Virusi vya corona: Je ni mbinu gani itakayotumika kusambaza chanjo ya corona kwa watu bilioni 7 duniani?

Iliyochapishwa

Timu za utabibu kote duniani zinashughulikia suala la kupata chanjo ambayo itakuwa na ufanisi dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

Waziri wa Uingereza Boris Johnson, ametaja hilo kuwa juhudi za pamoja zenye "kuhitaji ushirikiano wa haraka zaidi ya kipindi chochote kile cha maisha yetu".

Lakini mbali na sayansi ya teknolojia ya juu kupata ushindi dhidi ya jinamizi hili, vipi kuhusu namna ya kuanza kutoa chanjo hiyo kwa watu bilioni saba kote duniani.?

Uingereza, juhudi hizo zinaelekezwa katika chuo cha Sayansi cha Harwell huko Oxfordshire.

Kitakuwa kituo cha utengenezaji chanjo na Uvumbuzi Uingereza (VMIC), mipango iliyotokana na ugonjwa wa Covid-19.

"Tumepunguza muda wa kupatikana kwa chanjo hiyo hadi nusu yake. Kwahiyo tulikuwa tumejiwekea malengo ya iwe tayari kufikia mwisho wa 2022, lakini sasa tuna matumaini kwamba itakuwa inapatikana mtandaoni mwaka 2021," ameelezea Matthew Duchars, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uingereza cha VMIC.

'Kama kuoka keki'

Bwana Duchars bado hajachukua likizo kwasababu anajua kwamba eneo hilo huenda likatengeneza chanjo ya chuo kikuu cha Oxford. Anawasiliana kila wakati na timu ya Taasisi ya Jenner mkabala na Oxford.

Anasema ni jukumu kubwa.

"Ni muhimu mno, sio tu kwa nchi hiyo lakini dunia nzima kwa ujumla, kuwa na uwezo wa kutengeneza chanjo za aina hiyo kwa haraka na ufanisi," amesema.

"Kwa kulinganisha - ni sawa na kuoka keki nyumbani. Unaweza kutumia muda wa saa kadhaa kuoka keki nzuri sana na sasa umefika wakati wa kuoka keki milioni 70 na zote ziwe nzuri, kwa hiyo ni changamoto kubwa."

Chuo kikuu cha OXford tayari kimelazimika kutafuta japo kwa muda, maabara yenye nafasi ya kutosha kuanza kutengeneza chanjo yake wakati huu, hata kabla ya kujua matokeo yake katika majaribio ya ngazi ya duniani.

Hatimae, dunia itahitajika kutengeneza mabilioni ya chanjo kdhaa za ugonjwa wa Covid-19.

Zote zitalazimika kutengenezwa, kugawanywa na kusambazwa kote duniani.

Shirika la kimataifa la chanjo Gavi limesema kuwa nchi zinastahili kuanza kufikiria kuhusu jinsi chanjo hiyo itakavyoanza kutolewa kwa raia wake.

Lakini sio rahisi kupata ushirikiano wa kimataifa kwasababu nchi nyingi tajiri tayari zinaingia kwenye makubaliano ya pande mbili na kampuni za dawa ili kuhakikisha kwamba watapata chanjo iwapo itapitakana.

Kukabiliana na maslahi binafsi

Seth Berkley, Mkurugenzi Mtendaji wa Gavi, anasema moja ya changamoto kubwa hivi sasa ni kile kinachofahamika kama "Chanjo kwa taifa".

"Nafikiri nchi zote zinastahili kufikiria hili kwa mtazamo wa kidunia kwasababu ndio jambo sahihi kufanya lakini pia kwasababu ni suala linalozingatia maslahi ya kibinafsi," amesema.

"Ikiwa katika nchi zilizo karibu kiwango cha virusi kinasambaa kwa haraka, huwezi kurejea katika biashara kama kawaida, au usafiri wa watu. Ni muhimu kuwa na mtazamo huo: hatuko salama labda kila mmoja awe salama."

Pamoja na kuhakikisha nchi zinazoendelea zinapata chanjo sahihi, Bwana Berkley analazimika kufikiria kwa mtazamo wa uhalisia zaidi wa jinsi chanjo itakavyosambazwa ikiwemo ikiwa ama kuna vichupa vya kutosha vya kuhifadhi chanjo kote duniani.

Kumekuwa na taarifa za changamoto katika utengenezaji wa vichupa vya kuhifadhi chanjo hiyo.

"Tuna wasiwasi kuhusu hilo," Bwana Berkley amekubali, "kwa hiyo tuliamua kununua vichupa vya kutosha kwa chanjo kiasi ya watu bilioni mbili, hiyo ndio idadi ya chanjo tunatarajia kuwa nayo kufikia mwisho wa 2021."

Na ikiwa vichupa vya kuwekea chanjo vitakuwa tatizo, hiyo inamaanisha tatizo pia litakuwa kwa jokofu la kuhifadhia kwasababu ni lazima chanjo kuhifadhiwa kwa mazingira ya baridi.

Kuhifadhi iwe baridi

Profesa Toby Peters, mtaalamu wa usafirishaji katika mazingira baridi kutoka chuo kikuu cha Birmingham anasaidia mashirika kama Gavi kufikiria jinsi wanawaza kutumia vizuri majokofu yaliyopo katika nchi zinazoendelea.

Anasema: "Sio tu jokofu la kuhifadhi chanjo, ni pamoja na vingine vyote vinavyohusiana: vifaa vya kubebea kwenye ndege; magari ya kuisambaza kwenye maduka ya eneo, pikipiki na watu wanaoichukua hadi kuifikisha kwa jamii. Haya yote yanatakiwa kuendelea bila matatizo yoyote."

Profesa Peters amekuwa akizungumza na makampuni ya chakula na viywaji duniani kufikiria kuomba bidhaa za kuhifadhi chakula kuwa baridi ili kusaidia katika mradi huo.

Ili chanjo iweze kupatikana bila changamoto yoyote, nchi zinastahili kuangalia vipaombele vyao kwa watakaopewa chanjo.

Nani wa kupewa kupaumbele?

Dkt Charlie Weller, Mkuu wa chanjo wa Shirika la Wellcome Trust Uingereza, amesema kuwa nchi zitahitajika kuuliza maswali ya wazi.

"Nani anahitaji chanjo hii? Kundi gani lipo katika hatari zaidi? Kina nani wa kupewa kipaumbele? Kwsababu tunachokifahamu ni chanjo yoyote itakayopatikana mara ya kwanza lazima uhitaji utakuwa wa juu, kwahiyo ni lazima watu kuchagua hatua za kufuata."

Hata kutoa chanjo hiyo kwa watu itakuwa changamoto.

Mfano, Uingereza, inaangalia jinsi inavyotumia mtandao wake wa vituo vya upigaji kura kama njia moja ya kuitoa kwa watu. Lakini kwa nchi maskini hali inatia mashaka zaidi.

Pia unaweza kutazama: