Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Upimaji wa kinga ya mwili ni nini na una maana gani katika janga hili?
- Author, Rhoda Odhiambo
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Kinga ya mwili au antibodies ni aina ya protini ambayo mwili hutoa inapokabiliana na maambukizi.
Ili kujua kama mtu ana kinga ya mwili, madaktari hufanya kipimo hiki kuonesha kama mtu aliyepatikana na virusi hapo awali na baadae kupona amepata kinga dhidi yake.
Lakini katika janga hili la Covid -19, wataalam bado hawana uhakika wa muda wa kinga hiyo.
Na hii ndio kwa sababu wanataka kujua muda huo na pia kuweza kujua jinsi maambukizi ya corona yalivyosambaa barani Afrika na pia kote duniani.
Je upimaji huu ni sawa na ule wa Covid-19?
Mtu hupimwa corona anapoonyesha dalili zake; kama vile kukohoa, kuwa na joto la mwili la hali ya juu na dalili nyinginezo.
Lakini kuna wale pia ambao hawaonyeshi dalili hizi na watu hawa hupatakina na maambukizi haya wakati madaktari wanapofanya vipimo watu katika mkoa fulani kutokana na ongezeko la maambukizi katika eneo hilo.
Wakati madaktari wanapofanya vipimo vya kinga ya mwili, huwa wanachukua sampuli ya damu kutoka kwa mtu aliyekuwa ameambukizwa na Covid-19 hapo awali na kupona. Pia, wanachukua sampuli za damu kutoka kwa jamii ili kuelewa jinsi inavyoenea katika jamii.
Kwa nini ni muhimu barani Afrika?
Vipimo hivi sio muhimu hapa barani Afrika pekee bali kote duniani. Watalaam wa Afya wanapofanya vipimo wanataka kujua iwapo mtu anaweza kupata maambukizi ya Covid-19 tena na kutathmini kwa kina namna ugonjwa huu unavyosambaa katika jamii.
Mbali na hayo, pia itaweza kutoa jibu la jinsi ya kuwatibu wale ambao wako katika hali mahututi kutokana na ugonjwa huu wa corona.
Kwa sasa, hakuna tiba au chanjo ya corona lakini watalaam wa afya wanajaribu dawa ambazo hutumika katika magonjwa mengine kupunguza makali ya corona.
Wengine wanajaribu kutumia njia inayoitwa convalescent plasma. Hii inawahitaji madaktari kutumia plasma, kijenzi cha damu ambacho kina kina ya mwili kuweza kuwatibu wale ambao wameathirika. Majaribio yanafanyika katika mataifa ya Madagascar na
Afrika Kusini. Teknolojia hii sio kigeni. Iliweza kutumika katika janga la mafua ya nguruwe (swine flu) mwaka 2009. Watu wengi pia wanasema kuwa idadi ya maambukizi barani Afrika ni zaidi ya milioni kwa madai kuwa mataifa hapa hayafanyi vipimo vya kutosha.
Hii ni kutokana na ukosefu wa vifaa hivi. Lakini afisa mkuu wa shirika la Afya duniani WHO, bara Afrika, dokta Matshindisio Moeti anasema kuwa huenda viwango vya maambukizi ambavyo havijaripotiwa sio vingi sana kama inavyodaiwa.
Je tutarajie kwamba vipimo hivyo vitafanyika Afrika mashariki?
Kwa sasa ni mataifa saba pekee hapa Afrika ambayo yameanza kufanya vipimo hivi.
Mataifa haya yana uwakilishi wa kikanda na pia yana miradi ya kutosha. Mataifa mengine ambayo yaliweza kufanya vipimo hivi ni Kenya na Msumbiji.
Utafiti kutoka nchi hizi mbili ulionesha kuwa kuna watu waliokuwa wamepata maambkuzi ya corona, hawakuwa na dalili yeyote na wala hawakupokea matibabu hospitalini.
Wiki iliopita afisa mkuu wa Shirika la Africa CDC dokta John Nkegasong alisema kuwa watashirikiana na mataifa mengine kufanya vipimo hivi.