Mlipuko Beirut wawaua watu zaidi ya 100 na kusababisha uharibifu mkubwa nchini Lebanon

Iliyochapishwa

Wafanyakazi wa uokoaji nchini Lebanon wanasaka zaidi ya watu 100 waliotoweka kufuatia mlipuko mkubwa uliokumba eneo la bandari ya mji mkuu wa Beirut siku ya Jumanne.

Mlipuko huo umewaua takriban watu 100 kufikia sasa na kuwajeruhi wengine 4,000.

Mji wote uliyumbishwa na mlipuko huo ulioanza kwa moto katika bandari kulikosababisha kutokea kwa wingu la uyoga kutokea.

Raisi Michel Aoun alisema kwamba tani 2,750 za ammonium nitrate zilikuwa zimewekwa vibaya katika ghala moja kwa miaka sita.

Aliitisha kikao cha dharura siku ya Jumatano na kutangaza hali ya dharura ya wiki mbili .

Rais Aoun pia alitangaza kwamba serikali itatoa dola milioni 66 za hazina ya dharura. ''Kile tunachoshuhudia ni janga kubwa'', alisema mkuu wa kundi la msalaba mwekundu George Kettani akizungumza na vyombo vya habari. ''Kuna waathiriwa kila mahali''.

Maafisa walisema siku ya Jumanne kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo kilichosababisha mlipuko huo.

Baraza kuu la ulinzi nchini Lebanon lilisema kuwa wale waliohusika wataadhibiwa vilivyo.

Ammonium Nitrate ilikuwa imeshushwa kutoka kwa meli iliokamatwa katika bandari hiyo 2013 na kuwekwa katika ghala.

Mlipuko huo unajiri wakati mgumu kwa upande wa taifa hilo huku likikabiliwa na mgogoro wa kiuchumi unaosababishwa na mgawanyiko wa jadi pamoja na mgogoro mwingine wa virusi vya corona.

Hali ya wasiwasi pia ilikuwa juu kabla ya uamuzi wa siku ya Ijumaa kuhusu kesi ya mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu Rafik Hariri 2005.

Je ni nini kilichotokea?

Mlipuko huo ulitokea muda mfupi baada ya mwendo wa saa kumi na mbili siku ya Jumanne.

Mwandishi wa BBC aliyekuwa katika eneo hilo aliripoti miili ya watu waliokuwa wameuawa na uharibifu mkubwa unaoweza kuifunga bandari hiyo ya Beirut kwa muda.

Vyombo vya habari viliwaonyesha watu wakiwa wamenasa chini ya vifusi.

Shahidi mmoja alielezea mlipuko huo kuwa mkubwa hali inayoweza kusababisha watu kuwa viziwi, huku kanda ya video ikionesha magari yalioathirika pakubwa mbali na majumba yalioharibika.

''Majumba yote yaliokuwa karibu na mlipuko huu yameanguka. Ninatembea juu ya vigae na vifusi wakati wa usiku'', shahidi mmoja karibu na bandari hiyo aliambia AFP.

Hospitali zilidaiwa kushindwa kuhimili idadi ya watu na majumba mengi yaliharibiwa.

Mlipuko huo ulisikika umbali wa kilomita 240 katika kisiwa cha Cyprus mashariki mwa bahari ya mediterenean, huku watu katika eneo hilo wakisema walidhania lilikuwa tetemeko la ardhi.

Pia unaweza kutazama:

Je ammonium nitrate ni nini?

Amonium nitrate ina matumizi tofauti lakini matumizi yake mawili maarufu zaidi ni kilimo kama mbolea na kutengeneza vilipuzi.

Inalipuka kwa haraka inapokutana na moto na inapolipuka hutoa gesi yenye sumu ikiwemo ile ya nitrogen oxide na gesi ya ammonia.

Na kwasababu ni rahisi kulipuka kuna masharti makali kuhusu jinsi ambavyo inafaa kuhifadhiwa ili kusalia salama ikiwemo sharti kwamba eneo la kuihifadhi linafaa kuzuiwa kuvutia moto.

Je hali ikoje nchini Lebanon?

Lebanon inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa huku kukiwa na maandamano dhidi ya serikali kwa kushindwa kukabiliana na tatizo la kushuka kwa uchumi tangu mgogoro wa kiuchumi wa 1975-1990.

Wengi wanalaumu maafisa wakuu serikalini ambao wanatawala siasa kwa miaka kadhaa na kujilimbikizia mali huku wakishindwa kufanya mabadiliko muhimu ya kutatua tatizo la taifa hilo.

Raia wanakabiliwa na tatizo la kukatwa kwa umeme kila siku, ukosefu wa maji safi ya kunywa na huduma ya afya .

Kumekuwa na hofu katika mpaka na Israel ambayo ilisema wiki iliopita kwamba ilizuia jaribio la Hezbollah kuingia katika himaya ya Israel.

Lakini afisa mmoja mkuu wa Israel ameambia BBC kwamba Israel haina uhusiano wowote na mlipuko wa Beirut.

Mlipuko huo ulitokea karibu na eneo ambalo mlipuko mkubwa wa gari ulimuua waziri huyo wa zamani Hariri.