Mzozo wa Ukraine: ‘Tulikuwa tumezungukwa na jeshi la Urusi’-Mwanafunzi Mtanzania

Iliyochapishwa

Ni Siku ya 19 leo tangu uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na wanafunzi wengi wa kiafrika waliolazimika kutoroka mapigano nchini Ukraine wanasimulia masaibu yao na jinsi walivyoweza kukimbilia mataifa salama .

Mmoja wa wanafunzi hao ambaye amezungumza na BBC ni Majaliwa Mheta,Mtanzania aliyekuwa masomoni nchini Ukraine na kukimbilia Hungary. Yeye pamoja na wenzake wengi walikuwa katika mji wa Sumy walikokuwa wakisomea wakati mashambulizi makali yalipoanza .

Safari ya kwenda taifa la Hungary ilikuwa hatari sana na kuna wakati anasema walikuwa wamezingirwa na wanajeshi wa Urusi

Mheta anasema alikuwa na fursa ya kutoroka mapema kutoka Ukraine lakini hangeweza kufanya hivyo kwa sababu kuna wenzake wanne ambao wazazi wao walikuwa wamemtaka ahakikishe nao wapo salama .

Akalazimika kusalia huko hadi alipopata fursa ya kutoroka akiwa na watatu kati yao walipoabiri teksi wakiwa watu wanne hadi katika mji wa Budapest nchini Hungary .

Mheta anasimulia hofu waliokuwa nayo wakati mabomu yalipokuwa yakirushwa kila upande lakini muda huo wote anashukuru kwamba walikuwa wakiwasiliana na Ubalozi wa Tanzania.

Hatimaye alifaulu kufika Budapest wiki mbili zilizopita ambapo kuna wanafunzi wengine wa kiafrika takriban 80 ambao anawafahamu na kunao ambao wameanza kuhamia nchi nyingine za bara ulaya kuendelea na masomo yao baada ya kupatiwa fursa hizo na mataifa mbali mbali.

Simulizi za waafrika wengine Ukraine na Urusi