Tiba ya HIV iko tayari kwa majaribio

Majaribio ya tiba ya virusi vya ukimwi (VVU) yanatarajiwa kuanza nchini Denmark kabla ya mwisho wa mwaka, kupata dawa ambayo inaweza kuthibitisha kuwa tiba iliyosubiriwa kwa muda mrefu ya virusi hivyo vya ugonjwa wa Ukimwi.

Moja kwa moja

  1. Kashfa ya kumpiga busu mchezaji yamfuta kazi kocha wa timu ya taifa ya wanawake ya Hispania

    Spain

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Jorge Vilda (kulia) anaonekana kuwa mshirika wa karibu wa Luis Rubiales (kushoto)

    Jorge Vilda, kocha mkuu wa timu ya taifa ya wanawake iliyotwaa hivi majuzi Kombe la Dunia la Wanawake, amefukuzwa kazi kutokana na kashfa inayoendelea ya Luis Rubiales.

    Ushindi wa Hispania ulifunikwa na kashfa ya rais wa shirikisho la soka nchini humo Rubiales kumbusu mshambuliaji Jenni Hermoso, jambo ambalo alisema lilikuwa la makubaliano.

    Wengi katika benchi la ufundi la Vilda walijiuzulu huku wachezaji 81 wakikataa kuichezea Hispania baada ya tukio hilo. Rubiales amekataa kujiuzulu lakini amesimamishwa kwa muda na Fifa, shirikisho la soka duniani.

    Katika taarifa yake, shirikisho la Hispania RFEF halijatoa sababu mahususi za kutimuliwa kwa Vilda.

    Hata hivyo, RFEF imekuwa ikichunguza kama inaweza kumtimua Vilda - anayechukuliwa kuwa mshirika wa karibu wa Rubiales - tangu wiki iliyopita.

    Alionekana akimpigia makofi Rubiales kwenye mkutano mkuu usio wa kawaida wa RFEF mapema mwezi Agosti - wakati Rubiales alipokuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa hatajiuzulu na kusema angempa Vilda mkataba mpya..

  2. Wanafunzi waliovaa abaya Ufaransa 'watimuliwa' shule

    France

    Chanzo cha picha, AFP

    Waziri wa elimu wa Ufaransa amethibitisha kuwa karibu wanafunzi 300 walifika shuleni siku ya Jumatatu wakiwa wamevalia abaya, vazi refu la Kiislamu ambalo lilipigwa marufuku shuleni kuanzia wiki iliyopita.

    Kwa mujibu wa takwimu rasmi, wasichana 298 - wenye umri wa miaka 15 au zaidi - walifika shuleni wakiwa na vazi hilo lililopigwa marufuku.

    Chini ya maagizo yaliyowekwa na wizara, katika kila kisa kulikuwa na kipindi cha mazungumzo na wafanyakazi wa shule kuhusu vazi hilo.

    Wasichana wengi waliokubali kubadili vazi hilo waliweza kuendelea na masomo. Hata hivyo, wasichana 67 walikataa kufuata sheria hiyo na wakarudishwa nyumbani.

    Kinachofuata sasa ni mazungumzo na familia zao kutafuta suluhu. Ikiwa hiyo itashindikana, watatengwa.

    Ikilinganishwa na wavulana na wasichana milioni 12 walioanza muhula mpya Jumatatu, serikali inaamini kuwa takwimu zinaonyesha kuwa marufuku yake imekubaliwa kwa mapana.

    Ufaransa imepiga marufuku vikali mavazi ama ishara zozote za kidini katika shule zzake za serikali na majengo ya serikali, ikisema kwamba zinakiuka sheria.

  3. Tiba ya HIV iko tayari kwa majaribio

    HIV

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Majaribio ya tiba ya virusi vya ukimwi (VVU) yanatarajiwa kuanza nchini Denmark kabla ya mwisho wa mwaka, kupata dawa ambayo inaweza kuthibitisha kuwa tiba iliyosubiriwa kwa muda mrefu ya virusi hivyo vya ugonjwa wa Ukimwi.

