Uchaguzi wa kenya 2022: Picha za watu na matukio muhimu siku nzima ya upigaji kura Kenya

Iliyochapishwa

Raia wa Kenya leo Jumanne wamejitokeza katika vituo vya kupigia kura nchini humo wakiwa na shauku ya kuchagua rais atakayeiongoza nchi hiyo kwa miaka mitano ijayo pamoja na viongozi wengine wakiwemo Maseneta, gavana, wabunge na madiwani.

Kura hiyo inafuatia kampeni kali iliyotawaliwa na mijadala kuhusu gharama za maisha, ukosefu wa ajira na ufisadi.Wanaogombea urais ni aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, George Wajackoyah, David Mwaure na Naibu Rais wa sasa William Ruto.

Dosari chache zimejitokeza ikiwemo ucheleweshaji vifaa katika baadhi ya maeneo pamoja na vifaa vya kielektroniki vinavyokagua alama za vidole (vinavyojulikana kama vifaa vya Kiems) kuripotiwa kutofanya kazi vizuri katika maeneo tofauti.

Lakini kwa ujumla mchakato unaonekana kwenda vizuri mpaka sasa. Hizi ni picha za matukio mbalimbali yaliyojiri katika siku hii ya uchaguzi wa Kenya

Watu walidamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kuwahi foleni katika vituo vya kupigia kura

Wengine walithubutu hata kulala vituoni ili kuwahi nafasi asubuhi

Changamoto chache zilijitokeza kama hii ya Rahab Nduta ambaye yeye hakukuta jina lake katika kituo chake cha kupigia kura na kuambiwa kuwa jina lake lipo kituo kingine

Wazee, wenye ulemavu na hata wajawazito hawakubaki nyuma na walipata ushirikiano mzuri.