Vifo takriban 30 katika kambi DRC vinaonyesha Ebola inaweza kuwa inaenea kwa kasi

Chanzo cha picha, Reuters
Watu wasiopungua 30 wamefariki tangu mwanzoni mwa mwezi Mei katika kambi moja ya watu waliokimbia makazi yao kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Maafisa wa kambi walisema kiwango hicho cha vifo hakijawahi kushuhudiwa katika siku za nyuma, kutokana na dalili zilizoripotiwa, kunaweza kuashiria ugonjwa wa Ebola unaosambaa kwa kasi katika eneo hilo.
Haikuwezekana kuthibitisha chanzo cha vifo hivyo kwa sababu wagonjwa na ndugu zao katika kambi ya Kigonze huko Bunia — kitovu cha mlipuko wa Ebola nchini DRC — walikuwa wamekataa kufanyiwa vipimo ama kwa walio hai au waliokufa, hadi siku ya Alhamisi.
Hayo yalithibitishwa na msemaji wa kambi pamoja na shirika la misaada la Caritas.
Hata hivyo, watu wote waliokuwa wamefariki walionyesha dalili kama maumivu ya kichwa, homa na kutapika, ambazo ni dalili zinazohusishwa na Ebola.
Msemaji wa kambi, baba mmoja aliyempoteza mtoto, vyanzo vitatu vya misaada na kiongozi mmoja wa asasi za kiraia waliliambia shirika la habari la Reuters kuhusu hali hiyo.
“Hapo kabla watu hawakuwa wakifa kwa namna hii,” alisema msemaji wa kambi, Desire Grodya Bapi, katika mahojiano na Reuters.
Vifo hivyo katika kambi ya Kigonze, ambayo ina wakazi zaidi ya 15,000, vimezua hofu kwamba Ebola huenda inasambaa bila kugunduliwa miongoni mwa zaidi ya watu milioni 5 waliokimbia makazi yao mashariki mwa Congo.
Upinzani dhidi ya vipimo pamoja na hali duni ya usafi wa mazingira vinaongeza ugumu wa kudhibiti ugonjwa huo.
Soma zaidi:

