    Matokeo ya majaribio ya awali ya maabara yaliyofanywa na timu mbili za wanasayansi wa Australia kwa ushirikiano na wenzao kutoka Denmark yanatia moyo kuhusu matumaini ya kupata dawa.

    Utafiti wa Australia unaonyesha kwa hakika kwamba dawa ya Oncologic venetoclax ina uwezo wa kuchunguza "seli" katika mwili wa binadamu ambazo zinaathiriwa vibaya na virusi.

    Mwaka ujao, pamoja na Denmark, majaribio ya dawa hiyo pia yataanza huko Melbourne, Australia.

    Wakati huo huo, vidonge vyenye jina la kibiashara la VENCLEXTA vilitengenezwa awali ili kupambana na saratani ya damu.

    Ilithibitishwa nchini Marekani mnamo 2016 na tangu wakati huo, kulingana na madaktari, tayari imesaidia maelfu ya wagonjwa wa saratani.

    Kwa sasa kuna karibu watu milioni 40 wanaoishi na VVU duniani.

    Uchunguzi na hatimaye utumiaji wa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo unawezesha kuzuia kuongezeka kwa virusi vya ukimwi , hali inayozuia uharibifu wa kinga ya mwathiriwa mara moja.

    Wakati mtu anapotumia dawa mara kwa mara , mwathiriwa pia huwacha kuwa hatari kwa wapendwa wake – lakini yeye mwenye haponi kabisa.

    Unapowacha kutumia dawa kila siku makali ya ugonjwa huo hurudi.

  4. Mabilioni ya dola yazidi kuhaidiwa Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi Kenya

    kENYA

    Chanzo cha picha, AFP

    Ahadi za pesa tayari zimewawsilishwa kwa Afrika katika mkutano wa kilele wa hali ya hewa unaoendelea nchini Kenya, huku Uingereza ikiwa miongoni mwa nchi za kwanza kutoa ahadi.

    Imehaidi kutoa dola $61m katika miradi mipya ya kuwasaidia Waafrika kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa , Waziri wa Maendeleo wa Uingereza Andrew Mitchell alisema.

    "Hii ni pamoja na £34m kwa miradi mipya katika nchi 15 za Afrika kusaidia wanawake, jumuiya zilizo katika hatari, na zaidi ya wakulima 400,000 kujenga uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa," Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza ilisema.

    Falme za Kiarabu (UAE) pia imeahidi kuipatia Afrika dola $4.5bn katika uwekezaji wa nishati safi.

    Serikali ya Ujerumani ilitangaza mpango wa kusamehe madeni ya Kenya, ambapo itasamehe $65m ili taifa hilo la Afrika Mashariki liwekeze fedha hizo katika miradi ya kijani kibichi.

    Inatarajiwa kuahidi zaidi ya dola $486m nyingine kuendeleza mapambano ya Afrika dhidi ya hali ya hewa. Inatarajiwa mipango mingine na ufadhili utatangazwa katika Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika, ambao unakamilika Jumatano.

  5. Vigogo wa Jeshi DRC wakamatwa kufuatia vifo vya waandamanaji 43

    DRC

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Mamlaka ziliwakamata waandamanaji 168

    Maafisa wawili waandamizi wa jeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametiwa mbaroni baada ya kudaiwa kutoa amri ya kutumika kwa nguvu kufanya mauaji dhidi ya maandamano yaliyopigwa marufuku.

    Vikosi vya usalama viliingilia kati wakati maandamano dhidi ya walinda amani wa kimataifa yakiendelea Jumatano iliyopita na watu 43 waliuawa na wengine 56 kujeruhiwa.

    Waandamanaji hao walikuwa wa madhehebu mbalimbali ya kidini na walikuwa wakitaka vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Afrika Mashariki viondolewe katika maeneo yao.

