Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Kura zaendelea kuhesabiwa

Kidole cha mpiga kura kikipakwa wino
Iliyochapishwa

Vituo vya kupiga kura hatimaye vimefungwa, baada ya shughuli ya kupiga kura kukamilika.

Hii leo Jumatano ya Tarehe 28 Oktoba, mamilioni ya Watanzania wamepiga kura kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo. Huu ni uchaguzi wa sita toka nchi hiyo iliporejea kwenye siasa ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Tanzania kuna serikali mbili ya Muungano na ya Zanzibar, na hivyo mamlaka za uchaguzi pia zimechukua sura hiyo. Hii leo umefanyia uchaguzi wa Muungano ambao unahusisha Watanzania Bara na Zanzibar na unasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Pia uchaguzi wa Zanzibar unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Katika uchaguzi wa Muungano wapiga kura wamechagua nafasi tatu, Rais, Mbunge na Diwani na kwa upande wa Zanzibar kura mbili zimeongezeka, Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Wagombeaji urais Tanzania

  • Anawania awamu ya pili na ya mwisho madarakani.
  • Kampeni yake imejikita kati mafanikio yake kwenye sekta za madini, ujenzi wa miundombinu, elimu bure na mapambano dhidi ya rushwa.
  • Awamu yake ya kwanza pia imekosolewa kwa ukandamizaji wa haki za binadamu.
  • Ni mgombea wa chama tawala ambacho kipo madarakani toka uhuru, hivyo anatarajiwa kushinda uchaguzi huu.
  • Magufuli, 60, alichaguliwa Bungeni mara ya kwanza 1995 na kupata umaarufu akihudumu katika wizara ya ujenzi alipopata jina la utani la tingatinga.
  • Alimiminiwa risasi na wasiojulikana Setemba 2017, japo amenusurika shambulio hilo limemuacha na majeraha ya kudumu.
  • Alirejea Tanzania mwezi Julai 2020 baada ya miaka mitatu ya ughaibuni ili kugombea urais kupitia chama kikuu cha upinzani Chadema.
  • Kampeni yake imejikita kwenye kuheshimu haki za binadamu na kukuza uchumi wa watu.
  • Mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010 na 2015 na kuhudumu kama mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani.
  • Alituhumiwa ndani ya CCM kuwa alikuwa na mipango ya ‘kumhujumu’ Magufuli kwenye uchaguzi wa ndani ya chama 2020.
  • Sasa ni mgombea wa ACT, ambacho kimeweza kukua kutoka kuwa chama kidogo mpaka moja ya mihimili ya upinzani kwa kipindi kifupi.
  • Kachero mstaafu, alihudumu kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya rais mstaafu Jakaya Kikwete toka 2007 mpaka 2015.
  • Mwanasiasa mwandamizi wa upinzani ambaye amegombea urais katika chaguzi zote kasoro mwaka 2015.
  • Alikuwa kinara wa upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 na 2005.
  • Ushawishi wake ndani ya upinzani umepungua baada ya migogoro ya ndani ya CUF iliyolazimisha kundi hasimu kwake kujitoa chamani.
  • Profesa Lipumba ni moja ya wasomi maarufu wa uchumi nchini Tanzania ambapo alisoma shahada zake za juu kutoka chuo kikuu maarufu cha Stanford, Marekani.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kuwa kwa uchaguzi huu, idadi ya waliojiandikisha baada ya maboresho ya daftari la wapiga kura ni 29,188, 347 na ambao walitarajiwa kupiga kura katika vituo 80,155.

Watanzania wakiwa katika mstari kupiga kura

Kama ilivyo kwa chaguzi zote duniani kuna mambo ya msingi ambayo hutoa taswira ya mchakato mzima utakavyokuwa, na kwa upande wa Tanzania kuna mambo matano ambayo ni ya muhimu kuyafahamu.

Swali sasa ni je, tutarajie nini hususankwa uchaguzi wa urais?

Kwa sasa tume ya uchaguzi imeanza mchakato wa kuhesabu kura, huku ikitarajiwa kumtangaza mshindi ndani ya wiki moja.

Mshindi atatangazwa iwapo atapata asilimia kubwa ya jumla ya kura zitakazopigwa.

Zoezi la kupiga kura lilianza saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi jioni

Je, kuna uwezekano wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani?

La! Katiba ya Tanzania hairuhusu mahakama kuhoji wala kupinga matokeo ya urais mara mshindi wa uchaguzi atakapokuwa ametangazwa na tume ya uchaguzi.

Hii ni tofauti na mataifa mengi barani Afrika ambapo mahakama ya juu inaweza kuamuru uchaguzi wa urais kurudiwa iwapo matokeo yatatiliwa shaka.

Ni sheria ambayo imekuwa ikipingwa kwa muda mrefu.

Tayari mahakama ya Afrika imeamuru Tanzania kuviruhusu vyama vya siasa kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani.

Msimamizi akikagua kitambulisho cha mpiga kura

Je, mshindi ataingia ofisini wakati upi?

Rais mteule atapaswa kuingia ofisini haraka iwezekanavyo punde tu anapotangazwa rasmi kuwa mshindi.

Lakini kwa vyovyote vile, atapaswa kuingia ofisini katika kipindi kisichozidi siku saba baada ya matokeo rasmi kutolewa.

Matukio yaliyojitokeza hii leo.

Mpigakura akihakiki jina lake

Yaliyojiri hii leo wakati wa zoezi la kupiga kura

Msemaji wa CHADEMA , Makene aliithibitishia BBC kuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kawe kupitia chama hicho Halima Mdee, alikamatwa na kushikiliwa kwa takribani saa moja kisha kuachiwa baada ya kutokea mzozo kuhusu makosa ya kuingilia zoezi la uchaguzi baada ya Halima kudai kuwepo kwa mabegi ya 'kura feki'.

Kupitia ukurasa wa Twitter , Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, amesema mwenyekiti wa jimbo la Kigoma mjini Bwana Suleiman Simba alikamatwa na polisi katika kituo cha kupigia kura cha stendi mpya kata ya Kasingirima alipokuwa 'akizuia kura zilizopigwa'kuingizwa kituoni hapo, halikadhalika Tanga.

Pia kuliibuka madai kuwa mawakala wa uchaguzi kukosa barua zinazowathibitisha kusimamia shughuli za kura kutoka tume ya taifa ya uchaguzi, madai ambayo yamepingwa na Mkurugenzi wa uchaguzi Tanzania bara Dkt Charles Wilson Mahera, alipozungumza na BBC.

Halikadhalika Mwenyekiti wa Tume, Jaji Semistocles Kaijage amezungumza na wanahabari akisema kuwa madai hayo hayajafikishwa rasmi NEC na kuwa hakuna taarifa kuwa ni vituo gani vinavyoelezwa kutendeka matukio hayo.

Tutakuwa tukiwapa taarifa kuhusu matokeo ya uchaguzi kadiri taarifa rasmi zitakavyokuwa zikitufikia.