Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
George Floyd: Derek Chauvin afungwa jela kwa zaidi ya miaka 22
Aliyekuwa afisa polisi amehukumiwa kwa kumuua Mmarekani mweusi aliyefahamika kwa jina la George Floyd huko Minneapolis mnamo Mei 2020 na kupewa kifungo cha miaka 22 na miezi sita jela.
Jaji alisema hukumu ya Derek Chauvin ilitokana na unyanyasaji wake, matumizi mabaya ya nyadhifa yake na vilevile ukatili aliouonesha kwa Bwana Floyd.
Bwana Floyd, 48, alifariki baada ya Chauvin kumkaba shingo na magoti kwa muda wa dakika tisa.
Mauaji yake yalisababisha maandamano ya kimataifa dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi.
Chauvin, 45, alihukumiwa kwa mauaji ya shahada ya pili na mashtaka mengine mwezi uliopita.
Wakati wa kesi yake, wakili wake alielezea mauaji hayo kama "kosa lililofanywa kwa nia njema".
Chauvin pia aliambiwa ajiandikishe kama mkosaji na akazuiliwa kumiliki silaha kwa maisha yake yote.
Yeye na maafisa wengine watatu wa zamani wanashtakiwa pia kwa kukiuka haki za raia kwa George Floyd.
Familia ya Floyd na wafuasi wao wameridhia adhabu hiyo.
"Hukumu hii ya kihistoria inatoa faraja kwa familia ya Floyd na kwa taifa letu ni hatua moja mbele ya uwajibikaji," wakili Ben Crump aliandika kwenye kurasa yake ya tweeter.
Dada yake Floyd, Bridgett Floyd amesema hukumu hiyo "inaonesha kuwa mambo ya ukatili wa polisi yameanza kuchukuliwa kwa uzito" lakini bado kuna safari ndefu kufika".
Rais Joe Biden alisema hukumu hiyo "ilionekana inafaa" lakini alikiri kwamba hakujua maelezo yote.
Wakati wa usikilizaji wa hukumu, kaka yake Floyd Terrence Floyd alidai kiwango cha juu kinachotakiwa kutolewa ni adhabu ya miaka 40.
"Kwanini? Ulikuwa unafikiria nini? Ni nini ulikuwa unafikiria kichwani mwako wakati ulikuwa umepiga goti kwenye shingo ya kaka yangu?" alisema.
Binti wa Bwana Floyd, Gianna, mwenye umri wa miaka saba, alionekana kwenye rekodi ya video, akisema anamkumbuka baba yake na alimpenda sana.
"Huwa ninamuulizia kila mara," alisema. "baba yangu alikuwa akinisaidia kusafisha meno yangu kila siku."
Jaji alisema kesi hiyo ilikuwa yaenye maumivu makubwa kwa jamii na nchi, lakini zaidi ya yote, kwa familia ya Floyd.
"Kile hukumu haikutegemea ni hisia, au huruma, lakini wakati huo huo, nataka kutambua maumivu makubwa na makubwa ambayo familia zote zinahisi, haswa familia ya Floyd," alisema Jaji Peter Cahill.
Chauvin aliiambia mahakama kuwa anatoa salamu za pole kwa familia ya Floyd, akisema kutakuwa na "habari zingine siku za usoni" na anatumaini kuwa zitawapa tulizo la moyo".
Ingawa, hakuomba msamaha.
Mahakamani, mama yake Chauvin alisema mwanae alikuwa "mtu mzuri".
"Daima ninaamini kuwa huna hatia na sitabadili mtazamo wangu," Carolyn Pawlenty alisema.
Ni nini kilichotokea kwa George Floyd?
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 46 alinunua pakiti ya sigara katika duka moja huko Minneapolis Kusini jioni ya tarehe 25 Mei 2020.
Msaidizi wa duka aliamini alitumia sarafu bandia ya $ 20 na akapiga simu kwa polisi baada ya Bw Floyd kukataa kurudisha sigara.
Polisi walipofika, walimuamuru Bwana Floyd atoke kwenye gari lake lililokuwa limeegeshwa na kumfunga pingu. Makabiliano yalitokea wakati maafisa walipojaribu kumtia bwana Floyd kwenye gari la kikosi chao. Walimuangusha chini na kumkandamiza.
George Floyd alikufa vipi?
Upasuaji uliofanywa kama sehemu ya uchunguzi baada ya kifo cha Bwana Floyd, haukupata ushahidi wowote wa shinikizo la kubanwa kifua au kunyongwa.
Matokeo ya uchunguzi wa daktari yameonesha kwamba Bwana Floyd alikuwa na matatizo ya moyo na mchanganyiko wa yote hayo mawili, pengine vichocheo fulani katika mfumo wake na kukandamizwa na maafisa huenda kulichangia kifo chake.
Ripoti inasema kwamba Bwana Chauvin aliweka goti lake juu ya shingo ya Bwana Floyd na kumkandamiza kwa dakika 8 na sekunde 46 - ambapo Bw.Floyd hakuamka tena.
Karibia dakika mbili kabla ya kuondoa goti lake maafisa wengine waliangalia kiganja cha mkono cha Bwana Floyd ikiwa bado mapigo ya moyo yapo lakini hawakuona chochote.
Alipelekwa katika Kituo cha Matibabu kaunti ya Hennepin kwa kutumia gari la kubeba wagonjwa na kusemekana kwamba amekufa karibu saa moja baadae.