Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mlipuko Lebanon: Evelyn Wanjiru mkaazi wa Beirut raia wa Kenya aelezea jinsi mlipuko ulivyomkumba
Lebanon inaendelea kuomboleza baada ya mlipuko mkubwa katika mji mkuu wa Beirut ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 100 kufikia sasa.
Mji wote uliyumbishwa na mlipuko huo ulioanza kwa moto katika bandari.
Evelyn Wanjiru ni raia wa Kenya anayeishi na kufanya kazi mjini Beirut umbali wa dakika kumi kwa gari kutoka eneo kulipotokea mlipuko.
Wanjiru anasema alikuwa anatarajia kuhudhuria mkutano na alipofika nyumbani kutoka kazini akaanza kujitayarisha lakini ghafla akasikia nyumba inatetemeka na vitu vikaanza kudondoka.
''Nilipoanza kusikia mtetemeko nikatoka bafuni mbio na kwenda kuangalia rafiki zangu ninaokaa nao karibu. Lakini nusu ya safari nilisikia kitu kinanivuta kwa nyuma, nikagongwa mgongoni na kuanguka'', Wanjiru amesema.
Wanjiru anasema rafiki yake mmoja alimuona akiwa ameanguka akamsaidia kusimama na kukimbilia usalama wao.
Wasijue kwamba kule walikokuwa wanakimbilia ndiko kunakotoka mvutano na shinikizo la juu na wakati huohuo nyumba yao bado inaendelea kutetemeka kweli.
Wakajiona wamekutana wanne kila mmoja anakimbia na hajui anakoelekea.
''Tulikumbatiana na kupeana moyo tukaelekea upande wa pili kwenye kona fulani na tukasimama.'' Wanjiru ameelezea.
Kwasababu hawakuwa wanajua nini kinachoendelea, baada ya dakika mbili hivi nyumba ikaacha kutetemeka, wakakimbilia kwenye ushoroba wa juu na hapo ndipo walipoona moshi mkubwa ajabu hewani unafuka uliokuwa wa rangi nyekundu.
''Tukaanza kusikia sauti za magari ya kubeba wagonjwa na hapo ndipo tulipoamua kufungua televisheni''. Amesema Wanjiru.
Taarifa zilizowakaribisha kwenye runinga ziliwafuta utando wa macho na kuwajuza kuwa kumetokea mlipuko mkubwa eneo la bandari.
Inasemekana kwamba hali ya nyumba kutetemeka sio kuwa ilitokea kwa watu wa eneo la tukio au karibu na hapo tu bali hata katika maeneo ya vijijini hilo likidhihirisha nguvu ya mlipuko uliotokea.
Kwa mujibu wa mkaazi wa Beirut Bi. Wanjiru, hospitali iliyokuwa karibu ilichukua watu mia tano ikasema haiwezi kuchukua idadi zaidi ya hiyo na waathirika wengine wakaanza kupelekwa katika hospitali zingine.
''Karibu na eneo la mlipuko kuna mahoteli na huku maisha ni saa 24 yaani maisha ya raha hivi'' amesema Wanjiru.
Ingawa serikali ilikuwa imesema kwamba chanzo cha mlipuko huo huenda ikawa ni fataki lakini kwa jinsi hali ilivyokuwa, vitu kuanguka vyenyewe na mitetemeko ya ajabu, wakaazi wamelitilia mashaka.
Tukio hilo bado limeendelea kuzua maswali na wasiwasi mkubwa kwa umma hasa kwa kushindwa kung'amua ni nini hasa kilichotokea.