Mzozo wa Ukarine: 'Hakuna Mtanzania atakayekuja kusahau kilichotutokea Ukraine' - Dokta Larsen

Iliyochapishwa

Wiki ya pili sasa, mapigano yanaendelea nchini Ukraine, Urusi ikitaka kudhibiti miji mikubwa ya nchi hiyo.

Kumekuwa na jitihada kubwa kutoka mataifa mbalimbali kuondosha raia wake, ambapo kwa mujibu wa taarifa rasmi, zaidi ya raia wa kigeni 7,000 wameondolewa Ukraine kwa siku mbili za Jumanne na Jumatano.

Mashariki mwa Ukraine, katika mji wa Sumy, ulio mpakani mwa Urusi, kuna idadi kubwa ya raia wa Afrika ambao wengi wao wako huko kama wanafunzi katika vyuo mbalimbali.

Urusi kwa mara nyingine imekubali kusitisha mapigano kwa masaa mengine 12 kuruhusu raia katika maeneo 6 yaliyoathirika zaidi nchini Ukraine, kwa mujibu wa naibu waziri mkuu, Iryna Vereshchuk.

Jana na leo raia zaidi ya raia 7,000 hasa kaskazini mashariki mwa mji wa Sumy wamefanikiwa kuondolewa, akiwemo Dokta Larsen Mohamed, mmoja wa wanafunzi wanaosomea udaktari nchini humo.

" Tulitolewa kwa ulinzi mkubwa sana, kulikuwa na mabasi mengi, ni siku ambayo walitaka kututoa wanafunzi wakigeni wote, kwa hiyo tuliondoka wengi kwa msaada wa red Cross (Shirika la Msalaba Mwekundu) na jeshi kwa ujumla', Larsen aliaambia BBC kwa njia ya simu akiwa kwenye treni kuelekea mpaka wa Urusi.

Dr. Larsen ambaye anaongoza msafara wa Watanzania kuvuka mpaka wa Urusi anasema kumekuwa na mawasiliano mazuri katika siku za hivi karibuni na serikali ya Tanzania juu ya namna ya raia wa Watanzania kuondoka Ukraine.

"Nashukuru mpaka sasa hivi, balozi zimeshatuma watu mpakani wanatusubiri, wako wengine Watanzania wameshafika mpakani, tunashukuru kwa kweli serikali ya Tanzania imejitahidi sana', alisema.

Kwa mujibu wa Dr. Larsen ni kwamba wao ni kundi la mwisho la wanafunzi wa Kitanzania waliokuwa nchini Ukraine kutoka, hasa eneo la Sumy ambalo limekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wa kigeni.

Kwa mujibu wa Serikali ya Tanzania kupitia waziri wake wa masuala ya kigeni, Liberata Mulamula, Tanzania ilikuwa na wanafunzi zaidi ya 300 waliokuwa wanasoma katika vyuo mbalimbali nchini Ukraine.

Nini hawatasahau wanafunzi wa Kitanzania nchini Ukraine?

Pengine wiki mbili zilizopita zitakaa kichwani kwa wanafunzi wengi wa Kitanzania waliokuwa Ukraine wakiendelea na masomo yao. Wameshuhudia na kupata uzoefu wa mambo ambayo pengine wamekuwa wakiyasoma na kuyasikia mahali pengine. Ni uzoefu mpya wa kihistoria.

"Kusema ukweli ni mambo mengi na historia kubwa sana', anasema Dr Larsen baada a BBC kumuuliza hatasahu nini katika siku hizi za vita Ukraine.

"Kuona ndege na mavifaru kabisa, kusema ukweli ni kitu ambacho hatutakisahu, sidhani kama kuna Mtanzania yoyote alikuwa huku mwanafunzi atakuja kusahau na ile hali tuliyokuwa tunaishi kwa unyonge na ni watu ambao tulikuwa tumekata tamaa kabisa', anasema Dr. Larsen

Silaha za aina mbali mbali zimekuwa zikitumika katika vita hiyo ya Ukraine, ikiwemo vifaru na ndege za kivita anazozizungumza Larsen na kusababisha madhara makubwa.

Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi

Mkuu wa Idara ya ujasusi ya Marekani ameliambia bunge la nchi hiyo kwamba tangu kuanza kwa vita vya Ukraine wiki mbili zilizopita wanajeshi wa Urusi kati ya 2,000 na 4,000 wameuawa.

"Walikuwa na mpango mbaya," Scott Berrier alisema, wakati akikadiria, kwa ujasiri mdogo, vifo kulingana na taarifa za usalama na vyanzo vingine.

Emanuel Kaisi (sio jina lake halisi) Mtanzania aliyezungumza na BBC kwa njia ya simu naye alieleze madhila ambayo hawezi kuyasahau.

'Umeme tulikatiwa (mabomu yalikata umeme), chakula kipo ila foleni mpaka upate ni ngumu, ATM nazo watu wamejaa, hela zinaisha kwenye ATM unashindwa kupata pesa za kwenda kununua chakula, kwa hiyo tunapata shida kwakweli, watu tuna siku 3 hatujaoga ndani', alisema Kaisi muda mfupi kabla ya kuondoka Ukraine mapema wiki hii.

Licha ya mara kadhaa kukubaliana kusitisha mapigano na kufungua njia salama ili kuruhusu raia wa Ukraine na mataifa mengine kuvuka mipaka kwa usalama, kuna wakati kumekuwa na upuuzwaji wa makubaliano hayo, na kusababisha zoezi la kuwaondoa raia kuwa gumu.

Mpaka sasa zaidi ya watu milioni 2, wameikimbia Ukraine kwenda mataifa jirani kuhofia usalama wao.

Simulizi za waafrika wengine Ukraine na Urusi