Sababu tatu zinazozuia meli kupita Hormuz licha ya makubaliano ya Marekani na Iran

Husafirishwa kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz wakati wa machweo ya jua
Maelezo ya picha, Husafirishwa kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz wakati wa machweo ya jua
    • Author, Thomas Copeland
    • Author, Shruti Menon
    • Author, Barbara Metzler
    • Nafasi, BBC Verify
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati Rais wa Marekani, Donald Trump, alipotangaza makubaliano kati ya Marekani na Iran Jumapili na kueleza kuwa Mlango Bahari wa Hormuz umefunguliwa tena, alihitimisha ujumbe wake kwenye mtandao wake wa Truth Social kwa maneno: "Meli za dunia, washeni injini zenu. Mafuta yaanze kusafirishwa."

Hata hivyo, uchambuzi wa BBC Verify wa takwimu za ufuatiliaji wa meli kutoka MarineTraffic unaonyesha kuwa ni meli saba pekee zinazoonekana kupita katika njia hiyo muhimu ya maji tangu makubaliano hayo yatangazwe. Wakati huohuo, takribani meli 580 zinaonekana kusubiri ndani ya Ghuba ya Uajemi.

Iran ilifunga shuguli zote katika Mlango Bahari wa Hormuz, ambao hupitisha karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi ya dunia, kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel ya tarehe 28 Februari.

Wataalamu wanasema bado kuna vikwazo vikubwa vinavyozuia usafiri wa baharini kurejea katika kiwango cha kawaida kilichokuwapo kabla ya mzozo huo. Miongoni mwa changamoto hizo ni masuala ya usalama, mabomu ya baharini na ada za kupita.

Takwimu za MarineTraffic za Jumanne zinaonyesha kuwa zaidi ya meli 250 za kubeba mafuta na zaidi ya meli 330 za mizigo ziko ndani ya Ghuba hiyo.

Takribani asilimia 75 ya meli hizo za mafuta zimesimama bila kusonga. Picha za satelaiti zinaonyesha nyingi zikiwa karibu na vituo vikuu vya usafirishaji wa mafuta nchini Saudi Arabia, Iraq na Falme za Kiarabu.

Idadi halisi ya meli zilizoko katika eneo hilo huenda ikawa kubwa zaidi, kwa kuwa meli nyingi hazitangazi mahali zilipo kupitia mifumo ya ufuatiliaji wa baharini na hivyo hazionekani katika takwimu za MarineTraffic.

Mchambuzi mkuu wa soko la mafuta katika kampuni ya Kpler, Naveen Das, anasema ishara ya kwanza ya kurejea kwa shughuli za kawaida ingekuwa kuanza kwa meli zilizokwama ndani ya Ghuba kuondoka kwa wingi.

Hata hivyo, hadi sasa hali hiyo bado haijashuhudiwa

Taswira ya satelaiti inayoonyesha kundi la meli zikiwa zimetia nanga kutoka Iraq karibu na kituo cha mafuta cha baharini

1. Wasiwasi kuhusu usalama

"Nahodha atahitaji kuwa jasiri sana kupita katika Mlango Bahari wa Hormuz katika mazingira ya sasa," anasema Martin Kelly wa kampuni ya usimamizi wa migogoro ya EOS Risk Group akiambia BBC Verify.

Tangu Iran ilipoanza kuzuia kwa vitendo matumizi ya mlango huo mwishoni mwa Februari, imekuwa ikifyatua risasi dhidi ya meli zilizojaribu kupita bila ruhusa yake.

Marekani nayo iliweka mzingiro wa kijeshi katika bandari za Iran tarehe 13 Aprili na tangu wakati huo imedai kuzizuia meli tisa ambazo haikuzitambua kama zinazofuata masharti yake, ikiwemo kushambulia vyumba vya injini za baadhi ya meli kwa makombora ya Hellfire.

Ingawa Trump alitangaza kuondolewa mara moja kwa zuio hilo la kijeshi, baadaye alisema utaendelea hadi makubaliano na Iran yatakapotiwa saini rasmi.

