Watanzania walala gizani, umeme ukikatika ghafla

j

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Tanzania imekumbwa na kukatika kwa umeme kwa kiwango kikubwa Jumamosi jioni baada ya hitilafu ya kiufundi kuikumba Gridi ya Taifa ya Umeme, hali iliyovuruga usambazaji wa umeme katika mikoa yote iliyounganishwa na mtandao wa taifa wa usafirishaji wa umeme.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Juni 27, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilisema hitilafu hiyo ilitokea saa moja jioni, na kusababisha huduma za umeme kukatika katika maeneo yote yanayohudumiwa kupitia gridi ya taifa.

"Tanesco inaufahamisha umma kwamba leo, Juni 27, 2026, saa moja jioni, hitilafu ya kiufundi ilitokea katika mfumo wa Gridi ya Taifa ya Umeme, na kusababisha mikoa yote inayohudumiwa kupitia gridi hiyo kukosa huduma za umeme," shirika hilo lilisema.

Kukatika kwa umeme kumeathiri nyumba, biashara na taasisi za umma katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku wakazi wengi wakikumbwa na kukosekana kwa umeme ghafla wakati wahandisi wakianza juhudi za kurejesha mfumo huo.

Hata hivyo, Tanesco imesema timu zake za kiufundi zilikuwa zikifanya kazi usiku kucha kurejesha huduma ya umeme kwa awamu.

Shirika hilo halikufichua chanzo cha hitilafu hiyo wala kutoa makadirio ya muda wa kurejesha huduma kikamilifu, lakini liliwahakikishia wateja kwamba juhudi za kurejesha hali ya kawaida zilikuwa zinaendelea.

Usafiri watatizika

g

Chanzo cha picha, Tanesco

Hitilafu katika Gridi ya Taifa ya Umeme ya Tanzania Jumamosi jioni pia ilisababisha kusitishwa kwa huduma za Reli ya Kisasa ya SGR, na kuwaacha abiria wakikwama kwa saa kadhaa kabla ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuthibitisha chanzo cha usumbufu huo.

Kabla ya shirika la reli kutoa taarifa rasmi, hofu zilienea kwenye mitandao ya kijamii huku abiria wakishiriki taarifa kwamba treni zilikuwa zimesimama njiani na kutaka kufahamu kilichokuwa kikiendelea.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, TRC iliomba radhi kwa usumbufu huo, ikisema ulitokana na hitilafu ya umeme iliyoathiri gridi ya taifa.

"Shirika la Reli Tanzania (TRC) linaomba radhi kwa abiria wote kutokana na usumbufu uliojitokeza kufuatia kusimamishwa kwa huduma za treni za SGR kutokana na hitilafu katika mfumo wa Gridi ya Taifa ya Umeme," shirika hilo lilisema.

TRC ilisema juhudi za kurejesha huduma zilianza mara moja, huku timu yake ya kiufundi ikifanya kazi kwa pamoja na wahandisi wa Tanesco.

"Wataalamu wa TRC, wakishirikiana na wataalamu wa Tanesco, wanaendelea na juhudi za kurejesha huduma za treni," taarifa hiyo ilisema.

Shirika la reli halikubainisha idadi ya treni au abiria walioathiriwa na usumbufu huo.

Tukio hilo lilisimamisha kwa muda mojawapo ya mifumo mikuu ya usafiri nchini Tanzania, huku treni za SGR zinazotumia umeme zikishindwa kuendelea na safari zake hadi umeme utakaporejeshwa.