Mzozo Ukraine: Siwezi kurudi nyumbani kwa sasa

Iliyochapishwa

Wakati vita vya Urusi na Ukraine vinaingia siku ya 20 watu wanazidi kuihama Ukraine na hata Urusi kwenda nchi na maeneo salama.

Lakini kuna baadhi ya wanafunzi wa mataifa ya Afrika Mashariki walioko Urusi na Ukraine ambao wamekataa kurudi nyumbani .

Talo Harison mwanafunzi kutoka Kenya anasema ingawa maisha ni magumu lakini hataki kurudi.

Mwanahabari wetu Scolar Kisanga amezungumza naye na hizi ndizo sababu zake za kukataa kurudi nyumbani.

Talo Harison anasema yeye ni rais wa wanafunzi mjini Moscow hivyo jukumu lake kubwa ni kuwasimamia wanafunzi wa Afrika.

Anasema kwa sasa hivi, hofu ndio iliyopo mjini Moscow kwa kuwa hawajui ni nini kitafanyika kesho, kwa sasa kuna ugumu wa kupata pesa za matumizi au chakula kwa mfano kutumiwa pesa kutoka kwa wazazi imekuwa si jambo rahisi na hata wale waliokuwa wanafanya kazi, kampuni nyingi za kigeni zimefungwa.

Hivyo hofu kubwa ni pesa zikiisha, ni nini kitatokea baada ya hapo, ndio maana wengi wanaishi nayo.

Yeye mwenyewe binafsi anasema ana hofu lakini hataki kurudi nyumbani kwa kuwa masomo yanaendelea Urusi kama kawaida.

"Mimi nina hofu ila nimebakisha miezi minne nimalize masomo yangu, kilichonileta huku ni masomo hivyo staki kwenda na kurudi, nikirudi nyumbani ina maana nitarudia mwaka mzima," Talo anaeleza.

Talo amesisitiza kuwa masomo yanaendelea kama kawaida licha ya hofu iliyopo, mtu kama amesoma udaktari miaka mitano na akindoka sasa atakuwa amepoteza maana hawajui nini kitafanyika kesho.

Aidha Talo amesema, wametoka katika janga la corona ambalo liliwaathiri sana na kama uko mbali na wazazi iliathiri sana na sasa vita imekuja na inawaathiri ila wanaomba kila kitu kiwe sawa mpaka watakaporudi nyumbani.

Talo anaelewa kuwa Urusi iko hatarini zaidi kupata athari za vita licha ya kwamba dunia nzima inaweza kuathirika kutokana na vita hii lakini bado ni muhimu kwa yeye kumaliza masomo yake na hali ikiwa mbaya zaidi atarudi nyumbani.

Wanafunzi wengi wanaona bora kuvumilia ili wamalize masomo yao

Simulizi za waafrika wengine Ukraine na Urusi