mgogoro mkubwa katika Mashariki ya Kati una uwezekano wa kuigusa Lebanon kwa njia moja au nyingine.

Kama alivyowahi kusema mchambuzi wa masuala ya kimataifa aliyewahi kutembelea Beirut, hali ni ngumu zaidi kuliko inavyoonekana na hadithi zake hazina majibu rahisi.

Huenda hiyo ndiyo njia bora ya kuielezea Lebanon. Ni nchi yenye historia tata, changamoto nyingi na uwezo wa ajabu wa kuendelea kusimama licha ya misukosuko isiyoisha.