Afrika Kusini na Ghana zakumbwa na mvutano wa kidiplomasia kuhusu mauaji ya raia wa Ghana
Mvutano wa kidiplomasia umeibuka kati ya Afrika Kusini na Ghana kufuatia madai kwamba raia wa Ghana aliuawa wakati wa maandamano dhidi ya wahamiaji, madai ambayo maafisa wa Afrika Kusini wameyakanusha.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana ilisema imepokea kwa "mshtuko mkubwa" taarifa kwamba Bashiru Isak, mwenye umri wa miaka 40, alipigwa risasi na kuuawa Jumanne katika mtaa wa Khayelitsha. Wizara hiyo ilisema imetuma barua rasmi ya malalamiko na pia imewasilisha taarifa kwa polisi.
Kwa upande wake, Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini alieleza wasiwasi wake kwamba mamlaka za Ghana zinaendelea kusambaza taarifa zisizo sahihi kuhusu Afrika Kusini kuhusiana na suala la uhamiaji haramu.
Polisi wa Afrika Kusini walisema hawana rekodi yoyote ya mauaji yaliyotokea Khayelitsha kama yalivyoelezwa na Ghana.
Hata hivyo, walithibitisha kuwa wanachunguza mauaji ya raia mwingine wa Ghana, Kwabena Boagen, mwenye umri wa miaka 35, aliyeuawa siku moja kabla katika eneo la Nyanga, katika tukio linalohusishwa na uhalifu wa ulaghai wa fedha za ulinzi.
Polisi walisema Boagen alikuwa akiishi Khayelitsha lakini alikuwa akifanya kazi Nyanga, ambako mauaji hayo yalitokea. Pia walieleza kuwa uchunguzi wa maiti unaendelea kwa mujibu wa taratibu zao.
Awali, polisi waliiambia BBC kuwa watu wanaoshukiwa waliingia mahali ambako Boagen alikuwa akifanya kazi, wakamtaka awape fedha, na baadaye wakampiga risasi kabla ya kutoroka. Hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Wakirejea taarifa ya mamlaka za Ghana, polisi wa Afrika Kusini walitoa wito kwa mamlaka hizo kutoa maelezo zaidi kuhusu tukio linalodaiwa kutokea Khayelitsha ili uchunguzi uweze kufanyika kikamilifu.
Unaweza kusoma;