Maoni: Je, Muungano wa Zanzibar na Tanganyika una matatizo?

p

Chanzo cha picha, unitedrepublicoftanzania.com

Maelezo ya picha, Rais wa kwanza wa visiwa vya Zanzibar, Abeid Amani Karume (kulia) na Rais wa kwanza wa Tanganyika, Julius Kambarage Nyerere
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakati Rais wa kwanza wa visiwa vya Zanzibar, Abeid Amani Karume na Rais wa kwanza wa Tanganyika, Julius Kambarage Nyerere wanachanganya mchanga, kuashiria kuunganisha nchi mbili, bila shaka hawakujua kuwa uamuzi wao ungekuwa ndio mwanzo wa mjadala mrefu na usiokwisha kuhusu muungano wenyewe.

Muungano wa April 26, 1964 kati ya Tanganyika na Zanzibar, uliozalisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeingia tena katika vichwa vya habari kwa wiki kadhaa sasa. Mjadala imezuka katika vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na vyombo vya kutunga sheria, yaani Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Mijadala kuhusu muungano si kitu kipya, imekuwepo kwa miaka mingi. Huibuka ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na nje ya chama hicho kwa maana ya vyama vya upinzani, wasomi na wanaharakati. Hata wakati marais wote wawili (Nyerere na Karume) wakiwa hai, muungano ulijadiliwa.

Bahati mbaya mjadala wa sasa wa sasa kutokana na uwepo wa mitandao ya kijamii ambayo inatoa uhuru kila mtu kusema, popote alipo, unakolezwa na lugha za matusi na kibaguzi kutoka pande zote mbili za muungano. Lugha hizi sio misimamo rasmi ya serikali zote mbili.

Mjadala wa sasa umechochewa na hoja katika baraza la wawakilishi kuhusu wasiokuwa Wazanzibari kuchukua ajira za Wazanzibari na wasiokuwa Wazanzibari kwenda kutibiwa bure Zanzibar.

Swali muhimu: Je, muungano wa Tanganyika na Zanzibar una matatizo?

Muungano una tatizo?

l

Chanzo cha picha, unitedrepublicoftanzania.com

Jibu la swali hili si gumu. Ni kweli muungano una matatizo, na kwa lugha ya kisiasa huitwa “kero za muungano” ambazo kwa miaka mingi serikali zote mbili zimekaa pamoja, ikiwemo kuunda tume, kujaribu kuzipatia ufumbuzi. Lakini bado kero za muungano zipo.

Nyuma ya muungano ambao umeunganisha nchi mbili, biashara, ndoa, udugu na hata maingiliano ya kijamii, kuna malalamiko makubwa ya kutoridhika kutoka pande zote mbili.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Walio Zanzibar hulalamika kwamba muungano umeondoa uhuru wa Zanzibar, kutoka kuwa nchi kamili iliyokuwa ikitambuliwa hadi na Umoja wa Mataifa, hadi kuwa sehemu tu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yaani ni kama kutoka kuwa nchi hadi kuwa mkoa.

Hoja ni kwamba, nchi inapoacha kuwa nchi kamili na kuwa sehemu tu ya nchi, isiyotambulika kimataifa, kwa jicho la kisiasa na kiuchumi ni tabu kusema kuwa hayo ni maendeleo, bali ni kurudi nyuma. Yaani iliyokuwa nchi yao, imemezwa ndani ya muungano.

Na walio bara hulalama kwamba muungano unawapa Wazanzibari haki ambazo Watanzania wengine hawazipati. Kwa mambo yasiyokuwa ya muungano upande wa Zanzibar yanawahusu tu Wazanzibari na mambo yasiyo ya muungano na yaliyo ya muungano kwa upande wa Tanzania bara, yanawahusu watanzania wote, wakiwemo Wazanzibari.

Wapo wanaohoji Tanganyika kama nchi iko wapi, wakati Zanzibar bado ipo. Mjadala ambao hata mwaka 1993 ulikuwepo kutoka kwa wabunge ambao kwa jina maarufu wakiitwa G-55, waliotaka kuwepo kwa serikali ya Tanganyika.

Hizi ni baadhi ya hoja ambazo zimeendelea kujirudia. Kwa hakika kuna msururu wa zile zinazoitwa kero za muungano kwa miaka mingi. Na tatizo hasa linaonekana lipo kwenye mfumo wenyewe wa muungano, ndio umezalisha changamoto na sintofahamu hizi za miaka mingi.

Juhudi za kurekebisha Muungano

l

Chanzo cha picha, mitandao

Miongoni mwa juhudi za karibuni kabisa za kutatua kero za muungano, zilionekana katika rasimu ya Katiba Mpya ya Jaji Joseph Warioba, ambayo ilipendekeza muungano wa serikali tatu, badala ya serikali mbili zilizopo sasa.

Mchakato wa kuandika Katiba mpya ulikwama mwaka 2014 baada ya Bunge Maalumu la Katiba chini ya uenyekiti wa Samwel Sitta, kupitisha Katiba Inayopendekezwa, iliyopaswa kwenda kupigiwa kura ya Ndiyo au Hapana.

Rasimu hii ilifanyiwa marekebisho kupitia bunge hilo na kurudisha serikali mbili. Katiba yenyewe bado haijapitishwa kwa sababu mchakato ulisimama na hayati rais Rais John Pombe Magufuli aliutia kabatini mchakato wenyewe.

Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan ameonesha dalili ya uwezekano wa mchakato wa kupatikana katiba mpya kurudi tena. Ingawa swali linabaki; Je mchakato huo utaanzia wapi? Kwenye rasimu iliyopendekeza serikali tatu au rasimu iliyopendekeza serikali mbili?

Ikiwa muungano utaendelea kuwa wa serikali mbili, kwa hakika mjadala kuhusu kero zake utaendelea. Na sera ya chama tawala hadi sasa bado haijaonekana kubadilika kuhusu kutoka serikali mbili na kwenda tatu.

Na wakati wa vikao vya bunge malumu, baadhi wa wanasiasa wa CCM walikuwa wakijadili katika kkutoka serikali mbili na kuwa na serikali moja. Hili linaweza kuwa rahisi kwa Tanzania bara, ingawa linaweza kuwa gumu kukubalika Zanzibar hata kwa viongozi wa CCM wa Zanzibar.

Hadi pale zile ziitwazo kero au changamoto za muungano uliodumu kwa miaka 62 zipatiwe suluhisho, tataendelea kushuhudia mjadala ikiibuka na kupotea na kuibuka tena.