Picha za satelaiti za tarehe 15 Juni zilionyesha meli nne za kivita za Marekani karibu na eneo la zuio hilo katika kiingilio cha ghuba ya Oman.

Picha za satelaiti za meli nne za kivita za Marekani
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wataalamu wanasema kwamba baada ya tangazo la makubaliano hayo, wamiliki wa meli, makampuni ya bima na manahodha wameanza kujiandaa kwa safari za kutoka Ghuba kuelekea Bahari ya Arabia. Hata hivyo, hakuna anayependa kuwa wa kwanza kuchukua hatari hiyo.

"Tunachoona bado ni mtazamo wa kusubiri na kuona. Hakuna anayependa kuwa wa kwanza kujaribu," anasema Das.

"Baadhi ya wamiliki na manahodha ambao wanaonekana kuwa na uthubutu, kama kampuni fulani za Ugiriki, tunaweza kuwaona wakiingia na kutoka kwa mafanikio na hiyo inaweza kujenga imani kwa wengine," alisema.

Manahodha wengi watakumbuka matukio ya mwanzoni mwa mwezi Aprili wakati waziri wa mambo ya nje wa Iran alipotangaza kuwa mlango wa bahari ulikuwa wazi kabisa, alisema Michelle Wiese Bockman, mchambuzi mkuu wa shirika la ujasusi la Windward Maritime.

Siku moja tu baadaye, mamlaka ya Irani ilisema mlango wa bahari ulikuwa umefungwa na zaidi ya meli 33 zililazimika kubadili njia katikati ya usafiri huku kadhaa zikiripotiwa kurushwa, Bockman alisema.

"Tunahitaji kusubiri kwa siku kadhaa, labda hadi Ijumaa, kuona jinsi hali itakavyokuwa," alisema Martin Kelly.

2. Tishio la mabomu ya baharini

Mwanzoni mwa mzozo huo, Iran ilitishia kuwa ikiwa pwani au visiwa vyake vingeshambuliwa, ingetega mabomu mbalimbali ya baharini, yakiwemo mabomu yanayoelea majini.

Tangu wakati huo, Kituo cha Pamoja cha Taarifa za Usalama Baharini pamoja na Kituo cha Usalama wa Bahari cha Oman vimetoa tahadhari kuhusu vitu vinavyoelea vinavyoshukiwa kuwa mabomu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, pia aliwaambia maseneta kuwa Iran imeweka mabomu katika sehemu kubwa za Mlango Bahari wa Hormuz.

Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini, Arsenio Dominguez, ameiambia BBC kuwa kuondolewa kwa mabomu hayo ni hatua muhimu kabla shughuli za kawaida za usafiri wa baharini hazijarejea.

Wataalamu wanakadiria kuwa operesheni ya kusafisha mabomu inaweza kuchukua kati ya siku 30 hadi miezi sita.

"Tatizo ni kwamba hatujui hali halisi ilivyo, na ukosefu huo wa uhakika unatisha," anasema Phillip Belcher wa Chama cha Kimataifa cha Wamiliki Huru wa Meli za Mafuta.

Picha ya FRA Lyne Bay baharini

Chanzo cha picha, Royal Navy

Wataalamu wanaamini njia ya kusini karibu na Oman inaonekana kuwa salama zaidi, huku juhudi kubwa zikielekezwa katika kusafisha njia kuu ya usafiri.

Meli za kusafisha mabomu hulazimika kwenda kwa mwendo wa taratibu sana ili kuchunguza mazingira ya chini ya maji kabla ya kufungua njia salama kwa meli nyingine.

"Zinalazimika kusafiri kwa mwendo wa polepole sana, huenda wa mafundo mawili au matatu tu, ili ziweze kufanya uchunguzi wa mazingira yaliyoko chini ya maji," alisema Kelly.

(Fundo moja la baharini ni sawa na takribani kilomita 1.85 kwa saa.)

Uingereza na Ufaransa tayari zimepeleka meli za kijeshi katika eneo hilo kwa maandalizi ya operesheni ya kuondoa mabomu.

Wataalamu wanasema kuwa baada ya hapo, meli maalumu za kusafisha mabomu ya baharini zitapaswa kufungua njia pana na salama ya kutosha ili kuruhusu meli kupita kwa wakati mmoja zikiingia na kutoka katika Mlango Bahari wa Hormuz.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amesema nchi yake itatoa mchango wake kamili katika kuhakikisha Mlango Bahari wa Hormuz unafunguliwa tena haraka iwezekanavyo.

Meli ya usaidizi ya Jeshi la Wanamaji la Uingereza, RFA Lyme Bay, ambayo imewekewa vifaa vya kutambua na kutafuta mabomu ya baharini, ilionekana jana kwenye mifumo ya ufuatiliaji wa meli ikiwa karibu na kituo cha anga cha kijeshi cha RAF Akrotiri nchini Cyprus.

3. Ada za kupita

Kwa muda mrefu, meli zimekuwa zikipita katika Mlango Bahari wa Hormuz bila kulipa ada yoyote kwa kuwa ni njia ya asili inayopitia katika maji ya Iran na Oman.

Ingawa Marekani na Iran si wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria za Bahari (UNCLOS), unaozitaka nchi kuhakikisha meli zinapita kwa usalama katika maji yao, wataalamu wanasema msimamo wa Marekani ni kwamba haki ya kupita kwa uhuru katika Mlango Bahari wa Hormuz ni sehemu ya sheria za kimataifa zinazotambulika na kutumika kwa kawaida na mataifa yote.

Kwa upande mwingine, baadhi ya njia za maji zilizojengwa na binadamu, kama vile mfereji wa Panama na mfereji wa Suez, hutoza ada kwa meli zinazozitumia ili kugharamia huduma mbalimbali zinazotolewa wakati wa safari.

Hata hivyo, wakati wa mzozo huu, Iran imejaribu kuimarisha mamlaka yake juu ya mlango huo kwa kuanzisha mamlaka maalumu iliyopewa jukumu la kusimamia vibali vya usafiri salama.

Marekani na washirika wake wa nchi za Ghuba wamekuwa wakipinga mara kwa mara juhudi za Iran za kudhibiti au kuweka mamlaka yake juu ya Mlango Bahari wa Hormuz.

Alipotangaza makubaliano kati ya Marekani na Iran tarehe 14 Juni, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema kuwa Mlango Bahari wa Hormuz ungefunguliwa tena kwa meli kupita bila kutozwa ada yoyote.

Lakini shirika la habari la Fars la Iran limeripoti kuwa chini ya makubaliano mapya, Iran kwa kushirikiana na Oman inaweza kusimamia njia hiyo na hata kutoza ada za huduma kwa meli zinazopita.

Wataalamu wanaonya kuwa mfumo wowote mpya wa malipo unaweza kuongeza changamoto mpya katika usafirishaji wa baharini na hata kupunguza idadi ya meli zinazoweza kupita kila siku.

Maswali mengi bado hayajajibiwa: Nani atasimamia mfumo huo? Utatekelezwaje? Ada zitakusanywaje? Na mataifa mengine ya Ghuba yatauchukuliaje?

Ingawa baadhi ya maswali hayo yanaweza kujibiwa baada ya makubaliano rasmi kutiwa saini, wataalamu wanaamini kuwa hata Mlango Bahari wa Hormuz ukifunguliwa kisiasa, shughuli za kibiashara hazitarejea mara moja katika hali ya kawaida.

"Kufunguliwa kwa mlango huo kunaweza kutokea haraka kwa mtazamo wa kisiasa au kiusalama, lakini kurejea kwa mfumo wa kawaida wa biashara ya meli kutakuwa mchakato wa taratibu," anasema Dimitris Ampatzidis wa Kpler.

BBC Verify banner