    Maafisa waliokamatwa ni Mike Mikombe, mkuu wa walinzi huko Goma, na Donat Bawili, kiongozi wa jeshi mjini humo, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani Peter Kazadi. Haijabainika ni mashtaka gani watakabiliwa nayo.

    Waziri huyo aliahidi kuwa uchunguzi kuhusu mauaji hayo, ambayo yalizua ghadhabu ya kitaifa na kimataifa, utakuwa wa wazi.

  6. Cuba yabaini raia wake kutumika vita ya Ukraine

    Cuba

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya mambo ya nje ya Cuba imesema kuwa imebaini mtandao wa biashara haramu ya binadamu unaolenga kuwasajili raia wa Cuba kupigania Urusi katika vita vyake nchini Ukraine. Ilisema kwamba Wacuba wanaoishi Urusi na "hata wengine nchini Cuba" "wamejumuishwa katika vikosi vya kijeshi vilivyopigana katika vita vya Ukraine".

    Cuba ni mshirika wa karibu wa Urusi, lakini ilisisitiza katika taarifa yakekwamba "sio sehemu ya mzozo wa Ukraine".

    Mpaka sasa Urusi haijasema kitu kuhusu hilo.

    Wizara ya mambo ya nje ya Cuba haikubainisha ni nani aliyehusika na operesheni hiyo. Mwezi uliopita Rais Vladimir Putin aliamuru jeshi la Urusi kuongeza idadi ya wanajeshi wake baada ya vikosi vyake vya kivita kupata upinzani mkubwa nchini Ukraine.

  7. UN yaonya kuhusu idadi ya majeruhi kwenye maandamano ya Waeritrea huko Israel

    Eritrea

    Chanzo cha picha, AFP

    Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inasema "imesikitishwa" na idadi kubwa ya majeruhi wakati wa mapigano ya hivi majuzi yaliyohusisha Waeritrea nchini Israel.

    Siku ya Jumamosi takriban watu 140 walijeruhiwa mjini Tel Aviv, huku kukiwa na makabiliano makali yanayohusisha polisi wa Israel na mapigano kati ya wafuasi na wapinzani wa serikali ya Eritrea.

    Mzozo ulianza baada ya wanaharakati wa Eritrea kusema kuwa wameiomba mamlaka ya Israel kufuta tukio lililoandaliwa na ubalozi wa nchi yao.

    "Imeshtushwa na idadi kubwa ya majeruhi wakati wa maandamano yaliyohusisha wapinzani wa Eritrea, haswa Israeli," UN ilisema katika taarifa kwenye X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter. "Ni muhimu kwamba uchunguzi ufanyike, matamshi ya chuki yaepukwe - haswa na mamlaka", inasema.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema kuwa "mstari mwekundu" ulikuwa umevukwa na waasi hao na kuamuru kuondolewa kwa wahamiaji wa Kiafrika aliowataja kuwa "wameingia kinyume cha sheria"

  8. 'Wanawake wanateka watoto wao na kukimbilia Cyprus'

    UK

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kuna idadi kubwa ya wanawake wanaowateka watoto wao nyara nchini Uingereza. Wanawake wengi wanasema watoto wao walikabidhiwa kwa wenzi wao na mahakama za familia za Uingereza na Wales wamewateka nyara na kukimbilia kaskazini mwa Cyprus inayodhibitiwa na Uturuki.

    BBC ilizungumza na wanawake sita kati yao ili kuchunguza baadhi ya simulizi.

    "Nimeambiwa kuna hati ya kukamatwa kwangu. Amri za mahakama zinasema siwezi kuwasiliana na wanafamilia, mtoto wangu hawezi kuzungumza na bibi na babu yake," anasema Rose - sio jina lake halisi. "Imeharibu familia yangu."

    Amekimbilia katika nchi ya kigeni na anasema akaunti zake za benki zimezuiwa. Rose bado anaamini kuishi Kaskazini mwa Cyprus - sehemu ya kisiwa kilichogawanyika, kinachokaliwa na Uturuki lakini hakitambuliki kimataifa kama nchi - ni mahali salama kwake.

