Mzozo Ukraine: 'Tulitembea zaidi ya kilomita 50'-Mwanafunzi kutoka Tanzania

Iliyochapishwa

Ni Siku ya 21 leo tangu uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na wanafunzi wengi wa kiafrika walilazimika kutoroka mapigano nchini Ukraine kwenda mataifa salama.

Mashariki mwa Ukraine, katika mji wa Sumy, ulio mpakani mwa Urusi, kuna idadi kubwa ya raia wa Afrika ambao wengi wao wako huko kama wanafunzi katika vyuo mbalimbali.

Rebecca Baare ni miongoni mwa wanafunzi wa Tanzania ambao walikuwa wanasoma Ukraine, anatusimulia jinsi alivyopata moyo wa kutembea kilomita 50 baada ya kupata barua kutoka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi.

Rebecca anasema, kilichowafanya watembee umbali mrefu sana ni ugumu wa kupata usafiri, madereva wa magari ya kukodi walikuwa hawakubali kupeleka watu maeneo hayo.

Lakini waliamua kuanza safari baada ya kupokea barua ya serikali kutoka Urusi kuwa ni sehemu salama.

"Tulitembea kama kilomita 56, ila changamoto kubwa ilikuwa ni baridi ingawa hakukuwa na barafu inayoanguka na wanajeshi walipotambua kuwa sisi ni wanafunzi walikuwa wanatupa lifti katika sehemu fupifupi."

Magari mengi yalikuwa yanaogopa kwenda upande huo kwa kuwa ni sehemu ya adui.

"Tulikuwa tuna hofu lakini matumaini yalikuepo maana watu wa serikalini kwetu walikuwa wakiongea nasi kila mara."

Ameongeza kusema kuwa "Kurejea kwake nyumbani kumempa furaha sana ingawa hajui hatima yake ya kurudi Ukraine, inabidi watafute tena vyuo huku maana hatujui kama vita haitalipua chuo nilichokuwa nasoma."anasema Rebecca.

Simulizi za waafrika wengine Ukraine na Urusi