Uchaguzi wa seneti Georgia: Iwapo Raphael Warnock atashinda atakuwa seneta wa kwanza mweusi kushinda jimbo la Georgia

Iwpo atathibitishwa Bwana Warnock seneta wa kwanza mweusi katika jimbo la Georgia

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Iwpo atathibitishwa Bwana Warnock seneta wa kwanza mweusi katika jimbo la Georgia
Iliyochapishwa

Mgombea wa chama cha Democratic Raphael Warnock anatarajiwa kuchukua ushindi wa moja ya nafasi za useneti huko Georgia, na kumuondoa seneta anayegombea kurejea tena wa Republican Kelly Loeffler.

Huku asilimia 98 ya kura zikiwa zimeshahesabiwa, Shirika la Marekani la TV networks na lile la habari la Associated Press limetangaza kuwa Bwana Warnock anaelekea kupata ushindi.

Kuchukua udhibiti wa bunge la Seneti katika kipindi cha miaka miwili ya kwanza kwa rais mteule wa chama cha Democratic Joe Biden kunategemea matokeo hayo ya duru ya pili ya uchaguzi.

Matokeo hayo ni pigo kubwa kwa rais anayeondoka Donald Trump.

Uchaguzi huo unarudiwa kwasababu hakuna hata mmoja kati ya wagombea kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba aliyepata idadi ya kura zinazohitajika kutangazwa mshindi. Kulingana na sheria za jimbo hilo ni lazima mgombea kupata angalau asilimia 50 ya kura zilizopigwa.

Ikiwa atathibitishwa kuwa mshindi, Bwana Warnock atakuwa seneta wa kwanza mweusi katika jimbo la Georgia - jimbo lililokuwa la watumwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani - na seneta wa 11 mweusi katika historia ya Marekani.

Akidai kuwa ameshinda, Bwana Warnock alitoa heshima kwa maa yake Verlene, ambaye akiwa kijana alikuwa mfanyakazi wa shambani.

"Siku ile - kwasababu hii ni Marekani - mama mwenye umri wa miaka 82 ambaye alikuwa akichuna pamba, alikwenda kupiga kura na kumchagua kijana wake mdogo kama seneta wa Marekani," alisema.

Ingawa Bwana Biden wa Democrat angependa kuchukua viti vyote vya seneti ili apate udhibiti wa bunge hilo, chama cha Republican cha rais anayeondoka madarakani Donald Trump anahitaji kushinda kiti angalau kimoja ili aendeleze udhibiti wa bunge la seneti.

Kura za maoni zinaonesha nini?

Raphael Warnock, Democratic Senator-elect for Georgia

Chanzo cha picha, Reuters

Madai ya Bwana Trump ya wizi wa kura huenda yameondoa imani ya wapiga kura kwenye mfumo wa upigaji kura, kulingana na kura za maoni za Taasisi ya Edison.

Utafiti wa taasisi hiyo kwa wapiga kura waliokuwa wanaondoka kwenye vituo vya kupiga kura umebaini kuwa asilimia 70 walikuwa na uhakika kwa kiasi fulani kuwa kura zao zitahesabiwa sahihi, asilimia hiyo ikiwa imepungua kwa asilimia 15 tangu uchaguzi wa Novemba.

Aidha, kura za maoni zinaonesha wakaazi wa Georgia wamegawanyika kwa misingi ya chama wanachotaka kidhibiti bunge la seneti: asilimia 49 walipendelea chama cha Republican huku asilimia 48 wakipendelea chama cha Democratic.

Kwa misingi ya watu ikilinganishwa na Novemba watu weusi ambao walikuwa asilimia 29 walipendelea mgombea wa chama cha Democratic.

Huku Republicans, wakipata wingi kwa uungwaji mkono na wazungu.

Kinyang'anyiro hicho kitaamua nani atakuwa na udhibiti wa bunge la Seneti

Awali kituo cha habari cha CBS News mshirika wa BBC kimesema vyama vyote viwili vinakaribiana mno.

Matokeo yanatarajiwa kuanza kutangazwa saa kadhaa tokea sasa lakini ikiwa matokeo yataendelea kuonesha ukaribu wa namna hiyo huenda matokeo ya mwisho yakachukua muda kutangazwa.

Rais mteuliwa Joe Biden wa chama cha Democrats anahitaji kushinda uchaguzi huu ili aweze kupata udhibiti wa mabunge yote mawili.

Wakati huohuo, rais wa chama cha Republican anayeondoka madarakani Donald Trump anahitaji kushinda kiti kimoja tu ili adhibiti bunge hilo la Seneti.

Wabunge wa Republican Kelly Loeffler na David Perdue sasa hivi ndio wanaoshikilia viti hivyo viwili. Bi. Loeffler anakabiliana na Reverend Raphael Warnock huku Bwana Perdue akipambana na aliyekuwa mwanahabari Jon Ossoff.

Hakuna kati ya wagombea hao ambaye alipata asilimia 50 ya kura zilizopigwa kama inavyohitajika kuibuka na ushindi wa moja kwa moja katika uchaguzi uliofanyika Novemba hatua iliyolazimisha kufanyika kwa duru ya pili kulingana na sheria za uchaguzi za jimbo la Georgia

Kipi kilicho hatarini Georgia?

