Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Homo bodoensis: Hawa ndio mababu wa moja kwa moja wa binadamu, wasema wanasayansi
Kuna kipindi katika historia ya mabadiliko ya mwanadamu ambayo wanasayansi bado hawayaelewi vizuri.
Ni kidogo kinachojulikana kuhusu enzi hizi, ambazo zinajulikana kuwa mkanganyiko , kwasababu wataalamu bado hawakubaliani kuhusu spishi ya binadamu aliyekuwepo na kwamba wanawakilisha enzi zisizojulikana kati ya Homo erectus na binadamu wa sasa.
Na sasa kundi moja la watafiti limetaja spishi mpya ambayo inaweza kuangaza kuhusu mkanganyiko, huo ambao kulingana na uchanganuzi wao, ndio mababu wa moja kwa moja wa binadamu.
Ni kuhusu Homo bodoensis , ambao waliishi barani Afrika miaka 500,000 iliopita na ambao kulingana na wanzilishi wa utafiti huo , wanasaidia kukamilisha fumbo kuhusu wakati muhimu katika mabadiliko ya binadamu.
Lebo mpya
"Mkanganyiko huo unahusiana na enzi za Middle Pleistocene, muda unaojulikana kama Chibanian tangu 2020 , na ambao ulitokea kati ya miaka 774,000 na 129,000 iliopita.
Watalaamu hatahivyo hawaelewi mabaki yanatoka kutoka kwa spishi katika kipindi hicho. Na haijulikani ni spishi ipi ilizaa nyengine.
Kipindi cha Chibanian ni muhimu kwa sababu huo ndio wakati Homosapiens waliibuka Afrika na Neanderthals huko Uropa.
Tatizo ni kwamba mabaki ya wakati huo ambayo yalitangulia Homo sapiens na Neanderthals, "hayajaelezewa vizuri na yanaeleweka kwa njia tofauti," kulingana na waandishi wa utafiti huo.
Kwa hili, watafiti wanamaanisha kuwa mabaki yaliopo kutoka enzi za Chibanian yamepewa jina kama Homo heidelbergensis au Homo rhodesiensis , aina mbili ambazo, kulingana nao, mara nyingi zimeelezewa kukinzana.
"Kuzungumza kuhusu mabadiliko ya binadamu katika kipindi hiki hakuwezekani kwa sababu ya ukosefu wa istilahi za kutosha zinazotambua tofauti za kijiografia za binadamu," Mirjana Roksandic, mtaalamu wa paleoanthropolojia katika Chuo Kikuu cha Winnipeg nchini Canada, na mwandishi mkuu wa utafiti huo, alisema katika taarifa.
Kwa hoja hii, Roksandic na timu yake walichanganua tena seti ya mabaki ya Chibanian yanayopatikana Afrika na Eurasia, na kuhitimisha kuwa orodha za Homo heidelbergensis au Homo rhodesiensis zinapaswa kusimamishwa na kuwekwa katika kundi chini ya lebo mpya ya kipekee: Homo bodoensis.
Watafiti pia wanataja kwamba baadhi ya mabaki ambayo yametambuliwa kama Homo heidelbergensis ni Neanderthals.
Kuhusu orodha ya Homo rhodesiensis, wanaongeza kuwa imekuwa lebo isiyokubalika, kwa sababu jina lake linahusishwa na Cecil Rhodes, ishara ya ubeberu wa Uingereza uliokuwepo barani Afrika.
Ukweli
Homo bodoensis inatokana na fuvu la kichwa lililopatikana Bodo D'ar, Ethiopia.
Roksandic na wenzake wanahoji kuwa Homo bodoensis ndiye babu wa moja kwa moja wa wanadamu, na anajumuisha idadi kubwa ya wanadamu wa kale wa Chibanian barani Afrika na wengine kutoka Kusini-mashariki mwa Ulaya.
Waandishi wa utafiti wanatumai kuwa matumizi ya spishi ya Homo bodoensis itasaidia kurahisisha mawasiliano na uwazi kuhusu enzi za Chibanian.
Kulingana na Roksandic aliyeithibitishia BBC Mundo, taksonomia ya Homo bodoensis tayari imekubaliwa na Tume ya Kimataifa ya Nomenclature na Zoolojia, chombo kinachosimamia matumizi sahihi ya majina ya kisayansi ya wanyama.
Tahadhari
Wataalamu wawili waliowasiliana na BBC Mundo na ambao hawakuhusika katika uchunguzi huo walieleza kutoridhishwa kwao kuhusu matokeo hayo.
"Nadhani waandishi wanaibua tatizo muhimu la muda mrefu la paleoanthropolojia ambalo linatusumbua sisi sote, lakini hawatoi suluhu mwafaka ," anasema mwananthropolojia wa paleoa Zeray Alemseged, profesa wa biolojia na anatomia ya viumbe katika Chuo Kikuu cha Chicago nchini Marekani.
Alemseged anasema kwamba ili kutatua mkanganyiko karibu na Homo heidelbergensis haitoshi kutaja aina mpya kutoka kwa fuvu.
"Hilo halitatusaidia, tunachohitaji, nadhani, ni kutafuta mabaki zaidi kutoka Ulaya na Afrika ili tuwe na uelewa mzuri," anasema Alemseged.
"Spishi aina ya Homo heidelbergensis imekuwa jina ambalo limesalia bila kutatuliwa kwa muda, kwasababu kufikia sasa hakuna mtu anayeweza kukubaliana mabaki yake yalitokana na spishi gani ," anasema McKee.
"Ninashuku kwamba, vile vile, pendekezo jipya la Homo bodoensis litakuwa moja kati ya majina ambayo hayatasalia kwa muda mrefu."
"Jina jipya la spishi litasalia iwapo watafiti wengine watalitumia," anasema.