Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uvamizi wa jumba la Capitol: Afisa wa polisi Eugene Goodman asifiwa kuwa 'shujaa'
Afisa wa polisi wa bunge la Marekani ametajwa kuwa shujaa kwa kufanikiwa kuwazuia waandamanaji kuingia ukumbi wa bunge la Seneti kama wakati wa maandamano makali.
Kanda ya video inayomuonesha afisa huyo, aliyetambuliwa kama Eugene Goodman, akiwa hatua kadhaa kutoka kwa waandamanaji waliokuwa wakimfukuza apande juu ya ngazi.
Bw. Goodman kisha anaonekana akielekea upande wa lango la Seneti kabla ya kuwaelekeza wanaume hao upande mwingine.
Watu watano, akiwemo afisa wa polisi walifariki kutokana na maandamano hayo.
Afisa mwingine ambaye alikuwa zamu wakati wa uvamizi huo alijitoa uhai wikendi hii, familia yake ilisema.
Ukakamavu wa Bw. Goodman, unayesadikiwa kuwa mwanajeshi mkongwe aliyehudumu nchini, unajiri huku kukiwa na ukosoaji wa maafisa wa polisi kwa kushindwa kudhibiti usalama wakati waandamanji walipovamia jumba la bunge la Capitol Hill .
Usiku wa Jumatatu, idara hiyo ilisema maafisa wake wawili wamesimamishwa kazi na wengine kadhaa wanachunguzwa kwa kushukiwa kujihusisha na waandamanaji hao.
Kirk Burkhalter, Profesa wa chuo cha sheria cha New York na mkongwe aliyehudumu katika kitengo cha polisi cha New York kwa miaka 20 amesifu jinsi Bw. Goodman alivyoshughulikia maandamano hayo kwa "ustadi".
"Sidhani kuna mafunzo ya aina yoyote ya kukuandaa kwa hali kama hiyo," Bw. Burkhalter alisema.
Katika video hiyo iliyonaswa na mwandishi wa Huffington Post Igor Bobic, Bw. Goodman, ambaye ni mweusi, alikumbana na wafuasi wa Trump - ambao wote ni wanaume wazungu.
Mwanamume aliyekuwa akiongoza waandamanaji hao, akiwa amevalia fulana ya QAnon, ametambuliwa kama Doug Jensen kutoka Iowa.
Alikamatwa baadaye na maafisa wa polisi na FBI kutokana na jukumu lake katika maandamano hayo.
Kanda hiyo ya video inamuonesha Bw. Jensen akiongoza kundi la watu lililomfukuza Bw. Goodman - hatua chache kabla ya kuingia lango la ukumbi wa Seneti.
Alipokuwa akiendelea kumfukuza, Bw. Goodman alipiga mayowe katika radio yake akisema "ghorofa ya pili!", hatua inayoonekana aliyotumia kujielekezea mwenyewe waandamanaji hao ili wasiingie kuingia bungeni ambako watu walikuwa wamejificha.
Picha ya Bw. Goodman akifukuzwa na kundi la waandamanaji - baadhi yao wakiwa wamebeba bendera za majimbo yao, wengine wakiwa nabendra zinazofanana na zile za Wanazi - ilikuwa inasumbua sana, Bw. Burkhalter alisema.
"Iwe ni afisa wa polisi au la, kumuona mwanamume mweusi akifukuzwa na mtu aliyebeba bendera ya jimbo - picha hiyo ni mbaya sana. Kitu kama hicho hakifai kutokea tena," alisema.
"Inaashiria kila kitu tunachostahili kurekebisha."
Afisa Goodman amepongezwa na wabunge kadhaa wa Congress, huku baadhi yao wakitoa wito kwa afisa huyo kutuzwa medali ya heshima ya bunge kwa utendaji kazi bora.
"Wakati wafuasi wa Trump walipokuwa wakipekua bunge la Marekani, afisa huyo wa usalama wa Marekani aliwazuia waandamanaji hao kutoingia ukumbi wa Seneti na kuokoa maisha ya waliyokuwa ndani," aliandika mbunge wa bunge la wawakilishi Bill Pascrell katika mtandao wake wa Twitter.
"Jumatano iliyopita, nilikuwa ndani ya bunge la Seneti wakati afisa Eugene Goodman alipowaelekeza upande mwingine waandamanaji waliokuwa na hasira katika mazingira hatari kwake binafsi.
Uamuzi wake wa kuchukua hatua ya haraka siku hiyo iliokoa maisha, na tunamshukuru sana," aliandika Seneta Bob Casey siku ya Jumatatu.
Makabiliano kati ya Bw. Goodman na kundi la waandamanaji yalijiri dakika kadhaa kabla ya mamlaka ilipofanikiwa kufunga eneo la bunge, kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Washington Post.
Maafisa 2,000 - wa kitengo cha polisi wa bunge wana jukumu la kulinda jengo la Capitol na waliomo ndani yake.
Ni tofauti na polisi wa Washington DC, ambao wanashika doria katika mji mzima.
Tunafahamu nini kuhusu usimamizi wa polisi wa bungekufikia sasa?
Mkuu wa polisi wa Bunge la Marekani, Steven Sund, alijiuzulu wiki iliopita baada ya kikosi chake kukosolewa kutokana na jinsi kilivyoshughulikia maandamano hayo, ikiwa ni pamoja na wito uliotolewa hadharani na kiongozi wa ngazi ya juu wa chama cha Democratic Nancy Pelosi kumshinikiza Bw. Sund kujiuzulu.
Kaimu mwanasheria mkuu wa Marekani Michael Sherwin amesema idara ya haki inatafakari kuwafungulia mashtaka ya uhalifu maafisa wa polisi wa bunge walioonekana kushirikiana na waandamanaji.
Familia ya afisa Howard Liebengood, 51, aliyekuwa zamu wakati wa maandamano hayo, imesema alifariki siku ya Jumamosi.
Wakili wa familia ya Bw. Liebengood imetaja kifo cha afisa huyo aliyehudumu katika kitengo cha polisi wa bunge kwa miaka 15 kuwa "hasara kubwa".
Katika mtandao wa Twitter, Seneta wa Republican Mitt Romney alisema timu yake "imevunjwa moyo" na kifo cha Bw. Liebengood. "nilimjua Howie kama mtu mwenye furaha, alikuwa rafiki kwangu na kwa wafanyakazi wangu," Bw. Romney aliandika. "Ujasiri wake, na kuwajali wengine kwa dhati utakumbukwa na wengi wetu tuliopata nafasi ya kutangamana naye."
Kulingana na kituo cha CBS News, kinachoshirikiana na BBC nchini Marekani, kikosi cha polisi cha bunge la Capitol kinakabiliwa na matukio kadhaa ya maafisa wake kutishia kujidhuru baada ya shambulio la wiki iliopita dhidi ya bunge.
Bw. Burkhalter amesema jukumu la kuzembea kwa kuvunjika kwa usalama liko mikononi mwa uongozi wa idara hiyo.
Ikifikia wakati ambapo afisa mmoja kama Goodman, analazimika kufanya uamuzi wa kutafuta usaidizi, tumeshindwa vita hivyo, alisema.
"Hatukustahili kufikia kiwango hicho," aliongeza kusema.