Omar al-Bashir: ashtakiwa kwa mapinduzi yaliyomsaidia kuchukua madaraka 1989

Iliyochapishwa

Aliyekuwa rais wa Sudan Omar al- Bashir amefunguliwa kesi katika mji mkuu wa taifa hilo Khartoum , kuhusiana na mapinduzi ya kijeshi yaliyomsaidia kuchukua mamlaka zaidi ya miongo mitatu iliopita.

Bashir mwenye umri wa miaka 76 ambaye alihukumiwa kwa ufisadi, huenda akakabiliwa na hukumu ya kunyongwa iwapo atapatikana na hatia kuhusu jukumu lake katika mapinduzi hayo ya 1989.

Zaidi ya maafisa 20 wa zamani wanashtakiwa pamoja naye

Bashir alilazimishwa kuondoka mamlakani 2019 kufuatia maandamano makubwa.

Maandamano hayo ya raia yalianza polepole kabla ya kushika moto na kuwa wito dhidi ya rais Bashir kung'atuka madarakani. Tarehe 11 mwezi Aprili 2019, jeshi lilitangaza kwamba ameondolewa madarakani.

Serikali ya muungano ya mpito ilioshirikisha maafisa wakuu wa jeshi na raia ilibuniwa.

Bashir pia anasakwa na mahakama ya ICC kuhusu uhalifu wa kivita katika jukumu lake katika mauaji ya kimbari yaliotokea katika jimbo la Darfur.

Mamlaka ya Sudan ilisema February kwamba iko tayari kumpeleka kiongozi huyo wa zamani katika mahakama ya ICC.

Ni nini kilichotokea mahakamani?

Waliokuwa kizimbani kujitetea ni pamoja na makamu wa rais wa zamani Ali Osman Taha na Bakri Hassan Saleh kulingana na chombo cha habari cha AFP.

Mahakama hii itawasikiliza wote na tunawapatia washukiwa hawa 28 fursa ya kujitetea, ilimnukuu rais wa mahakama hiyo Issam al-Din Mohammad Ibrahim akisema.

Imeongezea kwamba mmoja ya mawakili 150 wa Bashir, Hashem al- Gali , alisema mahakamani kwamba mteja wao na washukiwa wengine walikuwa wanakabiliwa na kesi ya kisiasa inayofanyika katika mazingira yasio ya kawaida.

Mahakama hiyo iliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 11 kabla ya taarifa yoyote ama ushahidi kutolewa kulingana na chombo cha habari cha reuters.

Uamuzi huo uliafikiwa ili kuruhusu mawakili na ndugu za washukiwa hao kuhudhuria, iliongezea.

Kilichotokea mwaka 1989

Bashir alichukua mamlaka katika mapinduzi ya kijeshi tarehe 30 mwezi Juni 1989 dhidi ya serikali iliochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ya waziri mkuu Sadek al-Mahdi.

Pamoja na maafisa wengine ambao walihudumu katika serikali yake Bashir anatuhumiwa kupanga mapinduzi ambapo jeshi liliwakamata viongozi wa kisiasa wa Sudan , kuahirisha bunge kufunga uwanja wa ndege na kutangaza mapinduzi hayo kwenye redio.