Tonga: Volkano ya chini ya maji ikoje na ni kwa nini ilianzisha tsunami kusini mwa Pasifiki?

Chanzo cha picha, TONGA GEOLOGICAL SERVICES
Mlipuko wa volkano karibu na Tonga mnamo Januari 15 uliweka dunia nzima katika hali ya tahadhari.
Volkeno Ya Hunga Tonga-Hunga Haʻapai katika Pasifiki Kusini Ilisababisha mlipuko ambao ulisikika hadi Marekani, na kusababisha mawimbi ya zaidi ya mita moja kupiga pwani ya Tonga.
Katika taarifa yake ya kwanza kuhusu uharibifu huo, serikali Jumanne ilielezea hali hiyo kama "janga ambalo halijawahi kutokea" na iliripoti vifo vitatu vilivyothibitishwa vya watu wawili wa eneo hilo (mwanamke wa miaka 65 na mwanamume wa miaka 49) na Raia wa Uingereza. Huyu anajulikana kama Angela Glover mwenye umri wa miaka 50, ambaye kulingana na familia yake alikuwa akijaribu kuwaokoa mbwa wake lakini akasombwa na maji.
Mawasiliano katika eneo hilo yamesimama baada ya mlipuko na tsunami kukata nyaya ya chini ya bahari, na hivyo kufanya iwe vigumu kutathmini ukubwa wa uharibifu.
Lakini matokeo hayakuonekana katika visiwa vya Tonga tu. Kilomita 10,000 kutoka kwenye volcano, nchini Peru, vifo vya wanawake wawili viliripotiwa kutokana na mawimbi makubwa isivyo kawaida.
Na katika nchi nyingine, zikiwemo Japani na Chile, walitoa tahadhari kuhusu tsunami.
Volkano ya chini ya maji ni nini?
Volkano ya chini ya maji ni ile hutokea chini ya bahari.
Hutokea wakati matope ya magma kutoka ndani ya dunia hupenya kupitia nyufa hadi kwenye sakafu ya bahari.

Chanzo cha picha, EPA/Tonga Meterorology
Milipuko ya volkano ya chini ya maji ni wakati maeneo hupasuka ambapo mabamba ya ukoko wa dunia huundwa, kulingana na Ofisi ya Kitaifa ya masuala ya Bahari na Anga ya Marekani , NOAA
Katika maeneo matope ya magma huinuka na kujilimbikiza kati ya nyufa za miamba ya volcano, hadi kufikia kukosekana nafasi tena na inalipuka.
Kwa mujibu wa NOAA, robo tatu volkano kwenye sayari inalingana na milipuko chini ya maji.
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya bahari wanakadiria kuwa kuna volkeno milioni moja kwenye sakafu ya Bahari ya Pasifiki pekee.
Je, volkano ya Hunga Tonga-Hunga Ha'apai ikoje?
Volcano hiyo inajumuisha muungano wa visiwa viwili visivyokaliwa na watu, Hunga Tonga na Hunga Ha'apai, vilivyoko kilomita 65 kaskazini mwa mji mkuu wa Tonga, Nuku'alofa.
Hili ni eneo la shughuli za juu za ndani ya ardhi.
Inachomoza mita 100 juu ya bahari, lakini chini yake inafika urefu wa mita 1,800 na upana wa kilomita 20, aeleza mtaalamu wa volkano Shane Cronin, profesa wa sayansi ya Dunia katika Chuo Kikuu cha Auckland, katika makala katika ya jarida la The Conversation la nchini New Zealand.

Chanzo cha picha, CONSULATE OF THE KINGDOM OF TONGA
Mnamo mwaka 2009, 2014 na 2015 volkenohiyo ilikuwa na milipuko ya magma na mvuke, lakini ilikuwa ndogo zaidi kuliko ile ya Januari 2022.
Kulingana na Cronin, volkano hii inaweza kutoa milipuko yenye nguvu kama hii kila baada ya miaka elfu moja.
Volcano iko ndani ya kile kinachojulikana kama "caldera", ambalo ni bonde linalozidi kuwa kina kirefu baada ya kila mlipuko.
Mlipuko huo ulikuwa na nguvu kiasi gani?
Mlipuko huo wa dakika 8 ulikuwa na nguvu sana hivi kwamba ungeweza kusikika umbali wa zaidi ya kilomita 800.
Moshi na majivu vilifikia urefu wa kilomita 20 na umbali wa kilomita 260.

Huu ulikuwa mojawapo ya milipuko mikali zaidi katika eneo la Tonga katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Volcano ya Tonga ni ya aina ya basaltic, kama zile za Hawaii au Visiwa vya Kanari, yaani, milipuko yake si ya nguvu ikilinganishwa na aina nyingine za volkeno.
Milipuko ya basaltic huwa na matope ya magma yanayotiririka.
"Tofauti ni mgusano wa magma na maji ya bahari," mwanajiolojia Daniel Melnick, mtafiti katika Taasisi ya Sayansi ya Dunia ya Chuo Kikuu cha Austral nchini Chile, anaiambia BBC.
Mtaalamu huyo anarejelea ukweli kwamba wakati magma, ambayo inaweza kuwa karibu nyuzi joto 1,000, inapogusana na maji ghafla, mmenyuko mkali sana hutokea kwamba hugawanya magma.
Kile hutokea ni kwamba vipande vipya vya magma hugusana na maji, na kutoa milipuko mipya ambayo huzindua chembe za volkeno na milipuko kwa kasi ya juu zaidi.

Chanzo cha picha, NOOA
Ni kipi kilisababisha tsunami?
Kulingana na Melnick, kunaweza kuwa na sababu kuu mbili.
Ya kwanza ilikuwa mlipuko wenyewe. Mtaalamu huyo anarejelea "milipuko ya mabomu" ambayo husukuma maji mengi.
Na ya pili ni kwamba mlipuko huo ulisababisha kuporomoka kwa eneo la volcano na kuanguka chini ya maji na kusukuma maji.
"Ndiyo maana baada ya mlipuko huo kulikuwa na kipande kidogo tu cha kisiwa kilichosalia," anaelezea Melnick.
Kwa hali yoyote, Melnick na wataalam wengine wanakubali kwamba tafiti zaidi bado zinahitajika ili kuelewa vyema sababu za kutokea tsunami hii.
Ni kipi kinachoweza kutarajiwa siku zijazo?
Moshi na majivu yanayosambaa kwa wingi angani yanaingiliana pamoja na angahewa hivyo kusababisha dhoruba za umeme na upepo mkali katika eneo hilo.
Huenda ikachukua wiki kadhaa kabla ya kurudi katika hali yake ya kawaida, anasema mtaalamu huyo.
Pia wataalamu wanasema kuwa kunaweza kuwa na shughuli zaidi za volkeno, "lakini hakutakuwa na mlipuko kama huu."
"Kinachoweza kutokea ni kuporomoka tena kwa sababu udongo sio dhabiti, hali hii inaweza kusababisha tsunami nyingine, na kuwa na athari zaidi Tonga au Fiji."















