Esnath Gedion na ndoto ya kuwa mwanasheria, akiwa na mtoto wake darasani

- Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC Africa, Tanzania
- Iliyochapishwa
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, maelfu ya wanafunzi wa kike ambao awali walikatisha masomo yao baada ya kupata ujauzito wameanza kurudi mashuleni.
Hatua hii inakuja mwezi mmoa tu baada ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuondoa marufuku iliyokuwa imewekwa awali na mtangulizi wake John Pombe Magufuli ambae alipiga marufuku wanafunzi waliopata mimba kuendelea na mfumo rasmi wa masomo kwa madai kwamba, wanafunzi waliopata ujauzito watakuwa na ushawishi mbaya wakirudi darasani.
Maisha yamebadilika
Lakini katika idadi ya waliorudi shuleni, baadhi wamekuta maisha yamebadilika tofauti na walivyokuwa awali.
Hapa naingia katika moja wapo ya darasa lililosheheni wanafunzi wa kike, umri wao unaanzia miaka 13 had 21. Wote ni wahanga wa mimba za utotoni.
Macho yangu, ghafla yanavutiwa na Esnath Gedion, wenye umri wa miaka 19. Tofauti na wenzake, Esnath yuko darasani huku akiwa amempakata mtoto wake mwenye umri wa miezi minne.
"Sina mtu wa kumwachia mtoto nyumbani, na uwezo wa kumlipa mtu sina, ila nashukuru nilivyokuja shule, waliniruhusu kuingia na mtoto darasani," anasema Esnath.
'Nilijisikia Vibaya'

Esnath alipewa ujauzito na kijana aliyekutana nae siku moja wakiwa safarini bila kumfahamu kwa kina. Ilikwua ni mwaka jana akiwa kidato cha nne. Miezi mitano baada ya kugundulika shuleni alilazimishwa kukatisha masomo yake. Huu ulikuwa ni ukurasa mpya katika maisha yake.
"Nilijisikia vibaya sana nilipogundua nina ujauzito. Sikuona mbele wala nyumba. Niliona giza tu mbele yangu. Nilipoteza mwelekeo kabisa. Ndoto zangu zote zilikufa. Sikufikiria kama kuna siku nitarudi tena shuleni," anasema Esnath.
Hata hivyo, hali hii haikuishia kwa Esnath pekee, bali familia yake yote ilijawa na simanzi baada ya kuona binti yao amekatisha masomo.
"Bibi yangu ambaye ndie aliyenilea alihuzunika sana. Akaniambia umekatiza masomo ukiwa kidato cha nne? Akaniuliza nitamlisha nini mtoto?" anaeleza Esnath.
Nae bibi yake, ambae pia anaitwa Esnath, ambae mara nyingi anafanya biashara ya kuuza sambusa na kulimalima katika boma lake, anasema alihuzunika mno kuona mjukuu wake amepata ujauzito.
Unaweza pia kutazama:
"Nilihuzunika sana. Nilitamani hata kumpiga lakini sikuweza kwa sababu nilikuwa namuuguza mume wangu. Lakini sasa hivi nashukuru kuona amerudi shule," anasema.
Kukosa mtu wa kukaa na mtoto
Tangu kuondolewa kwa marufuku hiyo mwishoni mwa mwaka jana, ingawa ameruhusiwa kuingia darasani na kuendelea na masomo, lakini changamoto yake kubwa ni kukosa mtu wa kumwachia mtoto nyumbani.
"Umakinifu lazima upungue ninapokuwa darasani na mtoto, sio msumbufu akiwa darasani, lakini mara amegeuka huku, mara kule. Lakini changamoto yangu kubwa ni pale mtoto anapojisaidia, siwezi kumbadilisha akiwa darasani, na hakuna sehemu maalumu ya kumbadilisha," anasema Esnath.
Esnath, bado anaendelea kuishi na bibi yake ambae anafanya biashara ya kuuza sambusa, huku msaada mkubwa wakiutegemea kutoka kwa mamake aishie Dar es Salaam.
"Mara ndio anatutumie anachokipata. Mara nyengine anatuma elfu situ ambazo zinanisaidia nauli ya Kwenda shule," anasema Esnath, ambae kwa siku anaweza kutumia takriban kiasi cha shilingi elfu moja kupanda bajaji.
Zaidi ya wasichana 1500 walifukuzwa shuleni katika mkoa anaoishi Esnath wakati wa marufuku hiyo.

Lakini hii leo, ni miongoni mwa wasichana wapatao 240 ambao wamerudi shuleni mkoani humo mwaka huu.
Mfumo wezeshi
Thomas Amos Mbuba ambae ni mratibu wa mradi wa Alternative Education Pathway mkoani Mbeya anasema wana matumaini ya kuwarudishwa wasichana wengi zaidi baada ya kuja na mfumo wezeshi.
"Wanafunzi hawa tunawarudisha, tunatambua wamekaa muda mrefu, lakini tumekuja na mfumo ambao ni wezeshi, kwa maana watoto wa kike hawa wengine tunajua wana umri mkubwa, lakini watasoma kwa muda mfupi kadri inavyowezekana," anafafanua Thomas Amos Mbuba.
Esnath anasema hivi sasa anasoma ili awe mwanasheria, uamuzi wa kuondoa marufuku iliyowekwa awali, umewapa matumain malefu ya wasichana waliorudi shule nchi nzima. Ingawa kwa wengine, uamuzi huu unaonekana umekuja kuchelewa.














