Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Raila Odinga na William Ruto katika ushindani mkali

Iliyochapishwa

Huku takriban nusu ya matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Kenya yakiwa yamethibitishwa, wagombea wawili wakuu wamekabana koo.

Naibu Rais William Ruto amechukua uongozi kidogo dhidi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga - 51% dhidi ya 48%.

Mkuu wa tume ya uchaguzi amekiri kwamba utangazaji wa matokeo ya uchaguzi wa Jumanne unaendelea polepole.

Uhakiki wa matokeo umesitishwa mara kadhaa baada ya malalamiko kutoka kwa wafuasi na wagombea wakuu.

Jumamosi usiku, wafuasi wa Bw Odinga waliingia katika eneo lililozuiliwa na kuwashambulia maafisa wa uchaguzi, wakiwashutumu kwa kuvuruga kura.

Huku kukiwa na ghasia hizo, meneja mkuu wa kampeni za Bw Odinga aliweza kufika kwenye jukwaa lililotumiwa na maafisa wakuu wa tume ya uchaguzi, ambako alikosoa mchakato wa kuhakiki matokeo.

"Nataka kutangaza kwa taifa kwamba Bomas of Kenya ni eneo la uhalifu," alisema Saitabao Ole Kanchory, kabla ya kipaza sauti kuzimwa na kuchukuliwa''.

Bomas ni jina la kituo cha kitamaduni katika mji mkuu, Nairobi, ambacho kinatumika kama kituo kikuu cha kuhesabia kura.

Wafuasi wa Bw Ruto walishutumu wapinzani wao kwa kuingilia mchakato wa kujumlisha kura.

Polisi wa kutuliza ghasia wametumwa ndani ya jengo hilo ili kuimarisha usalama.

Kumekuwa na wito wa amani kutoka kwa viongozi na vyombo kadhaa likiwemo kanisa katoliki ambalo liliomba "uvumilivu na ustaarabu" na kuwataka wagombea wakuu "kujizuia na kuonesha ustaarabu" huku wasiwasi ukiongezeka.

"Nataka kuwa chombo cha kuleta amani, kuponya, kuunganisha na kudumisha matumaini katika nchi yetu," Bw Odinga alisema Jumapili asubuhi kwenye ibada ya kanisa jijini Nairobi, ikiwa ni matamshi yake ya kwanza kwa umma tangu siku ya uchaguzi.

Matokeo ya majimbo 141 kati ya 292 sasa yamethibitishwa, kwa mujibu wa ripoti ya BBC ya matangazo rasmi.

Mashirika ya habari yamekuwa yakitoa hesabu za muda kwa kutumia data rasmi kutoka kwa vituo 46,000 vya kupigia kura. Pia hesabu zao zinaonyesha ushindani mkali kati ya wagombea hao wawili.

Takriban kura milioni 14 zilipigwa - waliojitokeza kupiga kura ni 65%.

Tume ya uchaguzi ina hadi Jumanne tarehe 16 Agosti kutangaza mshindi.

"Lazima tufanye mabadiliko" ili kuharakisha mchakato wa kuhakiki matokeo, mkuu wa baraza la uchaguzi Wafula Chebukati alisema katika mkutano wake wa hivi wa leo.

"Inachukua saa tatu hadi nne" kushughulikia matokeo kutoka eneo bunge moja, alisema. "Baadhi ya maafisa wetu wanaorejea wamekaa hapa kwa siku tatu wakiwa wameketi kwenye viti, jambo ambalo halikubaliki kabisa."

Ni nini kinaendelea katika kituo kikuu cha kuhesabia kura?

Maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) bado wanashughulika na uhakiki wa matokeo katika kituo kikuu cha Bomas.

Wasimamizi wa uchaguzi wanalinganisha picha za fomu za matokeo kutoka vituo vya kupigia kura na fomu halisi ambazo maafisa wameleta kituoni ili kuhakikisha matokeo yanalingana.

Jitihada hizi kuu zimemfanya Bw Chebukati kuwashutumu maajenti kutoka vyama vikuu vinavyoshuhudia mchakato huo kwa kubadili zoezi la moja kwa moja kuwa la "uchunguzi".

Wakenya wanajisikiaje?

Kuna hali ya wasiwasi nchini kwani chaguzi zilizozozaniwa huko nyuma zilisababisha vurugu au mchakato mzima kufutwa.

Viongozi na mashirika kadhaa mashuhuri wamekuwa wakitoa wito wa uvumilivu na kuwataka Wakenya kudumisha amani.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Anthony Muheria amesema yeyote ambaye atatangazwa kuwa mshindi anapaswa "kukubali ushindi kwa heshima na unyenyekevu."

"Ikiwa umedhulumiwa, tafuta suluhu kupitia mchakato wa mahakama. Hakuna walioshindwa katika mchakato huu, mchakato wa kidemokrasia wenye mafanikio ni ushindi wetu sote," alisema.

"Tunalenga kujenga Kenya ambayo demokrasia yake inahimiza siasa za ushindani. Wagombea ambao hawajafaulu lazima wasichukuliwe kama walioshindwa, lakini kama Wakenya ambao wamechukua nafasi yao kupanua nafasi ya kidemokrasia."

Kufuatia kura ya 2007, takriban watu 1,200 waliuawa na 600,000 wakitoroka makazi yao kufuatia madai ya kuibiwa kwa kura.

Mnamo 2017, hitilafu kubwa za vifaa zilisababisha Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo na kuamuru uchaguzi wa urais urudiwe.

Wakti huu viongozi wanakabiliwa na shinikizo la kurekebisha mambo.

Nchi mara nyingi hukabiliwa na mkwamo wakati wa uchaguzi, shughuli kote nchini zimepungua na shule zinasalia kufungwa hadi angalau Alhamisi 18 Agosti. Katikati ya jiji la Nairobi , mitaa yenye shughuli nyingi haina watu.

Madai ya wizi wa kura ni ya zamani kwani yalikuwepo hata kabla ya chaguzi za vyama vingi kuanzishwa tena katika miaka ya 1990, lakini msukumo wa uchaguzi huru na wa haki haujawahi kulegalega.

Baada ya ghasia zilizofuata uchaguzi wa 2007, vyama vya siasa na wanaharakati walibishania matumizi ya teknolojia badala ya sajili halisi, ambayo inaweza kubadilishwa kwa urahisi, ili kuhakiki wapiga kura.

Uchaguzi wa mwaka huu ni wa mara ya tatu kwa teknolojia kutumika lakini ni uchaguzi ambao haujazuia kupingwa mahakamani.

Tutajua matokeo lini?

Bado haijafahamika ni lini matokeo ya mwisho yatatangazwa.

Iwapo kuna uongozi wa wazi katika kinyanganyiro hicho, sherehe zinaweza kuzuka miongoni mwa wafuasi wake - lakini IEBC pekee ndiyo inaweza kutangaza matokeo.

Ili kushinda kinyang'anyiro cha urais katika awamu ya kwanza, mgombea anahitaji:

  • zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa kote nchini
  • angalau 25% ya kura zilizopigwa katika angalau kaunti 24.
  • Vinginevyo upigaji kura unakwenda kwa duru ya pili ambayo kwa mujibu wa sheria inapaswa kufanyika ifikapo tarehe 8 Septemba.

Rais Uhuru Kenyatta anaondoka madarakani baada ya kuhudumu kwa mihula miwili. Amemuunga mkono mpinzani wake wa muda mrefu, Bw Odinga, badala ya naibu wake, Bw Ruto.