Naomi Campbell: Mwanamitindo apata mtoto msichana

Chanzo cha picha, PA Media
Mwanamitindo Naomi Campbell amekuwa mama wa mtoto wa kike.
Campbell mwenye umri wa miaka 50 alitangaza habari hiyo kwenye Instagram wakati akiweka picha ya mkono wake akiwa ameshika miguu ya mtoto.
"Baraka nzuri hii imenichagua kuwa mama yake, nimeheshimiwa sana kuwa na roho hii ya upole maishani mwangu," aliandika kwenye mtandao huo wa kijamii
Mbuni Marc Jacobs alikuwa miongoni mwa wale waliompongeza mwanamitindo huyo aliyezaliwa London, ambaye alikuwa hajaonyesha hapo awali kuwa alitarajia kupata mtoto
Mhariri wa Vogue wa Uingereza Edward Enninful pia alitoa pongezi zake, akiandika: "Kuwaona nyinyi wawili pamoja kumeukamilisha mwaka wangu. Mtaleteana furaha'
Mama ya Bi Campbell, Valerie Morris Campbell, alichapisha kwenye Instagram: "Nimefurahi sana kwani nimengoja muda mrefu kuwa bibi."
Hakuna maelezo zaidi juu ya mtoto mchanga yamepatikana, lakini wakati wa mahojiano na jarida la the Evening Standard mwaka wa 2017 Bi Campbell alizungumzia juu ya kutaka kuwa mama.
Alinukuliwa akisema: "Ninafikiria juu ya kuwa na watoto kila wakati. Lakini sasa kwa jinsi sayansi ilivyo nadhani ninaweza kufanya hivyo wakati ninataka."
Nyota huyo aligunduliwa akiwa msichana wa shule na akawa mwanamke wa kwanza mweusi wa Uingereza kuonekana kwenye jalada la Uingereza la Vogue.
Anajulikana pia kwa kazi yake ya uhisani, na mnamo 2005 alianzisha mpango wake wa Fashion For Relief, ili kuunganisha mitindo na uhisani.













