Mapinduzi Mali: Wanajeshi walioongoza mapinduzi wasema hakuna makubaliano kuhusu serikali ya mpito

kanali meja Ismael Wague (katikati) msemaji wa kamati ya kitaifa ya kuwaokoa raia wa Mali (CNSP)

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Viongozi wa mapinduzi wanasema kwamba raia wa Mali wenyewe watafanya uamuzi wa mwisho
Iliyochapishwa

Mazungumzo nchini Mali yanayolenga kutatua mzozo wa kisiasa unaoendelea kufuatia mapinduzi yaliofanyika wiki iliopita yamemalizika bila makubaliano.

Viongozi wa mataifa ya magharibi mwa Afrika wamesema kwamba rais alieondolewa madarakani Ibrahim Boubacar Keita , anafaa kurudishwa madarakani.

Lakini wajumbe hao kutoka kwa shirika la Ecowas walishindwa kuwaelewesha viongozi hao wa jeshi kwamba huo ndio uliokuwa uamuzi mzuri.

Bwana Keita alikabiliwa na maandamano makubwa kabla ya mapinduzi yake na raia wengi nchini Mali wameunga mkono kuondolewa kwake.

Msemaji wa jeshi kanali Ismael Wague alinukuliwa na Reuters akisema kwamba baada ya mazungumzo kuisha uamuzi wa mwisho kuhusu serikali ya mpito utatolewa na raia wa Mali wenyewe.

Lakini wazo la bwana Keita kurudi madarakani huenda lilikataliwa na rais huyo mwenyewe, kulingana na chombo cha habari cha AFP.

Kilinukuu taarifa tofauti kutoka kwa pande hizo mbili zilizosema kwamba rais huyo amekuwa katika kizuizi tangu mapinduzi hayo Jumanne iliopita na kwamba hangetaka kurudi madarakani

Waandamanaji wakisherehekea mapinduzi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wengi walisherehekea mapinduzi hayo kama 'ushindi'

Kundi la wapatanishi linaloongozwa na aliyekuwa rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan - litaripoti kwa viongozi wa serikali za Afrika kuhusu hatua zilizopigwa kulingana na kanali Wague alienukuliwa akisema.

Mazungumzo hayo yalianza kwa maelezo machache siku ya Jumamosi na kuendelea siku ya Jumapili na Jumatatu. Mwisho wa kikao bwana Jonathan alisema: Tumeafikiana baadhi ya makubaliano lakini hatujapata mwafaka kuhusu masuala yote.

Wiki iliopita, maelfu ya raia waliandamana katika barabara za mji mkuu wa Bamako , ili kusherehekea mapinduzi hayo ambayo yalishutumiwa kote duniani.

Bwana Keita alishinda muhula wa pili katika uchaguzi wa 2018, lakini tangu mwezi Juni amekabiliwa na maandamano makubwa kuhusu ufisadi , usimamizi mbaya wa uchumi na mizozo ya uchaguzi wa bunge.

Kumekuwa na hasira miongoni mwa wanajeshi kuhusu mishahara yao na vita dhidi ya Wanajihad katika eneo la kaskazini la taifa hilo ambapo mamia ya wanajeshi wameuwawa katika kipindi cha mwaka mmoja.