Kwa nini viongozi wa dini ya Kiislamu wanakamatwa Urusi?

Chanzo cha picha, telegram
Vikosi vya usalama vya Urusi hivi karibuni vimewakamata viongozi kadhaa wa dini ya Kiislamu na wanaharakati kadhaa wa kijamii. Vyombo vya habari vya serikali havijaripoti habari hizo, lakini masimulizi mengi kuwahusu yameibuka mtandaoni.
Kwa vyombo vya habari na chaneli za mrengo wa kulia, kukamatwa huku kulikuwa mwanzo wa kampeni iliyosubiriwa kwa muda mrefu ya kuvunja Jukwaa la Kidini la Waislamu wa Shirikisho la Urusi, taasisi inayoungwa mkono na Kremlin inayohusika na kuwawakilisha Waislamu.
Kwa vyombo vya habari vilivyo uhamishoni, matukio haya ni ishara ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu nchini Urusi, huku wengi wakielekeza kuhusu sheria mpya yenye utata ambayo inapiga marufuku sala za jamaa katika "majengo ya makazi."
BBC Monitoring imechunguza wimbi la kukamatwa, majibu ya viongozi wa dini wa eneo hilo na hatima ya jamii za Kiislamu nchini Urusi.
Waliokamatwa na kushtakiwa
Ripoti zinaonyesha kwamba viongozi wanane na wawakilishi wa jamii za Kiislamu walikamatwa Mei 2026. Mmoja wao aliachiliwa baadaye.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Wissam Bardwill, mufti wa zamani wa eneo la Karelia. Bw. Bardwill alihukumiwa kifungo cha siku 15 jela baada ya kudaiwa "kutotii amri za polisi" katika uwanja wa ndege wa Sheremetyevo Mei 14, shirika la habari la serikali la TASS liliripoti.
Pia, kulingana na ripoti ya chombo cha habari cha ndani cha Furtanga, Mei 12, Huduma ya Usalama ya Shirikisho la Urusi ilimkamata mwanazuoni wa Ingush, Akhmad Tangiyev na naibu wake Wissam Bardwil.
Tovuti maarufu ya habari ya Urusi Lenta.ru iliripoti kwamba Rael Asaynov, mufti wa Jamhuri ya Mordovia, alikamatwa Mei 19 kwa tuhuma za "hongo," akinukuu chanzo cha juu katika Baraza la Mufti la Urusi
Gazeti la biashara la Kommersant lilichapisha orodha ndefu ya wafungwa Mei 23, likinukuu ofisi ya vyombo vya habari ya mahakama na wachunguzi kadhaa ambao hawakutajwa majina.
Kulingana na Kommersant, Mohammad Khani, mkuu wa zamani wa shirika la kidini la Jumuiya ya Waislamu Kaskazini-Magharibi, amekamatwa huko St. Petersburg. Mmoja wa jamaa zake, pamoja na Nidal Awadullah Ahmed, naibu mufti wa eneo la Saratov nchini Urusi, pia walikamatwa.
Tovuti hiyo pia ilichapisha herufi za kwanza na za mwisho za majina ya wafungwa wengine wanne. Chombo cha habari cha uchunguzi "Agentstvo" kiliwatambua kuwa ni wawakilishi wa vituo vya jamii za Waislamu huko Tatarstan, Murmansk na Petrozavodsk.
Kwa nini walikamatwa?

Chanzo cha picha, rbc
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kukamatwa huku kulifanywa kwa sababu mbalimbali kuanzia "hongo" hadi "kutotii," lakini wanablogu na vyombo vya habari viliibua shutuma nzito zaidi.
Nyaraka za kesi, ambazo Kommersant inaripotiwa kuzipitia Mei 23, zinadai kwamba baadhi ya watu hawa walikuwa wamejiunga na Muslim Brotherhood, shirika ambalo limepigwa marufuku nchini Urusi tangu 2003.
Mwanaharakati wa vyombo vya habari anayeunga mkono serikali Ruslan Ostashko pia alirudia madai ya kuwa wana uhusiano na Muslim Brotherhood, pia aliwaelezea viongozi hao kuwa wanashirikiana na "mashirika ya ujasusi ya kigeni" na taasisi za Umoja wa Ulaya.
Vituo vya mrengo wa kulia vilikaribisha habari za kukamatwa kwa watu hao, vikionyesha waziwazi hamu yao ya muda mrefu ya kukandamiza Baraza la Mufti la Urusi.
Kituo cha mrengo wa kulia cha Sons of the Monarchy kiliandika Mei 19: "Vikosi vya usalama vya Urusi hatimaye vimewashughulikia wachochezi ambao wanachochea mzozo wa kidini nchini Urusi."
Kituo hicho kiliongeza: "Natumai huu ni mwanzo tu!"
Katika chapisho lililoandikwa na mwanablogu Yuri Baranchik Mei 21, anasema: "Wapenzi hawa wa mchakato wa kueneza 'Uislamu' na 'kueneza hijabu katika jamii ya Urusi' kwa muda mrefu wamestahili kufungwa jela. ... Inaonekana mtu katika utawala ghafla amegundua ukubwa na kiwango cha tishio hili.”
Mzozo kuhusu Urusi
Mojawapo ya kesi zenye utata zaidi ilifunguliwa Mei 29. Ilimhusisha Damir Mukhitdinov, naibu wa kwanza wa Ravil Aynuddin, mkuu wa Taasisi ya Kidini ya Waislamu wa Shirikisho la Urusi, ambaye alishtakiwa kwa "kuchochea chuki au uadui," kulingana na gazeti la biashara la RBC.
Siku tatu baadaye, gazeti la biashara la Vedomosti liliripoti kwamba Damir Mukhitdinov alitozwa faini ya rubles 150,000 (karibu dola 2,040) kwa kuonyesha michoro ya enzi ya Wamongolia.
Mchoro huo, ambao ulionekana ukutani mwa ofisi yake wakati wa mahojiano mwaka jana, unaonyesha Vita vya Kalka 1223, vita ambavyo vinachukuliwa kuwa hatua ya mabadiliko katika uvamizi wa kwanza wa majeshi ya Mongol katika Ulaya Mashariki.
Suala hilo lilisababisha wimbi la ukosoaji miongoni mwa wanablogu wanaounga mkono vita, wanaharakati wa kizalendo, na hata baadhi ya maafisa wa serikali. Baadhi walielezea mchoro huo kama chuki dhidi ya Urusi na wakataka Baraza la Mufti la Urusi, ambalo liko karibu na Kremlin, liitwe shirika la "msimamo mkali".
Damir Mukhitdinov mwanzoni alikataa shutuma za chuki dhidi ya Urusi na akatetea mchoro huo, akisema "Golden Horde" (taifa lililopotea la Milki ya Mongol katika karne ya 13) lilisababisha kuunganishwa kwa Urusi, uundaji wa taifa la Urusi, na maendeleo ya Urusi kama nchi ya makabila mengi na dini nyingi.
Lakini baadaye aliliondoa. "Nimeamua kuondoa picha hii," Damir Mukhtydinov alisema katika taarifa iliyochapishwa mwaka 2025, kwenye tovuti rasmi ya Baraza la Mufti la Urusi.
"Mahali pake itawekwa picha kuhusu matukio ya Vita vya Kizalendo [vita vya Umoja wa Kisovieti dhidi ya Ujerumani ya Nazi]."
Damir Mukhitdinov, katika jaribio la kusisitiza ujumuishaji wa Urusi ya kisasa, anaonekana kuachana na mfumo wa simulizi la kipekee la kihistoria la serikali.
Baraza la Mufti la Urusi linasema nini?
Baraza la Mufti la Urusi lilibaki kimya huku habari za kukamatwa kwao zikiingia polepole kwenye vyombo vya habari vikuu.
Chanzo kisichojulikana ndani ya baraza hilo kilisema baraza halioni "dalili za kukamatwa kwa watu wengi" au "kampeni dhidi ya Waislamu," kulingana na ripoti ya tovuti inayounga mkono Kremlin Lenta.ru Mei 21.
Wakati huo huo, Rashid Abdurrashidov, naibu mufti wa Mordovia, alimtetea mwenzake Rael Asaynov wakati wa kukamatwa kwake, akiita tukio hilo "kutoelewana”.
Wiki chache baadaye, Ravil Gaynotdin, Mufti Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Mufti la Urusi, hatimaye alitoa taarifa rasmi kuhusu ripoti hizo.
"Tunakataa kabisa madai yaliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari na wanablogu kwamba Baraza la Waislamu wa Shirikisho la Urusi linahusishwa na msimamo mkali, ushawishi wa kigeni, na mvutano wa kikabila," alisema mnamo Juni 8.
Alisema majaribio ya kuionyesha taasisi hii kama chanzo cha itikadi kali yatachochea mgawanyiko na kuwanufaisha wapinzani wa kigeni.
Katika taarifa yake hakutaja kukamatwa, kuhojiwa, au mashtaka na alisisitiza tu utayari wa shirika "kushirikiana na mamlaka za shirikisho na za kikanda."
Hili halishangazi, kutokana na utiifu wake wa muda mrefu kwa Vladimir Putin.
Dalili za ukandamizaji

Chanzo cha picha, Tsargrad
Hata hivyo, Ravil Gaynotdin aliwomba Putin kuingilia kati mapema Mei kupinga muswada ambao ungepiga marufuku sherehe za kidini na sala za kusanyiko katika majengo ya makazi.
Mpango huo, uliowasilishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2024, umepokea uungwaji mkono kutoka kwa wanasiasa mashuhuri kutoka chama tawala, akiwemo Pyotr Tolstoy, kiongozi wa bunge Sergei Mironov, na Leonid Slutsky, kiongozi wa Chama cha Kidemokrasia cha Liberal cha Urusi.
“Mpango huu unamaanisha kwamba ni wakazi waliosajiliwa katika makazi, ndio pekee wanaweza kusali katika makazi hayo. Inawezekana mtu kuhesabiwa kuwa amevunja sheria ikiwa ataswali na jamaa au marafiki wakati wa kuwatembelea,” Ravil Gaynotdin aliandika katika barua ya wazi kwa Putin Mei 6.
Alisema mpango huo unakiuka haki ya kikatiba ya kufuata dini na unaweza kusababisha misimamo mikali kwa watu.
Pia alidokeza kwamba mpango huo unalenga jamii za Waislamu, kwani kuna ukosefu wa nafasi katika maeneo ya umma kwa Waislamu kusali na mamlaka hazitoi vibali vya kujenga misikiti, vituo vya kitamaduni, na maeneo ya ibada, maeneo ambapo sala za jamaa zingekuwa halali chini ya sheria iliyopendekezwa.
Chombo cha habari kilicho uhamishoni Novaya Gazeta Europa kiliandika mpango huo ni "mbinu ya kupinga wahamiaji."
Kuanzia 2023 kumekuwa na mfululizo wa "uvamizi" kwenye maeneo ya ibada ya Waislamu kote nchini, ambapo wahamiaji walikamatwa na kupelekwa moja kwa moja kwenye ofisi za usajili na uandikishaji wa kijeshi, kimesema chombo hicho.
Utii hausaidii tena
Zaidi ya Waislamu milioni 20 wanaishi Urusi, idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya, huku wengi wao wakiishi katika maeneo ya Kaskazini mwa Caucasus na Volga.
Baada ya vita vya kujitenga vilivyozuka katika enzi ya baada ya Usovieti, Putin aliunda msururu wa miundo ya utawala katika jamhuri za Kiislamu za Urusi.
Serikali ilitaka kuonyesha taswira ya mshikamano wa dini mbalimbali kwa kufadhili miradi ya ujenzi wa misikiti ya gharama kubwa na kuweka viongozi wanaotii sheria, akiwemo Rais wa Chechnya Ramzan Kadyrov.
Sambamba na sera za serikali, taasisi za Kiislamu nchini Urusi (ikiwa ni pamoja na Baraza la Kidini la Waislamu wa Shirikisho la Urusi) zimetoa msaada wa nyenzo na kiitikadi katika vita vya Urusi nchini Ukraine.
Wakati huo huo, wafuasi wa Putin, wapenda vita wamezidi kuvutiwa na maono ya "Urusi ya Kikristo."
"Chuki dhidi ya Uislamu na hisia za kupinga wahamiaji zilikuwepo hapo awali, lakini vita vimechukua jukumu muhimu katika kuimarisha na kuangazia hisia hizi," msomi wa Kiislamu ambaye hakutajwa jina alikiambia chombo huru cha habari cha Doxa Mei 21.
Hapo awali, gharama ya tofauti za kidini nchini Urusi ililipwa kwa utiifu wa kisiasa. Lakini kama gazeti la Novaya Gazeta Europa lilivyosema, wimbi la hivi karibuni la kukamatwa watu limezua swali, huenda kiwango hicho cha utiifu hakitoshi tena.