    Uingereza inasema inachukua kila kesi ya utekaji nyara wa watoto unaofanywa na wazazi kwa uzito mkubwa na sheria inaweza kutumika kuwarudisha watoto hao. Lakini Cyprus Kaskazini haijasaini mkataba wa kimataifa kuhusu utekaji nyara wa watoto na hakuna makubaliano rasmi ya kuwarejesha nyumbani.

  9. 'Tutapigana hadi mwanajeshi wa mwisho' - Kiongozi wa RSF wa Sudan

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Hapo awali Hemedti alitoa wito kufanyika kwa mazungumzo ili kupata suluhu

    Kiongozi wa Kikosi cha Sudan Rapid Support Forces (RSF) amesema wanajeshi wake "wana uwepo mkubwa katika mji mkuu" na "watapigana hadi mwanajeshi wa mwisho" huku mapambano ya kikatili ya kupigania madaraka kati ya jeshi la serikali na RSF yakikaribia kuingia mwezi wake wa tano.

    Katika ujumbe wa sauti uliotumwa kwenye mtandao wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo alirudia shutuma kwamba jeshi lilianzisha vita ili kuwawezesha washirika wa Rais aliyepinduliwa Omar al-Bashir kurejea madarakani.

    Ujumbe huo ni mabadiliko kutoka kwa kauli yake ya tarehe 27 Agosti wakati kamanda wa RSF, ambaye anajulikana zaidi kama Hemedti, alitoa wito wa suluhu la mazungumzo na kuelezea mipango ya kurejesha serikali inayoongozwa na raia.

    Hata hivyo, hatua hiyo ilikataliwa na mpinzani wake, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye amerudia kusema kwamba jeshi litaishinda RSF.

    Jenerali Burhan amejitokeza mara kadhaa hadharani, ikiwa ni pamoja na ziara mbili za kigeni nchini Sudan Kusini na Misri tangu mwishoni mwa Agosti, akipendekeza kuwa jeshi lina uwezo mkubwa.

    Serikali inayoongozwa na jeshi mara kwa mara imeitaka jumuiya ya kimataifa kutambua RSF, mshirika wake wa zamani, kama "shirika la kigaidi".

    • Wizara yake ya Mambo ya Nje ilisema mkutano wa hivi majuzi kati ya afisa wa RSF na mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki nchini Ethiopia ulikuwa "mfano mbaya".

    Soma zaidi:

    • Mzozo wa Sudan: 'Niliona miili ikitupwa kwenye kaburi la pamoja Darfur'
  10. Shirika lisilo la kiserikali kuwaachilia huru vifaru 2000 waliozuiliwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Idadi ya vifaru weupe wa Kusini imepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya uwindaji haramu

    Shirika la hifadhi ya wanyama pori African Parks limetangaza mipango ya kuwaachilia huru vifaru weupe 2,000 ambao kwa sasa wanahifadhiwa katika hifadhi ya Platinum Rhino, hifadhi kubwa zaidi duniani iliyopo Afrika Kusini.

    Shirika hilo lisilo la kiserikali limetangaza mpango huo baada ya kununua shamba la hekta 7,800 kwenye mpaka wa nchi hiyo na Botswana.

    "African Parks imenunua hifadhi kubwa zaidi duniani ya ufugaji wa faru waliofugwa katika jitihada za kuwaokoa na kuwahamishia maeneo salama, yanayosimamiwa vyema kote barani Afrika," shirika hilo lilisema katika taarifa yake Jumatatu.

    Shirika hilo limeongeza kuwa, mradi huo si tu kwamba utawakomboa kutoka kifungoni, bali pia kutahakikisha mustakabali wa wanyama hao walio hatarini kutoweka kwa kuwalinda dhidi ya uwindaji haramu.

    African Parks ilipata ufadhili wa dharura kununua shamba hilo la vifaru ambalo lilikuwa na matatizo ya kifedha baada ya mmiliki wake, John Hume, kuliuza mwezi Aprili.

    Hume amesifiwa kuwa mhifadhi lakini pia alikabiliwa na ukosoaji wa kutetea biashara ya pembe za faru, jambo ambalo alisema ni muhimu kuwakinga faru wake dhidi ya uwindaji haramu na kutafuta pesa za kuendeleza hifadhi hiyo.

    African Parks kwa sasa inafanya kazi na serikali 12 kuendesha maeneo 22 ya wanyamapori yaliyohifadhiwa kote barani Afrika.

    Inakadiriwa kuwa kuna faru weupe wa kusini wapatao 18,000 waliosalia porini.

    Pia unaweza kusoma:

    • Jinsi faru wanavyokuzwa kwenye maabara, sayansi inayoweza kuokoa viumbe vilivyo hatarini kutoweka
  11. Waziri mkuu wa Niger anatarajia kufikia makubaliano na Ecowas

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Niger baada ya mapinduzi Ali Mahamane Lamine Zeine alisema maandalizi yanafanywa iwapo wangeshambuliwa

    Wazir Mkuu mpya wa Niger amesema kuna matumaini ya kufikia makubaliano baina ya uongozi wa jeshi mjini Niamey na Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Magharib Ecowas.

    Ali Mahamane Lamine Zeine, aliyeteuliwa kwa wadhfa huo na serikali ya kijeshi, alikuwa akizungumza kwa mara ya kwanza hadharani katika mkutano na wandishi habari katika mji mkuu Niamey.

    “Hatujasitisha mazungumzo na Ecowas, bado tunaendelea kujadiliana. Tuna matumiani ya kufikia makubaliano katika siku zijazo,” aliwaambia wandishi habari.

    Jumuiya ya Ecowas imetishia kutumia nguvu kurejesha utawala wa kiraia nchini humo baada ya jeshi la kumlinda rais kufanya mapinduzi mnamo Julai 26 na kumng'oa madarakani rais Mohamed Bazoum.

    Kamanda wa mapinduzi hayo, jenerali Abdourahmane Tchiani, alijitangaza kama kiongozi mpya na kumweka kizuizini rais Bazoum na familia yake.

    Lamine amesisitiza kuwa uongozi wa kijeshi utajihamai kutokana na uvamizi wowote.

    Waziri Mkuu huyo pia aliongeza kwamba uongozi mpya bado unaendelea kufanya mazungumzo na Ufaransa ili kuondoa vikosi vya Ufaransa vilivyoko nchini humo. Ufarsana ina takriban wanajeshi 1,500 nchini Niger, baadhi yao wakiwa katika kambi moja karibu na mji mkuu.

    Ufaransa imekataa kutambua viongozi waliofanya mapinduzi na kusisitiza kwamba bado inatambua tu uongozi wa rais Bazoum kama serikali halali, hatua ambayo imezua ghadhabu miongoni mwa uongozi wa kijeshi mjini Niamey.

    Serikali hiyo imejibu kwa kutangaza kumfukuza balozi wa Ufaransa nchini humo huku mamia ya raia wanaounga mkono mapinduzi wakiandamana kutaka balozi huyo aondoke nchi hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

    • Mapinduzi Niger: Historia ya mapinduzi manne Niger tangu uhuru
  12. New Zealand: Mwanamke aachwa na kifaa cha upasuaji cha ukubwa wa sahani kwenye tumbo lake kwa miezi 18

    .

    Chanzo cha picha, APPLIED MEDICAL

    Kifaa "cha ukubwa wa sahani ya chakula cha jioni" kiliachwa kwenye tumbo la mwanamke huko New Zealand baada ya kujifungua kwa upasuaji katika hospitali ya Auckland.

    Kifaa hicho kilichotumika kushikilia sehemu iliyofanyiwa upasuaji –kilitolewa miezi 18 baada ya mwanamke huyo kujifungua.

    Wakati huo wote, mwanamke huyo alivumilia maumivu makali, akitembelea madaktari kadhaa hadi kifaa hicho kilipopatikana kupitia uchunguzi wa CT scan.

    Wadhibiti wa afya walisema mfumo wa hospitali za umma hautoi huduma nzuri kwa wagonjwa.

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    • Awali, bodi ya afya ya wilaya ya Auckland Te Whatu Ora Auckland ilikuwa imejitetea kuwa hawawezi kukosa kuwa waangalifu na kutumia ujuzi wa hali ya juu kwa wagonjwa.

    Lakini Kamishna wa Afya na Ulemavu wa New Zealand hakukubaliana nao, kulingana na matokeo yaliyotolewa Jumatatu.

    "Wafanyikazi waliohusika katika upasuaji hawakuwa na la kusema jinsi kifaa hicho kilivyoishia kuwa ndani ya tumbo, au kwa nini hakikutambuliwa wakati upasuaji unamalizika," alisema.

    Ni kifaa kikubwa kilichotengenezwa kwa plastiki angavu na kufungwa kwenye pete mbili.

    Kwa kawaida huondolewa baada ya mkato kwenye kizazi kufungwa wakati wa operesheni kabla ya kuunganishwa kwa ngozi.

    Pia unaweza kusoma:

    • Pini ya usalama: Kifaa kidogo ambacho wanawake wa India hutumia kupambana na unyanyasaji wa kijinsia
  13. Mke wa rais wa Ukraine aelezea athari ya vita kwa familia yake

    .

    Mke wa rais wa Ukraine Olena Zelenska ameiambia BBC kuhusu athari za kihisia za uvamizi wa Urusi na athari ya vita kwa familia yake.

    Katika mahojiano ya kibinafsi, alisema ilikuwa ngumu kuona watoto wake wakiishi kwa kutokuwa na uhakika, hawawezi kupanga maisha yao ya baadaye.

    Pia alizungumza juu ya familia kukosa kuwa na wakati pamoja.

    Hii inaweza kuonekana kama ubinafsi kidogo, lakini ninamuhitaji mume wangu, wala sio mtu wa kihistoria karibu nami," alisema.

    Urusi ilipovamia Ukraine mnamo Februari 2022, kwa miezi kadhaa Olena Zelenska alikuwa mafichoni katika maeneo ya siri na watoto wake.

    Alielezea hali yake ya kihisia mwanzoni mwa uvamizi kama "hisia ya mara kwa mara ya homoni ya adrenalini". Kadiri muda ulivyopita, aliona ni “muhimu” kujituliza na kuanza kuishi katika “hali iliyopo”.

    Baada ya kuibuka kutoka mafichoni mwaka jana, vita vilimsukuma mwandishi huyo wa zamani kuangaziwa, na tangu wakati huo amezunguka ulimwengu kukutana na viongozi na kutoa hotuba.

    "Hatuishi pamoja na mume wangu, familia imetengana." Olena Zelenska aliambia BBC, "Tuna fursa ya kuonana lakini si mara nyingi kama ambavyo tungependa. Mwanangu anatamani kuwa na babake karibu."

    "Lakini tumeendelea kuwa na imani, tuna nguvu za kihisia na kimwili. Na nina uhakika tutashughulikia hili pamoja," aliongeza.

    "Inaniumiza kuona kwamba watoto wangu hawapangi chochote. Katika umri kama huo, wakiwa vijana. Binti yangu ana miaka 19. Wana ndoto ya kusafiri na kupata hisia mpya. Hana fursa kama hiyo.

    Pia unaweza kusoma zaidi:

    • Mzozo wa Ukraine: Mfahamu mke wa Rais wa Ukraine Olena Zelenask anayetafutwa na Urusi
    • Olena Zelenska: Mke wa Rais wa Ukraine aeleza alichofanya mumewe asubuhi ya kwanza Urusi ilipoivamia Ukraine
  14. Vita vya Ukraine: Sergei Surovikin 'aonekana kwenye picha ya kwanza' tangu uasi wa Wagner

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Picha iliyowekwa mtandaoni inaonekana kuonyesha jenerali wa Urusi ambaye hajaonekana hadharani tangu maasi ya kundi la mamluki la Wagner mwezi Juni.

    Sergei Surovikin anasemekana kuwa karibu na bosi wa Wagner Yevgeny Prigozhin, ambaye alifariki katika ajali ya ndege mwezi uliopita.

    Kumekuwa na ripoti kwamba Jenerali Surovikin anachunguzwa kwa uwezekano wa kushiriki katika maasi hayo.

    Lakini picha inayodaiwa kumuonyesha kamanda wa zamani wa Urusi nchini Ukraine sasa imechapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

    "Jenerali Sergei Surovikin yuko nje. Akiwa hai, mwenye afya njema, nyumbani, na familia yake, huko Moscow. Picha iliyopigwa leo, "mtu mashuhuri wa vyombo vya habari vya Kirusi Ksenia Sobchak aliandika katika maelezo kwenye picha kwenye Telegram siku ya Jumatatu.

    BBC bado haijathibitisha uhalisi wa picha hiyo, ambayo inaonyesha mwanamume aliyevalia miwani akitembea na mwanamke mwenye nywele nyekundu anayefanana na mke wa jenerali huyo, Anna.

    Mwandishi wa habari wa Urusi Alexei Venediktov aliandika kitu tofauti kwenye Telegram: "Jenerali Surovikin yuko nyumbani na familia yake. Yuko likizo na anapatikana kwa wizara ya ulinzi."

    Pia unaweza kusoma:

    • Yevgeny Prigozhin: Je, mkuu wa Wagner alikuwa ni 'maiti inayotembea?'
  15. Antony: Brazil imemwacha winga wa Manchester United baada ya tuhuma za unyanyasaji

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Brazil imemtema kikosini winga wa Manchester United Antony kufuatia madai unyanyasaji yaliyotolewa na mpenzi wake wa zamani .

    Shirikisho la kandanda la Brazil lilisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ameondolewa kwenye kikosi baada ya "mambo kujulikana" ambayo "yanahitaji kuchunguzwa".

    Chombo cha habari cha Brazil UOL kilichapisha mada yaliyotolewa na mpenzi wa zamani wa Antony siku ya Jumatatu.

    Polisi mjini Sao Paulo na Greater Manchester wanachunguza madai hayo, ambayo mchezaji huyo ameyakanusha.

    "Ninaweza kusema kwa utulivu kwamba shutuma hizo ni za uongo na kwamba ushahidi uliotolewa tayari na ushahidi mwingine utakaotolewa unaonyesha kwamba sina hatia kwa tuhuma hizo," Antony alisema kwenye mtandao wa kijamii.

    "Nina imani kuwa uchunguzi unaoendelea wa polisi utadhihirisha ukweli kuhusu kutokuwa na hatia."

    Antony anashutumiwa kwa kumshambulia mpenzi wake wa zamani Gabriela Cavallin "kwa kumpiga kwa kichwa" kwenye chumba cha hoteli mjini Manchester mnamo Januari 15, na kumwacha akiwa amekatwa kichwa ambacho kilihitaji matibabu kutoka kwa daktari.

    Pia unaweza kusoma:

    • Tetesi za Soka Ulaya Jumanne 05.09.2023
  16. Wegovy: Kampuni ya dawa za kupunguza uzito ndio yenye thamani kubwa zaidi barani Ulaya

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kampuni ya kuunda dawa za kupunguza uzito, Wegovy, imekuwa kampuni yenye thamani zaidi barani Ulayana kuondoa ufalme wa kampuni ya mavazi ya kifahari ya Ufaransa ya LVMH.

    Hisaza kampuni hiyo zilipanda baada ya kampuni kubwa ya dawa ya Denmark, Novo Nordisk, kuzindua dawa hiyo maarufu nchini Uingereza.

