Kifo cha Magufuli: Namna gani Magufuli aliyagusa maisha ya watu wenye kipato kidogo?

Magu
    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
  • Iliyochapishwa

Hayati John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, daima alisisitiza yeye ni Rais wa wanyonge na serikali yake ipo kwa ajili ya kuwatetea.

Aliyagusa maisha ya watu wa chini kwa kiasi kikubwa; hasa kwa maamuzi yake aliyoyatoa kila apitapo.

Hakuchelea kusikiliza sauti za wanawake waliomlalamikia mambo mbalimbali.

tz

Chanzo cha picha, Ikulu

Huku kachomoza na kipaza sauti akiwa nusu mwili kutoka garini.

Alikuwa ni msikilizaji mzuri panapohusika sauti za malalamiko yaliyogusa maisha ya watu.

Ingawa kuna watakao mkosoa kwamba hakuwa msikilizaji mzuri zinapokuja sauti za wapinzani wake kisiasa.

Juhudi zake za dhati

M

Chanzo cha picha, IKULU

Wakati akizindua Kituo Kikuu cha Kimataifa cha Mabasi cha Dar es Salaam, kilichopo Mbezi-Luis, siku ya Jumatano, Febuari 24, 2021. Magufuli alitoa agizo kwa wateule wake.

"Mkiwafukuza Wamachinga hapa wakati stendi imeandikwa ni Stendi ya Magufuli itaonesha Magufuli ndiye anawafukuza, sitokubali. Watengenezewe utaratibu, abiria wakanunue chakula kwa wamachinga. Mihogo na matikiti maji nayo yanunuliwe. Hiyo ndiyo serikali inayojali wananchi wake."

Hili ni moja ya agizo la mwisho mwisho katika utawala wake, miongoni mwa maagizo mengi mfano wake, aliyoyatoa kama sehemu ya kutekeleza kawaida yake ya kutetea wafanyabiashara wa mitaji midogo.

Ni wakati wa utawala wake ndipo wamachinga wa Kariakoo walipopewa rasmi mitaa kumi ya kufanyika biashara katika soko hilo kubwa. Maelfu kwa maelfu wananufaika na uamuzi huo hadi leo.

Katika ziara yake mkoani Morogoro Julai 2017, alitoa agizo kwa viongozi wa manispaa na mkoa huo, kuacha kuwaondoa wafanyabiashara wadogowadogo. Wakiwemo mamantilie, bodaboda katika kituo cha mabasi ya mikoani cha Msanvu.

Hayati Magufuli alikuwa na ziara za mara kwa mara katika mikoa ya nchi.

Kila apitapo alitoa fursa kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi papo hapo. Huku wananchi wakipiga vigelegele na makofi kwa kukunwa na aliyokuwa akiyafanya.

Mbele ya kadamnasi, kero nyingine zilisababisha watumishi wa umma kusimamishwa kazi ama kufukuzwa kwa sababu ya uzembe.

Vijasho vilikuwa vinawatoka wanapowekwa kiti moto kujibu malalamiko ama tuhuma mbele ya kamera.

Wakosoaji na waungaji mkono

M

Julai, Mosi 2020 . Benki ya Dunia iliitangaza rasmi Tanzania kuingia katika uchumi wa kipato cha kati ngazi ya chini.

Na kujiunga na mataifa mengine saba ya eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Kwa mujibu wa dira ya maendeleo ya Tanzania, taifa hilo lilipanga kuingia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kwa maana hiyo utawala wake ulifanikiwa kukimbia na kuwa mbele ya muda.

Baada ya kifo chake, kurasa za mbele za magazeti yenye mrengo wa kiserikali, yalijikita kuweka picha za miradi mikubwa iliyofanyika na inayoendelea kufanyika. Kama sehemu ya kumbukumbu ya mafanikio ya utawala wake.

Ingawa wapinzani wake kisiasa hujenga hoja kuwa alijikita zaidi kuangazia maendeleo ya vitu.

