Serikali ya Equatorial Guinea yajiuzulu kwa kushindwa kufikia malengo yake

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Serikali ya Guinea ya Ikweta imejiuzulu baada ya kushindwa kutimiza malengo yake, Makamu wa Rais Teodoro Nguema Obiang Mangue amesema.
Obiang, ambaye pia ni mtoto wa Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, alisema waziri mkuu aliwasilisha tangazo la kujiuzulu kwa wanachama wote wa serikali kwa sababu ilikuwa imefikia 10% ya malengo yake.
Hakutaja malengo lakini taarifa ya chama tawala ilisema rais ameona kuwa serikali inakuza ufisadi na imeshindwa kuleta mseto wa uchumi.
Rais Obiang ndiye kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani na kuitawala nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ya Afrika Magharibi tangu mwaka 1979 kwa mkono wa chuma, huku akiwateua jamaa zake kushikilia nyadhifa muhimu serikalini.
Rais aliteua serikali inayoondoka mwaka 2024, huku Manuel Osa Nsue Nsua akiwa waziri mkuu.
Siku ya Jumanne, makamu wa rais alisema hatua hiyo inaambatana na "kanuni kwamba wajibu katika usimamizi wa umma lazima uambatane na matokeo".
"Kiwango cha utekelezaji kilichopatikana hakitoshi kuhusiana na matarajio na ahadi zilizofanywa," aliandika kwenye mtandao wake wa X.
Katika taarifa kwenye Facebook, chama tawala nchini Guinea ya Ikweta (PDGE) kilisema rais hakuridhishwa na usimamizi wa serikali inayoondoka.
Serikali mpya inatarajiwa kuteuliwa.

























