Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Athari gani zinahofiwa kutokea Afghanistan baada ya majeshi ya Marekani kuondoka?
Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton ametahadharisha kutokea kwa ''madhara makubwa'' kutokana na uamuzi wa Rais Joe Biden kuondoa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan.
Bi. Clinton ameiambia CNN kuwa kuna hatari wanamgambo wa Kiislamu wa Taliban walioondolewa mwaka 2001 kwa operesheni iliyoongozwa na Marekani wanaweza kuchukua udhibiti tena nchini Afghanistan.
Marekani ina nia ya kumaliza kuondoa vikosi vyake ifikapo tarehe 11 mwezi Septemba .
Hatahivyo, Taliban wameendelea kufanya mashambulizi zaidi.
''Hiki ndicho kitu tunachokiita tatizo baya'', Bi Clinton aliiambia CNN. ''Kuna athari zinazoonekana ambazo hazikutarajiwa kukaa na kuondoka,'' alisema.
Bi Clinton, kama Bw.Biden mwanademocrat, alikuwa mfuasi wa nguvu akiunga mkono uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan baada ya mashambulizi ya 9/11 mwaka 2001.
Bw. Biden anataka kumaliza kuondoa wanajeshi wakati wa miaka 20 ya kumbukumbu ya mashambulizi hayo itakayofanyika baadaye mwaka huu.
Takriban wanajeshi 2,500 wako nchini Afghanistan wakiwa sehemu ya wanajeshi wa Nato 9,600 walio nchini humo.
Rais alisema kuwa kuondoka kwa Marekani kulihalalishwa kwani vikosi vya Marekani vilihakikisha kuwa nchi hiyo haiwezi tena kuwa kambi ya wanajihadi wa kigeni kupanga njama dhidi ya nchi za Magharibi.
Akihojiwa kuhusu uamuzi wa rais na CNN, Bi Clinton alisema ''Serikali yetu inapaswa kutazama athari kubwa mbili'', hasa kuanza kwa shughuli za vikundi vyenye msimamo mkali na kusababisha wimbi la wakimbizi baadaye kutoka Afghanistan.
Alisema uwezekano wa kuporomoka kwa serikali ya Afghanistan na uwezekano wa Taliban kuchukua udhibiti kunaweza kusababisha vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe.
Bi Clinton alisema pia ilikuwa muhimu kulinda ''raia wengi maelfu wa Afghanistan'' ambao walifanya kazi na Marekani na Nato wakati wa mzozo, na pia amesema mpango wa visa unapaswa kuundwa ili kuwasaidia wakimbizi wowote.
Vikosi vya Marekani vilivyosalia nchini Afghanistan rasmi vilianza kuondoka tarehe 1 mwezi Mei, wakati machafuko yakishika kasi.
Vikosi vya usalama vya Afghanistan viko kwenye tahadhari kubwa ya mashambulizi siku ya Jumatatu, maafisa wanasema takribani wanajeshi saba waliuawa na shambulizi la Taliban kwenye kituo cha kijeshi katika jimbo la Farah
Walisema wapiganaji walilipua kituo baada ya kuchimba handaki kwa karibu mita 400 (1312ft) kuipata kutoka nyumba iliyo karibu.
Askari mmoja alikuwa amekamatwa na waasi, walisema. Ripoti nyingine zinasema idadi ya majeruhi wa jeshi la Afghanistan ni kubwa zaidi.