Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya Uchaguzi Kenya 2022: Tume ya uchaguzi Kenya imebadili mpango kazi ili kuharakisha ujumlishaji wa matokeo ya kura za urais
- Author, Idris Situma
- Nafasi, BBC Swahili, Nairobi
- Iliyochapishwa
Ikiwa ni siku ya nne sasa wakenya wakisubiri kwa hamu na ghamu kumjua rais wao mpya, Tume huru ya uchaguzi na mipaka ya Kenya IEBC imelazimika kubadili mpango wake wa kazi ilikuharakisha ujumlishaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais mbali na kuhakiki stakabadhi zinazotoka katika maeneo yote nchini.
Mwenyekiti wa IEBC bwana Wafula Chebukati amekiri mwendo wa kupokea na kuhakiki matokeo hayo ya urais umekuwa wa kasi ya chini mno huku afisa mmoja akihitaji kati ya saa tatu na nne kuhudumiwa katika kituo cha kitaifa cha uchaguzi cha ukumbi wa Bomas Nairobi.
"Tume ya IEBC imegundua kuwa tunachukua kati ya saa 3 - 4 kukamilisha mchakato wa kupokea matokeo kutoka kwa afisa aliyesimamia uchaguzi katika eneo bunge moja. Tuna baadhi ya maofisa ambao wamekaa kwenye viti hivi kwa siku tatu. Maafisa 265 wameripoti. Tumefaulu kuwashughulikia 141 na kusalia na 124 ambao bado wako kwenye foleni'' Alisema Chebukati.
" Tunataka kufanya marekebisho yafuatayo: Wasimamizi wa uchaguzi watakabidhi fomu zao asili 34A kwa afisa wa kitaifa wa kujumlisha mara tu baada ya tangazo hili.
Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea nchini Kenya baada ya raia wake kushiriki katika uchaguzi mkuu siku ya Jumanne.
Watatoa ripoti kwa dawati la TEHAMA, kwa uthibitisho wa matokeo yaliyotumwa dhidi ya Fomu 34A.
Baada ya hapo mawakala wa rais watapewa nakala za Fomu 34A na Fomu 34B kwa matumizi yao wenyewe. Tunageuza tu mtiririko wa mchakato. Tunaamini tutaweza kumalizana na maofisa wote ifikapo mwisho wa siku leo''.Alisema bwana Chebukati.
Wakati huo huo Tume hiyo ya IEBC imebadilisha orodha na hadhi ya watu wanaoruhusiwa kuingia kwenye kituo hicho cha kitaifa kujumlisha kura katika ukumbi wa Bomas.
Kamishna Prof. Abdi Yakub Guliye, amesema mabadiliko haya yanalenga kuhakikisha utaratibu na usalama unalindwa baada ya kuibuka majibizano kati ya wafanyakazi wa tume na mawakala wa upande wa wagombea wa urais wanaoongoza katika uchaguzi huu William Ruto na wale wa Raila Odinga.
''Kuanzia sasa ikiwa wewe si wakala mkuu wa Rais, naibu wakala mkuu, na makarani waliothibitishwa. Hakuna mtu mwingine atakayeruhusiwa kuketi katika ukumbi huu kuanzia dakika hii na kuendelea mbele.
Tumetoa maagizo kwa polisi kuchunguza upya kiingilio ndani ya Bomas (kituo cha kitaifa cha kuhesabu kura.) Waangalizi Wanadiplomasia na waandishi wa habari walioidhinishwa wanaruhusiwa kuendelea na kazi yao.
Baadhi ya mawakala wa mgombea wa urais wa Muungano wa Azimio, Raila Odinga walionesha kutoridhishwa na kauli hiyo ya IEBC. Alisema Prof Guliye.
Haya yanajiri katika kituo cha kitamaduni kiitwacho Bomas katika mji mkuu, Nairobi, ambapo maafisa kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wanashughulika na kuthibitisha matokeo.
Wanalinganisha picha za fomu za matokeo kutoka zaidi ya vituo 46,000 vya kupigia kura nchi nzima na fomu halisi zinazoletwa na maafisa kutoka kila moja ya maeneo bunge 290. Hii ni kuhakikisha kuwa matokeo yanalingana.
Haya yanashuhudiwa na maajenti wa vyama kutoka vyama vikuu, ambao Bw Chebukati anasema wanaendelea kuchelewesha hilo kwa kuligeuza kuwa la "uchunguzi" wa matokeo.
Shughuli ya kuhesabu kura katika baadhi ya vituo pia ilicheleweshwa na kusafiri hadi Nairobi, haswa na maafisa kutoka maeneo ya mbali, kunaweza kuwa sababu zaidi ya kupunguza kasi ya mambo.
Tutakuwa tukiwapa taarifa kuhusu matokeo ya uchaguzi kadiri taarifa rasmi zitakavyokuwa zikitufikia.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma