Waridi wa BBC: Mume wangu ana umri mkubwa ndio, lakini mbona liwe tatizo?

Ciru Njuguna na akiwa na mume wake Greg Twin

Chanzo cha picha, Ciru Njuguna

Maelezo ya picha, Ciru Njuguna na akiwa na mume wake Greg Twin
    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Unapokutana na Ciru Njuguna na Greg Twin mara ya kwanza, si rahisi kufikiria kwamba wanaweza kuwa wameoana na wanaishi kama mume na mke.

Wawili hao wameachana umri kwa zaidi ya miaka 30.

Mumewe Twin asili yake ni Ujerumani na ukizingatia kwamba ana miaka 61, amewazidi umri wazazi wote wawili wa Ciru.

Lakini unapotangamana wanandoa hao wawili zaidi ndipo unapogundua kwamba wana uhusiano wa karibu sana na wamependana kwa kweli.

Ni tofauti hii ya muonekano wao ambayo imekuwa gumzo na Ciru Njuguna anasema amekuwa akishutumiwa sana.

Lakini kwake anasema haoni tatizo.

Anasema umri hauna maana yoyote katika ndoa bali ni watu wawili kusikilizana na kuheshimiana.

Ciru Njuguna

Chanzo cha picha, Ciru Njuguna

Maelezo ya picha, Ciru Njuguna na mumewe walikutana kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook

Kukutana kwa njia isiyo ya kawaida

Ciru Njuguna na Greg Twin wamekuwa kwenye uhusiano na baadaye kwenye ndoa tangu mwaka wa 2012 walipokutana.

Wawili hao walikutana katika mtandao wa Facebook.

Ciru anasema miezi kadhaa kabla ya kukutana na Greg, alikuwa ameumizwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na kwa hivyo moyo wake ulikuwa bado na machungu.

Walipokutana, haja yake ilikuwa ni kukutana na marafiki wa kutoka mtandaoni.

Alikuwa na msisimko wa kukutana na mtu wa asili ya rangi nyeupe lakini pia alitamani kujua zaidi kuhusu nchi yake ya Ujerumani alikozaliwa na kadhalika.

Ciru alikutana na mumewe Greg Twin akiwa na umri wa miaka 20

Chanzo cha picha, Ciru Njuguna

Maelezo ya picha, Ciru alikutana na mumewe Greg Twin akiwa na umri wa miaka 20

Baada yao kuwa na mazungumzo ya kina kirefu katika mitandao ya kijamii hatimaye Greg alimwalika Ciru kukutana kwa kile alichokitaja kama 'kikombe cha kahawa'. Ciru aliupokea mwaliko huo.

"Nilikuwa na miaka 20 tulipokutana, upande wangu sikuwa nimewahi kuzungumza na mwanamume aliyekuwa na umri uliokuwa mkubwa mno, kando na watu wa jamii yangu," anasema.

"Hata hivyo, hilo halikuwa tatizo kwani nilimtazama kama mwanamume wa kawaida nilipomuona kwa mara ya kwanza."

"Nilipokwenda kukutana naye wakati huo pia sikuwa na malengo ya kutafuta mpenzi wala mume tulikutana tu kama marafiki,"anasema Ciru.

Ciru anasema kuwa alikuwa anasubiri kuingia chuo kikuu baada ya kukamilisha masomo shule ya upili wakati walipokutana.

Greg naye alikuwa anatafuta tu rafiki wa kukutana naye kwenye ukurasa wa Facebook.

"Ila kinachoumiza zaidi ni kuwa watu wengi hujiuliza ni vipi msichana wa miaka 19 alikubali kukutana na mwanamume wa miaka zaidi ya 50 atakuwa anatafuta nini ila kama yeye sio kahaba?" anasema.

"Kuwajibu ni kuwa kati yangu na Greg hakuna aliyekuwa na mpango wa ndoa wala mapenzi ila urafiki na pia kulikuwa na mengi ya kuzungumza katika mkutano wetu wa kwanza, kwa mfano kazi yake, kunihusu mimi na maisha yangu na kadhalika."

Ujauzito wa ghafla

Ciru anasema baada ya muda si mrefu baada yao kuanza urafiki, aligundua alikuwa mjamzito.

Ciru anasema kuwa alikuwa bado mdogo wa umri kuelewa masuala kuhusiana na mimba na malezi ya watoto.

Ciru na mumewe

Chanzo cha picha, Ciru

Maelezo ya picha, Wakati Ciru alipopata ujauzito ulikuwa msimu wake wa tafakari na wasiwasi mkuu maisha yake

Vile vile Ciru anasema kuwa kwa kipindi hicho alikuwa amekwaruzana na wazazi wake pia katika mambo mengine.

Kwa hivyo ulikuwa msimu wa tafakari na wasiwasi mkuu maishani.

"Kabla ya kukutana na Greg na pia kupata ujauzito nilikuwa nimewakosesha usingizi wazazi wangu , waliponituma shule nchini Uganda kwa masomo ya juu," anakumbuka.

"Nikiwa huko niliacha shule ghafla na kuanza maisha mengine kinyume na matarajio ya wazazi. Kwa hivyo nilifahamu kuwa huu haukuwa muda wa wazazi wangu kujua kuwa nilikuwa nimebeba ujauzito.

"Niliamua kuwa nisingetoboa siri ya ujauzito wangu. Mtu niliyemweleza alikuwa ni Greg pekee yake na kwa bahati nzuri alikubali kuwajibikia mimba na mtoto akizaliwa," anakumbuka Ciru.

