Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Al-Aqsa: Waislamu wahofia mipango ya Waisrael juu ya eneo lao takatifu zaidi huko Jerusalem
"Ardhi yote ya Israeli iliahidiwa kwa watoto wa Mungu… na hapa ndipo tutakapojenga Hekalu jipya ili watu wote duniani waweze kuja na kusali pamoja."
Hayo yalikuwa maneno yenye uwezekano wa kuchochea hisia ya Moshe Feiglin, mwanasiasa wa mrengo wa kulia wa Israel, ambaye alizungumza na mwanahabari wa BBC anashuka kutoka katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa huko Jerusalem, ambako alikuwa ameenda kuomba na kuimba nyimbo za kidini pamoja na kundi la karibu waumini 20 Wayahudi.
Feiglin alizungumza wazi na bila kuficha kana kwamba msimamo wake haukuwa wenye utata.
Lakini alichosema na kufanya kilikiuka kabisa makubaliano nyeti yanayolenga kudumisha amani katika mojawapo ya maeneo matakatifu na nyeti zaidi duniani.
Kwa Moshe Feiglin na wengine kama yeye, suala hili ni rahisi tu. Wanataka kujenga Hekalu kubwa jipya la Kiyahudi katika eneo lilelile ambalo, kwa miaka 1,400 iliyopita, limekuwa mojawapo ya maeneo matakatifu zaidi ya Uislamu: Al-Aqsa.
Eneo hilo—lijulikanalo kwa Waislamu kama al-Haram al-Sharif (Patakatifu pa Tukufu) na kwa Wayahudi kama Temple Mount—ni mojawapo ya maeneo yanayotambulika zaidi navile vile ni kivutio Mashariki ya Kati.
Msikiti wenye kuba la dhahabu wa 'Dome of the Rock' unatawala eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 35, na unaweza kuonekana kwa umbali wa maili kadhaa.
Al-Aqsa umetajwa katika Qur'an, na Waislamu wanaamini kuwa Mtume Muhammad (SAW) alipaa kwenda mbinguni kutoka hapo. Pia ni eneo lililotengwa kwa ibada ya Waislamu pekee… lakini je, hili inakaribia kubadilika?
Eneo hilo pia ni mahali muhimu zaidi katika Uyahudi. Chini yake karibu na Ukuta wa Magharibi, Wayahudi husali na kuomboleza uharibifu uliosababishwa na Warumi miaka 2,000 iliyopita wa Hekalu la Kiyahudi lililokuwa juu ya eneo hilo.
Kulingana na kile kinachojulikana kama "Status Quo", makubaliano ambayo yamedumu kwa miongo kadhaa, uangalizi wa eneo la Al-Aqsa uko chini ya taasisi ya Kiislamu inayoendeshwa na Jordan: Waqf.
Wasio Waislamu wanaweza kutembelea Al-Aqsa, lakini hawaruhusiwi kusali au kufanya ibada za kidini hapo. Baraza Kuu la Marabi la Israel na marabi wengi wa Kiyahudi wa mrengo wa Haredi pia hupiga marufuku sala ya Wayahudi katika eneo hilo kwa sababu za halakhah (zinazohusiana na sheria za Kiyahudi).
Hizo ndizo sheria na makubaliano ambayo Feiglin na wengine sasa wanayapuuza waziwazi.
"Kituo cha dini nyingi"
Ripoti za hivi karibuni na madai kwamba maafisa wa Israel na Marekani wanashirikiana kuachana na kile kinachojulikana kama "status quo" zimezua wasiwasi mkubwa.
Chombo cha habari cha Middle East Eye kiliripoti, kikinukuu vyanzo mbalimbali, kwamba chombo kipya kilichoundwa na serikali ya Israel kitatangaza eneo la Al-Aqsa kuwa "kituo cha dini nyingi".
Alipoulizwa kuhusu ripoti hizo hivi karibuni katika kikao cha bunge, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema kwamba "hakuwa na taarifa hizo," ingawa Balozi wa Marekani nchini Israeli Mike Huckabee, mshirika wa karibu wa Rais Donald Trump, mara kwa mara amekuwa akizungumzia uhusiano wa Kiyahudi na maeneo matakatifu ya Jerusalem na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Ripoti nyingine zinaashiria kwamba sala za Kiyahudi kwa kiwango kikubwa zinaweza kuruhusiwa katika eneo hilo, huku Israel ikichukua hatua taratibu za usimamizi kamili wa maeneo yote ya Al-Aqsa.