    Mwishoni mwa siku ya Jumatatu, kampuni hiyo ilikuwa na thamani ya soko la hisa ya $428bn (£339bn).

    Dawa hiyo sasa inapatikana katika mfumo wa huduma ya afya ya umma wa Uingereza na pia kwenye soko la kibinafsi.

    Wegovy ni dawa ya kuzuia unenepaji kupita kiasi ambayo hutumiwa mara moja kwa wiki ambayo 'huudanganya mwili' kufikiria kuwa tayari umeshiba, kwa hivyo wanaishia kula chakula kidogo na kupoteza uzito.

    Watu mashuhuri kama vile Elon Musk ni miongoni mwa watumiaji walioripotiwa wa kutumia dawa hiyo, ambayo imevutia wasanii wa Hollywood na umma kwa upana zaidi tangu ilipoidhinishwa na wadhibiti nchini Marekani mnamo 2021.

    Wegovy na Ozempic -dawa za kisukari zenye athari sawa - zimetajwa kama dawa za "muujiza".

    Lakini wataalam wanaonya kuwa tiba hizo sio suluhisho la haraka wala zinazoweka kuwa mbadala kwa lishe bora na mazoezi.

    Soma zaidi:

    • Je unajua madhara ya njia za mkato katika kutafuta kupunguza unene wa mwili wako?
    • Je, mlo wa majimaji ni salama katika kupunguza uzito haraka?
    • Je, wajua kuwa usingizi husababisha ugonjwa wa kunenepa?
  17. Habari za hivi punde, Ukraine yasema ndege zisizo na rubani za Urusi zimeanguka nchini Romania

    th

    Chanzo cha picha, EPA

    Ukraine imedai kuwa ndege zisizo na rubani za Urusi zilitua katika ardhi ya Romania wakati wa mashambulizi katika mji jirani wa Ukraine.

    Waziri wa Mambo ya Nje Dmytro Kuleba aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano na waandishi mjini Kyiv kwamba Ukraine ina ushahidi wa picha unaounga mkono madai yake.

    Hata hivyo, Romania imekataa taarifa ya Kyiv ya matukio na BBC Verify inasema haiwezi kuthibitisha picha hiyo.

    Mzozo huo ulikuja wakati viongozi wa Urusi na Uturuki wakifanya mazungumzo.

    Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikuwa amesafiri hadi mji wa Sochi nchini Urusi katika jaribio la kumshawishi rais Vladimir Putin kufufua makubaliano yaliyoiruhusu Ukraine kusafirisha nafaka kwa usalama kupitia Bahari Nyeusi.

    Bw Putin alisema makubaliano hayo, ambayo Moscow iliachana nayo mwezi Julai, hayatarejeshwa hadi mataifa ya Magharibi yatimize matakwa yake ya kuondolewa vikwazo kwa mazao ya kilimo ya Urusi.

    Lakini alisema kwamba Urusi ilikuwa ikisonga mbele na mipango ya kusambaza nafaka za bure kwa nchi sita za Afrika.

    Urusi imekuwa ikishambulia vituo vya bandari vya Ukraine kando ya Mto Danube kwa zaidi ya mwezi mmoja, ikijaribu kuzuia Ukraine kutumia mto huo kusafirisha nafaka yake nje ya nchi.

    Huku meli nyingi zikizuiwa kutumia bandari za Bahari Nyeusi za Ukrainie, Moscow inaonekana kuwa na nia ya kuzuia Kyiv kutengeneza njia mbadala zinazofaa.

    Pia unaweza kusoma:

    • Je Ukraine kupewa ndege za kivita za F-16 kutaipa ushindi dhidi ya Urusi?
    • Urusi inapanga kuichosha Ukraine kwa mashambulizi ya muda mrefu-Zelensky
    • Ndege ya kivita inayosoma akili kwa siku zijazo
  18. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo Jumanne tarehe 6 Septemba 2023