Wanamgambo wa Al-Shabab wavamia hoteli Mogadishu, Somalia

A general view at the scene of a bomb explosion at the Afrik Hotel in Mogadishu, Somalia, with crowds seen in the street

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wanamgambo wa Al-Shabab hutekeleza mashambulizi mara kwa mara
Iliyochapishwa

Wanamgambo wa Al-Shabab nchini Somalia wamehusika katika makabiliano ya polisi na vikosi vya usalama katika hoteli moja iliyopo mji mkuu wa Mogadishu.

Kundi la Al-Shabab limekiri kutekeleza shambulizi hilo katika hoteli ya Afrik ambalo lilianza na bomu lililokuwa limetegwa kweye gari Jumapili mchana.

Kundi hilo ambalo linahusishwa na kundi la wanamgambo la Al-Qaeda, mara nyingi hutekeleza mashambulizi dhidi ya serikali.

Inasemekana kuwa gari moja liligonga eneo la mbele la hoteli hiyo na kulipuka kabla ya mshambuliaji aliyekuwa amejihami kwa silaha kuvamia jengo la hoteli, kulingana na maafisa na wengine walioshuhudia shambulizi hilo.

"Mlipuko huo ulifanya hoteli hiyo ikaanza kutetemeka wakati tukiwa ndani tunaendelea na mzungumzo. tulishutuka, tusijue la kufanya," aliyeshuhudia Ahmed Nur amenukuliwa na shirika la habari la Reuters.

"Sasa operesheni imekamilika. Watu 9, wakiwemo wavamizi wanne, wamefariki dunia na raia 10 wakajeruhiwa. Hakuna umeme," msemaji wa polisi amezungumza na wanahabari kutoka eneo la tukio kupitia mtandao wako wa Facebook.

Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble amesema katika taarifa kuwa miongoni mwa waliouawa ni aliyekuwa jenerali wa jeshi, Mohamed Nur Galal.

Kifo hicho pia kimethibitishwa na Rais Mohamed Farmaajo.

"Nimemuomba Mwenyezi Mungu ahurumie raia wa Somali waliopoteza maisha yao katika shambulio hilo baya na ninatoa risala za rambirambi kwa kifo cha jenerali Mohamed Nur Galal, aliyekuwa mwanajeshi wa Somali," alisema.

Ambulances are seen near the scene of a car bomb explosion

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Magari ya kubeba wagonjwa yameonekana yakiwa karibu na eneo lililoshambuliwa kwa bomu.

Wanamgambo hao waliilenga Hotel Afrik licha ya kwamba ipo kwenye eneo lililo chini ya ulinzi mkali na ipo karibu na uwanja mkubwa wa ndege mjini humo, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC aliyeko Mogadishu, Bella Hassan.

Hoteli hiyo ni maarufu sana nchini humo na mikutano mingi ya maafisa wa serikali ya Somali hufanyika hapo.

Msimamizi wa polisi wa eneo hilo amesema wabunge kadhaa na maafisa waandamizi wa jeshi walikuwa ndani ya hoteli hiyo wakati shambulio hilo linatokea.

Video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilionesha moshi mkubwa ukifuka katika eneo hilo mapema Jumapili.

Shambulio hilo linatokea ikiwa ni wiki kadhaa tu baada ya aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump kuagiza kuondoka kwa wanajeshi 700 ambao wamekuwa wakiunga mkono vikosi vya usalama vya eneo hilo dhidi ya makundi ya wanamgambo wakiwemo wanamgambo wa Al-Shabab.

Kuna hofu kuwa kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani huenda kukaongeza ukosefu wa udhibiti wa matukio kama hayo katika taifa ambalo litafanya uchaguzi mwezi ujao.