Eid al-Fitr: Waislamu duniani wanaweza kupata fursa ya kusheherekea Eid al-fitr siku moja?

Chanzo cha picha, Getty Images
Sherehe za Eid (Eid al-Fitr) zimeanza leo katika maeneo na nchi mbalimbali duniani. Nchi nyingi za kiislam ikiwemo Saud Arabia zimeanza sherehe za Eid leo. Nchini Afghanistan, Eid imeadhimishwa Jumapili. Kenya, Uganda wao leo Jumatatu wanasheherekea kitaifa sikukuu hii ya Eid. Tanzania kitaifa Eid itakuwa Jumanne, kama ilivyo nchi nyingine nyingi duniani kama India.
Lakini swali kubwa, kwa nini Waislamu wote wa ulimwengu hawasherehekei Eid siku moja.
Mwandishi wa BBC Bangla Rakib Hasnat anaelezea kwa kina katika makala hii.
Ikiwa mwezi utaonekana mahali popote nchini siku ya 29 ya Ramadhani, basi taasisi za kitaifa katika nchi husika zitatangaza Eid siku inayofuata na ikiwa haitatokea basi Eid inasherehekewa baada ya kukamilika kwa siku thelathini za Ramadhani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa kawaida Eid husherehekewa nchini Bangladesh siku moja baada ya Eid nchini Saudi Arabia. Katika baadhi ya maeneo, Eid husherehekewa pamoja na Saudi Arabia na kila mwaka kunakuwa na mjadala kuhusu muandamo wa mwezi. Hilo linatokea katika mataifa yote ya Afrika, ikiwemo ya Afrika Mashariki. Kutofautiana kwenye siku ya kuadhimisha Sikukuu ya Eid.
Dakta Shamser Ali, mwanafizikia mashuhuri wa Bangladesh na pia mwandishi wa Uislamu na Sayansi (Islam and Science), anasema kuwa ulimwengu wa Kiislamu unaweza kusherehekea sikukuu ya Iddi siku hiyo hiyo kwa kufuata kanuni za Uislamu.
Kulingana na Shamser, hakuna kulazimishwa kuona mwezi katika nchi ya mtu husika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Anasema, "Sio kwamba mwezi uonekane katika nchi yenu. Imam Abu Hanifa na Mtume wamesema saumu ifungwe siku mwezi unapoandamana. "
Shamsher Ali anasema kwamba Mecca ni mahali patakatifu kwa Waislamu. Ikiwa mwezi utaonekana hapo, basi Eid inapaswa kusherehekewa katika nchi za Kiislamu kwa msingi huo. Tofauti ya muda kati ya nchi mbili sio shida kubwa katika hili.
Kwa hili, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imependekeza kumaliza kufunga na siku inayofuata iwe siku ya Eid.
Pamoja na hayo, Eid inasherehekewa nchini Bangladesh siku moja baada ya Saudi Arabia, huku Kamati ya Kitaifa ya Muandamo wa Mwezi ikisema kuwa Mtume anasema kuwa funga ianze na kuisha baada ya kuuona mwezi.

Chanzo cha picha, ANI
Je, ni hoja gani tofauti?
Kutokana na sababu za kijiografia, mwezi unaonekana nchini Bangladesh siku moja baada ya nchi za Kiarabu. Katika nchi za Kiarabu, mwezi unaonekana kabla ya Bangladesh.
Hata hivyo, Malaysia na Indonesia, ambao wapo mbele ya wakati kwa Bangladesh, wanasherehekea Eid sawa na ulimwengu wa Kiarabu. Baadhi ya nchi za Kiislamu za Afrika pia hufanya hivyo.
Zubair Muhammad Ahsanul Haque, Profesa wa Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Dhaka, anasema kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, ikiwa mwezi utaonekana katika nchi yoyote ya Kiislamu, basi itawahusu Waislamu wote.
Kila mtu anakubali kwamba mwandamo wa mwezi kwa mwaka wa Hijri huanza mara tu mwezi unapoonekana kwa macho. Hii ndiyo sheria ya Uislamu.
Kwa sababu hiyo, viongozi wengi wa dini ya Kiislamu bado wanasisitiza kuuona mwezi kwa macho katika nchi zao.
AFM Akbar Hussain, Profesa wa Idara ya Al-Quran na Mafunzo ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Kushtia, anasema anadhani endapo Eid itawekwa kwenye pendekezo la Bodi ya Sharia, kutakuwa na mkanganyiko wowote katika hili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Nini kinaamuliwa kimataifa?
Mnamo Mei 2016, mkutano wa kimataifa ulifanyika Istanbul. Wasomi wa Kiislamu kutoka nchi 50 zikiwemo Uturuki, Qatar, Jordan, Saudi Arabia, Malaysia, UAE, Morocco walikusanyika.
Mkutano huu unajulikana kama Kongamano la Muungano wa Kalenda ya Kimataifa ya Hijri. Katika mkutano huu, uamuzi ulichukuliwa kuhusiana na tofauti baina ya Waislamu mbalimbali duniani kuhusu kalenda ya Hijri.
Watu wengi walisema kuwa Waislamu wote duniani wajumuishwe katika kalenda moja na ikitokea hivyo basi Eid na mfungo unaweza kuanza siku hiyo hiyo katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Inasubiriwa kuona kama mpango huo utawezekana.












