Afisa wa Marekani athibitisha mashambulizi ya Iran dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Afisa mmoja wa Marekani amethibitisha kuwa Iran ilirusha makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Marekani katika nchi jirani, zikiwemo Bahrain na Kuwait.
Awali, Wanajeshi wa Iran (IRGC) walitangaza kuwa walishambulia vituo muhimu vya kijeshi vya Marekani, vikiwemo Kambi ya Anga ya Ali al Salem nchini Kuwait na makao makuu ya Jeshi la Wanamaji la Marekani la Fifth Fleet nchini Bahrain.
Katika taarifa yake, IRGC ilisema ilitekeleza mashambulizi hayo kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani, na kwamba yalikuwa ni jibu la mashambulizi ya awali ya Marekani.
IRGC ilidai kuwa ililenga vituo vinane vya kijeshi vya Marekani, huku ikiituhumu Washington kwa kushambulia vituo vitano vya majini vya Iran kwa kile ilichokiita kisingizio cha vikosi vyake kuzuia meli katika Mlango wa Hormuz.
Hata hivyo, maafisa wa Marekani bado hawajatoa taarifa kuhusu kiwango cha uharibifu au iwapo kuna watu waliojeruhiwa au kuuawa.
IRGC pia ilisema kuwa, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, Iran ina jukumu la kudhibiti usafirishaji wa meli katika Mlango wa Hormuz na kuonya kuwa itachukua hatua kali dhidi ya meli yoyote itakayoona inakiuka sheria.
Maelezo zaidi:























