John Magufuli: Viongozi wa Afrika wamuomboleza rais wa zamani wa Tanzania

Marais wa nchi za Afrika wamempa heshima za mwisho Rais wa zamani wa Tanzania John Magufuli katika shughuli ya kuuaga mwili wake jijini Dodoma.Bara "lilisikitishwa na kifo cha mwanamapinduzi," alisema Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Bwana Magufuli alifariki dunia wiki iliyopita kufuatia shida za moyo akiwa na umri wa miaka 61.
Mrithi wake Rais Samia Suluhu Hassan alimkumbuka kama mtetezi wa masikini na mcha mungu ."Hakuwa kiongozi wetu tu bali pia mlezi na mzazi kwa wengi ... na mtu mwaminifu," Rais Samia alisema.
Alipewa jina tingatinga, Bwana Magufuli alikuwa maarufu kwa watanzania wengi waliokubali mtindo wake wa utawala wa na hakupenda mzaha katika kazi.Wakosoaji, hata hivyo, walimshtumu kwa kuwa kiongozi wa kiimla na kwa kuwakandamiza wapinzani Alipuuza pia athari za virusi vya corona na kusimamisha uchapishaji wa idadi ya vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huo.
Wanasiasa wa upinzani wanasema kwamba Bwana Magufuli alikufa kutokana na Covid-19, lakini hilo halijathibitishwa.
Viongozi wa Tanzania waliohudhuria mazishi na maelfu ya watu katika uwanja wa michezo huko Dodoma hawakuvaa maski au kutii kanuni za kzuia mrundiko wa watu -Tahadhari za kiafya ambazo rais huyo wa zamani alikuwa akizipuuza.
Walakini, viongozi waliohudhuria shughuli hiyo na wajumbe wengine walivaa maski.Mwishoni mwa wiki makumi ya maelfu ya watu katika jiji kubwa zaidi nchini, Dar es Salaam, walifurika barabara ili kutoa heshima zao.
Siku ya Jumapili kulikuwa na kukanyagana katika uwanja ambao jeneza la Bwana Magufuli lilikuwa likionyeshwa - idadi ya majeruhi bado haijajulikana.Atazikwa katika mji wa kaskazini magharibi mwa Chato Ijumaa.
Je, Viongozi wa Afrika walisema nini?
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi alisema rais huyo wa zamani wa Tanzania "atakaa katika nyoyo" za wengi.
Katika risala zake , Rais wa Malawi Lazaro Chakwera alimtaja Bwana Magufuli kama "mtoto bora kabisa wa bara Afrika" ambaye "maisha yake ya utumishi" yatakumbukwa.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alimtaja kama "Mwafrika wa kweli" ambaye hakuchelea kujitangaza kama Mwafrika.Bwana Ramaphosa alimkumbuka rais huyo wa zamani kwa kuwa "shujaa" dhidi ya ufisadi, na ambaye aliwafanyia kazi watu wake.

Alisema pia rais wa Tanzania alikuwa bingwa wa utamaduni na mila za Kiafrika, haswa utumiaji wa Kiswahili, lugha ya Afrika Mashariki, katika bara zima.
"Kiswahili kimeanzishwa katika shule za Afrika Kusini kama heshima kwa Marehemu Rais John Magufuli ambaye alisisitiza juu ya matumizi yake," Bwana Ramaphosa alisema.Hii iliungwa mkono na Rais wa Botswana Mokgweetsi Masese, ambaye alisema kuwa Bwana Magufuli alikuwa "mwalimu mzuri", kama Rais mwanzilishi wa Tanzania Julius Nyerere."Hata huko Botswana alitarajia sisi tuzungumze Kiswahili… Sisi pia tumeanzisha Kiswahili katika mitaala yetu."

Katika risala yake , Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pia alimshauri mrithi wa Bw Magufuli, akisema: "Kwako dada yangu na sasa mwenzangu, barabara umeshaonyeshwa na ndugu yetu Rais Magufuli."
"Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Umoja wa Afrika kwa pamoja wamehuzunishwa na kifo cha mwanamapinduzi Dkt John Magufuli. Tunawaombea watanzania. DR Congo iko pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu," alisema Rais Tshisekedi, ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.