Ripoti nyingine zinaashiria kwamba sala za Wayahudi kwa kiwango kikubwa zinaweza kuruhusiwa katika eneo hilo, huku Israel ikichukua hatua kwa hatua majukumu yote ya usimamizi wake.
Israeli ilitwaa Jerusalem Mashariki, ikiwemo Mji Mkongwe na maeneo yake matakatifu, pamoja na sehemu nyingine za Ukingo wa Magharibi, kutoka Jordan katika Vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967, na baadaye ikaunganisha eneo hilo chini ya utawala wake katika hatua ambayo nchi nyingi hazitambui hilo.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba hakuna mabadiliko ya "status quo" inayodumishwa kwa sasa.
"Haitatokea," anaonya Dkt. Mustafa Abu Sway, naibu mkurugenzi wa Baraza la Waqf.
Kutoka sehemu ya juu yenye mwonekano mzuri katika Mji Mkongwe, anakiri kwamba udhibiti wa Al-Aqsa ni suala nyeti ambalo sasa linaonekana kuwapa ujasiri baadhi ya wahusika wa Israeli.
Pia ana wasiwasi kwamba mabadiliko yoyote rasmi ya "status quo" yanaweza kwa urahisi kusababisha kuibuka kwa mivutano upya kati ya Wayahudi na Waislamu.
"Kutoacha suala la Msikiti wa Al-Aqsa ni kama kuanzisha matatizo mengine.
Kunahatarisha amani katika eneo hili na kuwagombanisha watu wote dhidi ya kila mmoja," anasema Abu Sway, mtaalamu anayeheshimika wa Kipalestina katika masomo ya Kiislamu na historia ya eneo hilo.
Wasiwasi kimataifa
Jordan, nchi za Ghuba, na Misri zimeonyesha wasiwasi na hofu kuhusu kile wanachokiona kama kudhoofika kwa mamlaka ya Kiislamu katika msikiti wa Al-Aqsa.
Serikali ya Uingereza pia imesema kwamba "makubaliano ya kihistoria ya 'status quo' katika maeneo matakatifu ya Jerusalem lazima yaheshimiwe."
Lakini baadhi ya raia wa Israel ambao hawajifichi tena wanaamini kwamba sasa ni wakati wao.
"Hekalu hili ni letu! Liko mikononi mwetu!" alishangilia Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa mrengo wa kulia mwenye msimamo mkali wa Israeli, Itamar Ben-Gvir, katika video iliyosambaa sana ya maandamano ya Siku ya Jerusalem mwezi uliopita.
Ben-Gvir aliongoza maandamano ya raia wa Israel waliokuwa wakipeperusha bendera kupitia Jerusalem Mashariki, ikiwemo eneo la Waislamu ya Mji Mkongwe, hadi kufika Al-Aqsa.
Mjumbe huyo mwenye utata wa serikali ya muungano ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ni mgeni wa mara kwa mara katika eneo la Al-Aqsa.
Katika video hiyo, anaonekana akiimba nyimbo na kuonyesha bendera ya Israel akipinga waziwazi makubaliano ya "status quo".
Lakini kwa Ben-Gvir, ambaye tayari ametumia nafasi yake ya uwaziri kuruhusu sala na kuimba kwa Wayahudi katika baadhi ya maeneo ya eneo hilo, hii ni mwanzo tu wa ongezeko la udhibiti mkubwa zaidi wa Kiyahudi na wa Israel katika eneo hilo.
Zaidi ya miaka 25 iliyopita, mnamo mwezi Septemba mwaka 2000, mwanasiasa wa mrengo wa kulia wa Israel Ariel Sharon alifanya jambo ambalo wakati huo lilionekana kuwa lisilowezekana. Akiandamana na mamia ya maafisa wa polisi wa Israel wenye silaha, kiongozi wa upinzani wa chama cha Likud alitembelea Mji Mkongwe na kupanda hadi katika eneo la Al-Aqsa.
Wengi walichukulia kitendo hicho kama cha makusudi cha uchochezi na kinachoweza kuzidisha mivutano, na kuwa moja ya vichocheo vilivyoanzisha maandamano makubwa ya muda mrefu ya Wapalestina maarufu kama the Al-Aqsa Intifada.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyofuata, zaidi ya watu 4,000 walipoteza maisha katika matukio ya vurugu ndani ya Israeli na maeneo yanayokaliwa ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.
Al-Aqsa ni mojawapo ya maeneo nyeti zaidi katika siasa za duniani, na matukio ya zamani pamoja na mivutano ya sasa yanaongeza hofu ya matokeo mabaya kama hayo kutokea tena.