MAELEZO

Chanzo cha picha, MAELEZO

Akijenga miradi mikubwa ya mamilioni ya pesa za walipa kodi na mikopo kutoka nje. Huku akisahau maisha ya hao walalahoi na wanyonge.

Wakosoaji wake wanaamini kasi yake ya kuanzisha miradi hiyo, hasa katika miundo mbinu na usafiri haikuenda sawa na kasi ya maendeleo katika maisha ya mtu moja moja.

Misemo ya, 'tunaisoma namba,' 'chuma kimekaza.' Ilizuka miongoni mwa wananchi kuelezea hali ngumu wanayopitia wakati wa miaka yake mitano madarakani.

Raia walipolalamika ugumu wa maisha na upatikanaji wa fedha. Magufuli alijibu kwa ukali kwamba wanatakiwa wafanye kazi. Akinukuu Bibilia kupigilia msumari hoja yake, 'na asiyefanya kazi na asile.'

Na wale waliolalamika ukosefu wa pesa, akiwajibu kwa kusema walizoea pesa za kupiga dili ambazo katika utawala wake hazipo tena. Wasahau!

Kwa ufupi juhudi zake za kupambana na umasikini hazikumkuna kila mtu. Wapo ambao waliona mbinu na sera zake zimezidi kuleta hali mbaya. Ubanaji wake ulikuwa kama mtego wa panya, haukuathiri walaji pekee, bali hata ambao hawakuwahi kula.

Je, alifanikiwa kuwavuusha katika umasikini?

MA

Chanzo cha picha, Getty Images

Hoja ya ikiwa utawala wake chini ya juhudi zake za dhati, miradi mikubwa na uchumi wa kati.

Yamefanikiwa kuyabadilisha maisha ya watu wa kipato cha chini.

Ni ukakasi mkubwa kusema yamefanikiwa.

Kwa sababu Tanzania kama yalivyo mataifa mengine masikini, bado raia wake wanajiona wako katika umasikini uleule wa jana na juzi.

Hushukuru wa kupewa fursa lakini umasikini wa kitaifa bado unawaandama.

Ripoti za mashirika makubwa zinapokuja na kueleza ukuaji wa uchumi.

Athari chanya ya ukuaji huo haiokekani moja kwa moja katika maisha ya wanyonge. Kwa sababu bei ya mchele, sukari, unga inaendelea kubaki ileile ile na wakati mwingine hupanda. Na wengi wao kipato ni kilekile.

Ambalo halina mjadala kuhusu utawala wa Magufuli na raia wa hali ya chini, ni kwamba aliwajali kwa maneno na vitendo. Aliwatatulia baadhi ya kero kubwa na kuwarahisishia ufanyaji wa shughuli zao.

Yumkini lengo lake la kuwavuusha katika tope la umasikini haikufanikiwa kwa asilimia mia moja. Bali juhudi zake za dhati zilionekana.

Na hilo ndilo ambalo sehemu kubwa ya watu wa maisha ya chini wanaendelea kumshukuru. Juhudi za dhati!

MM

Kama angemaliza miaka mengine mitano, ingetoa sura kamili ya mabadiliko kutokana na juhudi na sera za kuyapambania maisha ya wanyonge.

Au pangehitajika mwongo mwingine wa mtawala mwingine hadi kuonekane mabadiliko ya kweli katika maisha ya masikini wa Watanzania.

Magufuli amefariki na kila kundi lina hadithi yake kuhusu utawala wake. Waandishi wa habari watakupa yao ya moyoni. Wanasiasa wa upinzani watakupa orodha ya matatizo kwa upande wao.

Hata walalahoi, wanyonge na wafanyabiashara watakaokupa hadithi chanya na hasi kwa namna wimbi la utawala huo lilivyowapiga. Kwa ufupi kayagusa maisha ya wanyonge, kwa heri au kwa shari.