Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Chama cha NRM chamuidhinisha Museveni kuongoza taifa kwa muhula wa sita
Chama tawala cha rais wa Uganda Yoweri kaguta Museveni NRM kimesema kuwa kiongozi huyo amepata saini za kutosha kumuwezesha kugombe kiti cha urais.
Iwapo Bwana Museveni atachaguliwa kuiongoza Uganda kwa muhula mwingine wa miaka mitano, atakuwa ameliongoza taifa hilo kwa miaka arobaini, na anaweza kuongoza miaka zaidi iwapo atataka kufanya hivyo.
Msemaji wa chama cha NRM Rogers Mulindwa ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Bwana Museveni tayari "ameidhinishwa na chama kama mgombea wake " katika uchaguzi ujao.
Ingawa tarehe rasmi ya uchaguzi mkuu wa Uganda haijatangazwa, inatarajiwa kuwa uchaguzi huo utafanyika Februari 2021.
Bwana Mulindwa amesema kuwa hakuna mtu mwingine katika chama cha NRM aliyeonesha nia ya kukabiliana na Bwana Museveni ili kukisimamia katika uchaguzi wa urais.
Museveni sasa anatarajiwa kukabiliana na Mbunge wa upinzani Robert Kyagulanyi, anayefahamika zaidi kwa jina la usanii kama Bobi Wine kubera mwenye umri wa miaka 38, ambaye anatarajiwa kuwania kiti cha urais.
Bwana Kyagulanyi amekuwa akiukosoa utawala wa rais Museveni kwa kuwekea vikwazo wapinzani katika juhudi zao za kujiandaa kwa uchaguzi
Bwana Museveni ameliongoza taifa la Uganda kwa miaka 34, akiwa ni miongoni mwa viongozi wa Afrika waliodumu kwa miaka mingi zaidi mamlakani. Anayeongoza ni Kiongozi wa Guinea Equatorial Teodoro Obiang ambaye amekuwa mamlakani kwa miaka 41 akifuatiwa na rais Paul Biya wa Cameroun ambaye ameliongoza taifa hilo kwa miaka 38 hadi sasa.
Upinzani unamtuhumu Bwana Museveni kutumia nguvu na vitisho dhidi ya upinzani na kutumia raslimali za taifa kuwafurahisha wanaomuunga mkono na kutafuta wafuasi wengine.
Wapinzani nchini Uganda wanalalamika kuwa katika kipindi cha mwezi wa Julai pekee mikutano miwili ya upinzani imesambaratishwa na polisi , ili hali mikutano ya upande wa serikali ikiruhusiwa kufanyika kila mara.
Hatahivyo msemaji wa chama tawala Rogers Mulindwa amepinga madai ya upinzani, akisema kuwa sheria zinavunjwa kwa pande zote. Mulindwa amesema wapinzani wanaoishutumu serikali kuwazuia kufanya mikutano ''wanafanya ili kuvutia ufuasi'', limeripoti shirika la habari la Reuters.
Bwana Museveni alichaguliwa kuiongoza Uganda mara tano.
Mwaka 2005 bunge la Uganda liliondoa kipengele cha katiba kinachohusu ukomo wa mihula ya uongozi wa rais.
Mwaka 2017 bunge hilo lenye wabunge wengi wa chama cha NRM- liliondoa ukomo wa umri wa rais, jambo lililokuwa kikwazo kwa rais Museveni kugombea tena kiti hich, na hivyo kumpa ruhusa ya kuwania urais.
Upigaji kura juu ya kipengele hicho cha katiba kinachohusu umri wa rais uliibua mjadala mkali na hata wabunge kupigana makonde, na kuwalazimu maafisa wa usalama kuingilia bungeni na kuwaondosha kwa nguvu wabunge wa upinzani bungeni.