Kura hiyo itaamua uwiano wa nguvu ya uongozi katika bunge la Seneti.

Sasa hivi chama cha Republican kinashikilia viti 52 kati ya 100. Na ikiwa Democrats watapata ushindi, bunge la Senati litakuwa limegawanyika nusu kwa nusu hatua itakayomuwezesha makamu rais wa chama cha Democratic Kamala Harris kufanya maamuzi ya upigaji wa kura.

Hili litakuwa muhimu katika upitishaji wa ajenda za Joe Biden bungeni ikiwemo masuala ya msingi kama vile afya na udhibiti wa mazingira - sera ambazo zinapingwa vikali na Republicans.

Bunge la Seneti pia lina nguvu ya kuidhinisha au kukataa baraza la mawaziri lililochaguliwa na Bwana Biden pamoja na nyadhifa za majaji.

Ikiwa Bwana Ossoff na Warnock watashinda, Ikulu ya Marekani, bunge la Seneti na bunge la Wawakilishi yote yatakuwa chini ya udhibiti wa chama cha Democratic kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kwa rais Barack Obama mwaka 2008.

Shughuli ya upigaji kura ikoje?

Hesabu ya kura

Upigaji kura ulikamilika saa moja usiku saa za eneo ingawa wale wote waliokuwa wamepanga foleni kupiga kura nje ya vituo vya kupiga kura wakati huo wameruhusiwa kupiga kura.

Wahudumu katika uchaguzi huo wa Georgia jimbo lenye kaunti 159 wanaendelea kuhesabu kura ikiwa ni pamoja na zile zilizopigwa mapema na kura zilizopigwa kwa njia ya posta.

Kulingana na shirika la habari la CBS News, idadi ya kura zote zilizopigwa zinakadiriwa kuwa zaidi ya milioni nne.

Zaidi ya kura milioni tatu - ikiwa ni takriban asilimia 40 ya wapiga kura waliosajiliwa - zilikuwa zimepigwa kabla ya Jumanne.

Upigaji kura wa mapema ulikuwa ndio msingi na muhimu mno kwa Bwana Biden katika kupata ushindi wa urais.

Aidha wapangaji mikakati wa chama cha Republican wamesema wana matumaini ya kuibuka na ushindi ikiwa zaidi ya wapiga kura milioni moja watajitokeza siku ya kupiga kura.

Asilimia 80 ya kura zilizopigwa zinatarajiwa kuhesabiwa kufikia saa sita usiku saa za eneo lakini bado haiko wazi ikiwa maafisa husika wataendelea na shughuli zao usiku kucha.

rais Trump aliwasihi wafuasi wa Democrats kujitokeza na kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo

David Perdue amekuwa akijitenga tangu alipotangamana na mtu aliyesemekana kuwa virusi vya corona huku mgombea mwenzake wa Republican Bi. Loeffler akiweka picha zake na wafuasi wake mtandaoni kuonesha wanapiga kura.

Wagombea wote wa Democratic wanatarajia kuvutia wafuasi wao katika maeneo ya mijini hasa viungani mwa Atlanta.

Bwana Perdue karibu ashinde katika duru ya kwanza dhidi ya Ossoff katika uchaguzi uliofanyika Novemba kwa kupata asilimia 49.7 ya kura zilizopigwa.

Nafasi nyingine ilikuwa na wagombea wengi huku wa Democrat Bwana Warnock akipata asilimia 32.9 ya kura zilizopigwa dhidi ya mpinzani wake Loeffler aliyepata asilimia 25.9.

Chama cha Democrat kimeshinda kiti cha useneta jimbo la Georgia miaka 20 iliyopita lakini katika uchaguzi huo chama hicho huenda kikapata nguvu kutokana na ushindi wa Bwana Biden dhidi ya Trump.

Kipi kinachotarajiwa?

Jumatano, matukio mengi ya kisiasa yanatarajiwa katika mji wa Washington DC, wakati ambapo wabunge watakusanyika kwa kikao maalum kuidhinisha matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba.

Katika mchakato wa kawaida kabisa wa kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden, wabunge kadhaa wa Republican wameapa kupinga matokeo.

Kundi la wabunge hao likiongozwa na Seneta Ted Cruz na Bi. Loeffler, linataka mchakato huo kucheleweshwa kwa siku 10 ili kuchunguza madai ya wizi wa kura yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo.

Hata hivyo, hatua hiyo inatarajiwa kupingwa kwasababu inasemekana idadi kubwa ya maseneta itakubali kuidhinisha matokeo hayo ambayo tayari yamepitishwa na majimbo ya Marekani.

Aidha Bwana Biden wa chama cha Democrat, anatarajiwa kuapishwa rasmi kama rais wa Marekani Januari 20.

Rais Trump kwa upande wake amekataa kukubali kuwa alishindwa na Biden aliyepata kura 306 dhidi ya 232 za Trump kwenye kura za wajumbe zinazotumika kuamua nani anakuwa rais wa Marekani.

Bwana Biden alishinda zaidi ya kura milioni saba dhidi ya rais wa sasa.