Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022:Fahamu hatua kuanzia upigaji kura hadi kutangazwa kwa matokeo na tume ya IEBC

Baada ya mchakato mzima wa upigaji kura ambao ulianza rasmi saa kumi mbili alfajiri siku tarehe 9 Jumanne ,vituo vilifungwa mwendo wa saa kumi na moja jioni na zoezi la kuhesabu kura likaanza katika vituo hivyo.
Kinachofuata ni matokeo hayo kuwekwa katika fomu zifaazo za 34A na 34B na kisha matokeo ya urais kuwasilishwa na msimamizi wa kituo hadi katika kituo cha kujumlisha kura cha eneo bunge .
Katika kituo hicho, hesabu na matangazo ya matokeo ya viti vya wawakilishi wa wadi na mbunge hufanywa kisha matokeo ya kura za urais,ugavana,useneta na mbunge wa wanawake hujumlishwa .
Baada ya hapo,afisa msimazi wa uchaguzi katika kituo cha kujumlisha kura huwasilisha kura za urais kwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ili kuthibitishwa ,kuhakikiwa na matokeo ya mwisho kutangazwa. Jumla ya hesabu za kura za ugavana,useneta na mwakilishi wa akina mama huwasilishwa katika kituo cha kaunti cha kujumlisha kura ili matokeo kuhakikiwa ,kuthibitishwa na kutangazwa.
Mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka Wafula Chebukati ana muda wa kipindi cha siku saba kutangaza matokeo ya urais .Hata hivyo anaweza kuyatangza mapema kabla ya kukamilika kwa muda huo .Mshindi wa kura ya urais atatambuika endapo-
- Atapata asilimia 50+1 ya kura zote zilizopigwa
- Atapa asilimia 25 ya kura katika Zaidi ya nusu ya kaunti zote 47 nchini.
Endapo hakuna atakayeshinda kura kuafikiwa vigezo hivyo,basi italazimu Tume ya uchaguzi kuandaa duru ya pili ya kura katika kipindi cha siku 30 kutokea siku ya matokeo hayokutangazwa .
Iwapo kuna mgombeaji wa urais ambaye hataridhishwa na matokeo hayo atakuwa na siku saba kuwasilisha rufaa kwa mahakama ya juu zaidi ambayo nayo itakuwa na siku14 kutoa uamuzi kuhusu ombi lake .

Pia unaweza pia kusoma
UNAYOFAA KUJUA:Uchaguzi Kenya 2022: Je Naibu wa rais wa Kenya William Ruto anakabiliwa na changamoto gani katika kumteua naibu wake wa rais?