Ciru Njuguna na akiwa na mume wake Greg Twin

Chanzo cha picha, Ciru Njuguna

Cha mno ni kuwa licha ya Greg kukubali kuwajibikia mimba, walikosana baada ya muda na wakawa hawako pamoja tena kama wapenzi.

Greg pia alikuwa anarejea kwao Ujerumani .

"Tulikosana nikiwa na mimba, na ikawa pia hatukuwasilina tena wakati huo, kumaanisha kuwa msimu wa ujauzito wangu nilikuwa pekee yangu. Ulikuwa wakati wenye changamoto nyingi hasa kwa kuwa pia mama aligundua kuwa nilikuwa na ujauzito," Ciru anasema.

Ciru alijaribu kila awezalo kukaa mbali na wazazi wake kwa lengo la kuficha ujauzito, na hata kutoroka nyumbani kwao hadi alipojifungua wanawe wawili wa kiume.

Uhusiano wake na mumewe haukuimarika mara moja licha ya kuwa baba ya watoto alipotumiwa picha za pacha wake akiwa nchini Ujerumani alionekana kusisimka mno.

Kipindi cha miaka mitatu, Ciru na Greg hawakuwa pamoja na alichukua malezi ya watoto wao kama mama mlezi pekee yake.

Unaweza pia kusoma:

Mwaka wa 2016 Greg alirejea tena nchini Kenya na walianza kuishi pamoja ila kukaa kwao kulikuwa kwa muda kwani mwaka wa 2017 walitengana ghafla na mumewe akarejea tena nchini Ujerumani.

Ciru anaeleza kuwa alikuwa na machungu mengi ya kubeba mimba pekee yake na kuanza malezi kwa miaka mitatu bila baba yao.

Hilo liliathiri uhusiano wao walipoanza kuishi pamoja tena.

"Nilihisi machungu ya kuachwa na ujauzito, na kwa hivyo baada ya muda tulitengana ghafla," Ciru anasema.

Kurudiana kwao na kuanza ndoa thabiti kulifanyika baada ya Ciru kuchumbiwa mara kama tatu hivi na kutengana kwa sababu mmoja au nyengine.

Mume kuuza mali

Hatimaye Februari 2020 Greg aliamua kuuza mali yake yote aliokuwa nayo nchini kwao ujerumani, na kuhamia Kenya kwa ajili ya kuhakikisha kuwa ndoa yao ingefaulu.

Ciru na Greg

Chanzo cha picha, Ciru

Maelezo ya picha, Ciru anasema kuwa Greg alihakikisha ametimiza tamaduni zote za ndoa kabla hawajaanza ndoa rasmi.

Ciru anasema kuwa Greg alihakikisha ametimiza tamaduni zote za ndoa kabla hawajaanza ndoa rasmi.

Ciru anasema kuwa hakupata fursa ya kukutana na wazazi wa mumewe kwa kuwa wote ni marehemu, ila ameweza kuwasiliana na jamaa wengine wa mumewe, kwa mfano kakake.

Ni kwanini Ciku alimpenda mume wake licha ya umri mkubwa?

"Greg kwa kweli ni mwanamume na nusu. Yeye ana roho safi. Kando na hayo ni mwanamume ambaye anawajali sana watu na anawajibikia majukumu ya watu ambao wako karibu naye, kwa hivyo mambo kama hayo na mengine yalinisukuma kumpenda hata zaidi," Ciru anasema.

Mwanadada huyu humsifia sana mumewe akianza kwa muonekano wake yeye anasema haoni uzee ila anaona mwanamume aliye na sura ya kuvutia.

Pia anasema mumewe ni mcheshi wa maneno na haishi kucheka kila wakati anapokuwa karibu naye.

Kwa hio ilikuwa rahisi sana kuvutiwa na yeye na kumpenda.

Kero kutoka kwa watu

Lakini kinachoudhi mno ni watu wanaokosoa ndoa yao.

"Kinachonishangaza ni baadhi ya maoni yanayotolewa kuhusu mume wangu, wamemuita babu yangu na kadhalika - lakini ninachokijua ni kuwa hakuna sheria inayosema kuwa huwezi kuwa na uhusiano na mwanamume mwenye umri uliosonga au umri mdogo. Mimi nampenda mume wangu mno na haijalishi watu watasema nini kutuhusu," Ciru anasema

Ciru na mumewe

Chanzo cha picha, Ciru na Greg

Maelezo ya picha, Ciru na Greg waliamua kuzungumzia mtandaoni uhusiano wao ulivyo na masuala mengine yaliyoibuka

Kutokana na uhusiano wao, Ciru na Greg waliona pengo la kujaza katika mtandao wa kijamii.

Waliamua kuzungumzia mtandaoni uhusiano wao ulivyo na masuala ibuka.

Kwa mfano, huwa wanajibu maswali kuhusu changamoto za kuishi na mume au mke aliye na umri tofauti na wako na pia kutoa ushauri.

Vile vile, hujadili hali ya kuishi na mtu ambaye sio wa kutoka kabila au asili yako katika kusaidia jamii kuelewa kuwa mahusiano yanazidi muonekano au hali ya mtu.

Mume wangu anaitwa majina kama vile babu au baba. Wengine hudai eti nina lengo la kumuangamiza - wengine pia wanasema kuwa yeye ni mkoloni na mimi ni mtumwa wake.

"Kitu kinachokera zaidi katika maongezi ambayo nimesikia watu wakisema kuhusu ndoa yangu na mume wangu ni kuwa mimi ni mtumwa wa kingono kwa kaburu. Hili ni mmojawapo wa mambo ambayo yimeuchoma moyo wangu mno ila sitakata tamaa kumpenda mume na watoto wangu."