Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Waliokuwa vigogo na kutupwa nje kwa muda wachaguliwa tena
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Raia nchini Kenya wanaendelea kusubiri matokeo kujua nani atakayekuwa rais mpya baada ya shughuli ya kupiga kura kukamilika Agosti 9, 2022.
Na hadi kufikia sasa, wananchi wameanza kutambua viongozi wao katika nyadhifa tano zilizosalia yaani gavana, seneta, mbunge, mwakilishi wa kina mama na mbunge wa bunge la kaunti.
Hata hivyo miongoni mwa waliobahatika kurejea tena kwenye ulingo wa siasa baada ya kukaa nje kwa muda ni pamoja na Farah Maalim.
Farah Maalim arejea baada ya kuwa nje kwa miaka 10
Aliyekuwa naibu spika Farah Maalim amerejea kwenye ulingo wa siasa baada ya kushinda kiti cha ubunge eneo la Dadaab.
Farah Maalim anarejea kwenye siasa baada ya kuwa nje kwa miaka 10 kumi kupitia chama cha Wiper.
Maalim aliwakilisha eneo bunge kubwa la Lagdera kuanzia 2007 hadi 2013 na mwaka huo wa 2013 aliwania kiti cha Seneti lakini akashindwa na Yussuf Haji (aliyefariki).
Mnamo 2017 aligombea ubunge wa Garissa Township lakini akashindwa na Aden Duale.
Hadi wakati huo, alidai kura ziliibiwa na kwenda mahakamani lakini baadaye akafuta kesi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangazwa mshindi na kukabidhiwa cheti, Maalim aliwashukuru wapiga kura kwa kumpa nafasi ya kuhudumu kwa mara nyingine.
"Sina maneno ya kutosha kuwashukuru watu wa Dadaab kwa kunipa imani ya kuwaongoza kwa mara nyingine tena. Imekuwa safari ndefu lakini iliyoisha kwa mwisho mwema. Sasa safari ya kweli na kazi ya kubadilisha maisha ya watu wetu inaanza," alisema.
"Kama ilivyo siku zote tunataka kuweka kipaumbele katika masuala ya maji, elimu na uboreshaji wa jumla wa miundombinu. Pia nitafanya kazi kwa karibu na serikali zote mbili kwa ajili ya kuboresha watu wetu."
Samuel Gonzi Rai
Gonzi Rai ameshinda kiti cha ubunge katika eneo la Kinango nafasi aliyoshika kwa miaka 20 katika vipindi tofauti tofauti.
Bwana Gonzi Rai ambaye amesimama kupitia chama cha Pamoja Africa Alliance ameibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake wa karibu Benjamin Dalu Tayari aliyesimama kupitia chama cha UDA.
Bwana tayari ndiye aliyemnyanganya tonge mdomo katika uchaguzi wa mwaka 2017.
Bwana Gonzi Rai ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 1992 hadi 2007 wakati huo akiwa chini ya chama cha KANU, kabla ya kuondolewa na Simeon Mkalla.
Hata hivyo katika safari yake hii, Gonzi Rai amekuwa ndani ya vyama kadha wa kadha.
Katika uchaguzi wa mwaka 2002 na 2007, Gonzi Rai aliwania ubunge kupitia chama cha Ford People huku mwaka 2013 akijitoza uwanjani kupitia chama cha TNA.
Wakati wa kampeni yake, miongoni mwa masuala alioahidi kuyatafutia ufumbuzi ni pamoja na maji, kukabiliana na kutojua kusoma na kuandika na kuimarisha usalama wa chakula katika eneo bunge lake.
Danson Mungatana
Katika eneo bunge la Garsen, baada ya kujaribu mara mbili, kurejea kwenye ulingo wa siasa bila mafanikio, mbunge wa zamani Danson Mungatana hatimaye ana kila sababu ya kutabasamu.
Bw Mungatana ambaye amesimama kupitia chama cha (United Democratic Alliance) ametangazwa kuwa seneta mteule wa Tana River baada ya kuwashinda wapinzani wake.
Bwana Mungatana amekaa nje ya siasa kwa miaka 10 tangu alipopoteza kiti chake cha ubunge.
"Hii ni ndoto iliyotimia. Mwanzo wa hatma yenye matumaini kwa watu wa kaunti ya Tana River, mimi mwenyewe na familia yangu," alisema.
Mnamo 2013, Bw Mungatana ambaye pia ni wakili, alijaribu bahati yake katika kiti cha ugavana Tana River na kuibuka wa nne.
Tena mnamo 2017, alijaribu tena kwa mara ya pili, na kuibuka wa nne.
Pia naye, aliwahi kukumbana na jinamizi linaloumiza wengi mjini baada ya kupatana na matapeli wa Afrika Magharibi, na kupoteza Sh76 milioni waliokuwa wamemuahidi kuwa bilionea.
Mwaka 2019, alikamatwa na shirika la kupambana na ufisadi kwa madai ya kuhusika katika ufujaji wa Sh51 milioni katika Kaunti ya Kilifi.
Mwalimu Harrison Garama Kombe
Huko Magarini, Kilifi, Harrison Kombe wa chama cha (ODM) amepata ubunge baada ya kutokuwepo kwa miaka mitano.
Mwalimu Harrison Garama Kombe aliingia katika siasa mwaka 2002 baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge katika bungee la 9 kuwakilisha Jimbo la Magarini kwa tiketi ya Shirikisho.
Bw Kombe, ambaye alihudumu kwa mihula miwili kuanzia 2002-2007 kupitia chama cha Shirikisho na 2013-2017.
Aidha, alizua utata mwaka wa 2017 alipodai kuwa anaweza kutibu VVU kwa kutumia tiba ya reflexology.
Mnamo mwaka 2007, kiti hicho kilitangazwa wazi na mahakama kuu ikiwa kumesalia miezi tisa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu na uchaguzi mdogo ulifanyika ambapo alishindwa na Amason Kingi Jeffah.
Mnamo mwaka wa 2007 katika uchaguzi mkuu, aligombea tena lakini akashindwa tena na Amason Kingi Jeffah.
Na kuanzia 2008, alirejea kufundisha katika Shule ya Upili hadi 2013 alipowania tena kiti cha Magarini na kukinyakua kwa tikiti ya URP kupitia muungano wa Jubilee.
Pia unawezakusoma: