Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Wajawazito wanakufa huku wagonjwa wakipigania oksijeni
Uchunguzi uliofanywa na BBC kwa wiki kadhaa katika hospitali ambazo ni chafu nchini Afrika Kusini umebaini mapungufu kadhaa ya kimfumo na kuonyesha namna madaktari na wauguzi wanavyopitia kipindi kigumu kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 huku mfumo wa afya ukikaribia kuporomoka.
Huku wahudumu muhimu wa afya wakiwa kwenye mgomo ama wameambukizwa virusi vya corona mashariki mwa Cape, wauguzi wanalazimika kufanya kazi ya usafi, madaktari wa upasuaji wanaosha wenyewe nguo za hospitali.
Pia kuna taarifa za kushtua kuwa watoto wanaokaribia kuzaliwa wanakufa kwa sababu ya msongamano na ukosefu wa wahuduma kwenye wodi za wamama wajawazito.
Huku madaktari, jumuiya za usimamizi ukikabiliana na ukosefu wa raslimali, daktari mmoja mwandamizi alielezea hali hiyo kama kuporomoka kabisa kwa mfumo wa kiafya kwa sababu ya ufisadi huku mwingine akizungumzia kuathirika vibaya kwa taasisi, idara ya afya imefilisika na mfumo huo sasa hivi unapitia changamoto kubwa licha ya kwamba umekosa usimamizi wowote wa kimkakati.
Hilo limejitokeza wakati tu ambapo Afrika Kusini ambayo ilikuwa imechukua hatua za kukabiliana na ugonjwa wa corona kwa miezi kadhaa iliyopita zilizolemaza hata shughuli za kiuchumi - sasa hivi maambukizi yanaendelea kuongezeka kote nchini humo na kupelekea Rais Cyril Ramaphosa kutoa onyo kwamba ni jukumu la kila mmoja kukabiliana na janga hilo.
Hofu na uchovu
Mfumo wa afya unaoyumba hasa katika mji wa Bandari wa Elizabeth, ulizua maswali kuhusu maafisa husika waliokuwa wanawajibika.
"Kuna hofu kubwa, uchovu wa kiakili na hata kihisia.Tunashirikiana na wafanyakazi kidogo sana hata kabla ya ugonjwa wa Covid-19 na sasa hivi tumepungua kwa asilimia 30 zaidi," amesema Dkt John Black.
"Huduma zimeanza kuporomoka kipindi hiki kigumu. Ugonjwa wa Covid umeweka wazi mapungufu yote ya mfumo. Unafanya kuwe na migogoro mingi," alisema, akithibitisha taarifa kwamba wagonjwa wamekuwa wakipigania oksijeni katika vyumba vya wagongwa katika Hospitali ya Livingstone Bandari ya Elizabeth.
Dkt. Black - mmoja kati ya wataalamu wawili tu wa magonjwa ya kuambukiza katika eneo hilo leye idadi ya watu karibia milioni saba - alikuwa ni daktari pekee katika Bandari ya Elizabeth aliyekubali kuzungumza na BBC kwa kurekodiwa lakini wauguzi wengine kadhaa na madaktari walizungumza kwa masharti ya kutotambuliwa, wakihofia kwamba huenda wakapoteza kazi zao iwapo watajulikana.
Panya wanakula uchafu wa rangi nyekundu`
Hospitali ya Livingstone -iliyotengwa kwa wagonjwa wa Covid-19 - madaktari na wauguzi wanaelezea matukio yanayoendelea kama vita, yaani damu na uchafu vyote vikiwa sakafuni, ukosefu vifaa vya kujikinga, upungufu wa oksijeni, upungufu mkubwa wa magari ya kubeba wagonjwa (ambulansi), ukosefu wa mashine za kusaidia kupumua na wagonjwa kulala chini kwa kutandika magazeti.
Pia panya nao wamejaa kwenye jalala la hospitali lenye taka nyekundu katika sehemu iliyowazi.
"Madaktari wanajitahidi kufanya upasuaji ambao ni wa dharura, kupangapanga, kusugua sakafu, kushirikiana na muuguzi mmoja au wawili. Wasimamizi wa kike wa wauguzi wanaosha nguo za hospitali," daktari mmoja ameandika kupitia barua pepe.
"Kila siku huwa ninakuja kufanya kazi kwa hofu," amesema muuguzi mwandamizi ambaye tu ndio amemaliza zamu yake.
"Maambukizi yanazidi kuongezeka. Kila wakati huwa kunatokea migogoro. Kuna wanawake wengi ambao ni wajawazito katika wodi zote," amesema muuguzi mwingine.
'Kina mama na watoto wanakufa'
Madaktari kadhaa wamesema wafanyakazi wamepata mfadhaiko kutokana na tukio la hivi karibuni ambapo chumba cha kujifungulia katika Bandari ya Elizabeth hospitali ya Dora Nginza kilizidiwa na wagonjwa kiasi kwamba kina mama kadhaa na watoto wachanga walikufa.
"Binafsi nilihusika na kuzalisha watoto wawili waliokuwa wamekufa tumboni na najua kuna wengine wengi. Hii si kawaida. Kuona kina mama na watoto kadhaa wamekufa kwa wiki moja katika hospitali moja haikubaliki," amesema mmoja wa madaktari.
Walishawishika kwamba vifo hivyo ni kutokana na upungufu wa wafanyakazi ambao umesababisha wanawake wengi wajawazito kusubiri kwa siku kadhaa kupata huduma, wakati mwingine hata wanalala tu kwenye ushoroba wa hospitali wakisubiri kufanyiwa upasuaji wa dharura.
Wahudumu wengine wa afya wenye taarifa za kinachoendelea kwenye wadi wamethibitsha taarifa za kutokea kwa vifo vingi vya watoto ambao bado hawajazaliwa wiki za hivi karibuni.
Mgogoro huo wa afya pia umeripotiwa na gazeti la Daily Maverick la Afrika Kusini na vyombo vingine vya eneo na kusemekana kwamba kumechangiwa na ukosefu wa usimamizi mzuri ambao umefanya idara mbalimbali kushirikiana wenyewe kwa wenyewe na kutumia ugonjwa wa Covid-19 kama fursa ya kutoa maliliko yao kuhusu kile kilichotokea", kulingana na afisa mmoja.
Hospitali ya Livingstone imekuwa bila afisa mkuu au timu ya usimamizi kwa mwaka mmoja na nusu baada ya timu iliyokuwepo kufutwa kazi kwa madai ya ufisadi.
"Kwa muda sasa tumekosa kiongozi," amesema Dkt Black akilalamikia ukosefu wa uongozi thabiti kutuliza migogoro inayoendelea kutibuka katika idara mbalimbali hospitalini hususan na wenyeji.
Jumuiya za wafanyakazi Afrika Kusini zimekuwa zikionyesha utendakazi wake katika Bandari ya Elizabeth wakati wa janga hili.
Wafanyakazi wanaohusika na kuosha nguo, kufanya usafi, na wauguzi wengine wote wamewahi kugoma kwa nyakati tofauti tofauti.
Hatua ya kufungwa ghafla kwa kliniki ndogo ndogo kumefanya wagonjwa wengi kuelekea kwenye hospitali kubwa tatu na kusababisha kuzidiwa na wagonjwa.
"Tumeshuhudia Jumuiya za wafanyakazi zikifunga hospitali moja baada ya nyingine. Kila wakati mfanyakazi mmoja au mgonjwa anapothibitishwa kuambikizwa virusi vya corona, wafanyakazi wote wanagoma. Huku malalamiko ya miungano yote hiyo ikitolewa, hakuna kinachotokea… kwa hadi wiki mbili," daktari mmoja amelalamika.
'Hatuwezi kuweka maisha ya wauguzi hatarini'
Maafisa wa muungano wa wafanyakazi wamekuwa wakitetea wanachama wao.
"Sio kweli kwamba tunatumia janga hili kujinufaisha," amesema Khaya Sodidi, katibu wa muungano wa wauguzi.
"Wauguzi wetu wamezidiwa, kulazimika kusafisha sakafu au kupika kwasababu hakuna wafanyakazi. Hatuwezi kuweka maisha ya wauguzi hatarini. Pia wao ni binadamu."
Aidha, madaktari kadhaa wametetea uamuzi wao wa kushiriki mgomo na kusema kwamba hatua iliyochukuliwa na wahudumu wa afya sio tu ni kwa sababu ya ugonjwa a Covid-19 lakini pia wamenyanyaswa kwa miaka mingi.
Mwingine amekosoa hatua ya kufunga kliniki kwasababu ya kutokea kwa maambukizi ya mtu mmoja au wawili na kusema kuwa hatua hiyo haikustahili.
Makubaliano ya pamoja miongoni mwa miungano na wahudumu wa afya ni kwamba mgogoro wa sasa wa kiafya ni matokeo ya moja kwa moja ya athari ambazo zimekuwepo kwa miaka mingi za usimamizi mbaya, wizara ya afya kutengewa pesa kidogo na ufisadi.
Athari zinatofautiana lakini hospitali ya Livingstone sasa hivi inakabiliana na janga ikiwa na theluthi moja tu ya wafanyakazi.
"Tuna historia ya tatizo la ukosefu wa wafanyakazi, ukosefu wa uongozi, ufisadi, na mengine mengi. Huduma za afya zimekuwa zikikumbana na changamoto hizi kwa miaka 10. Sasa mfumo umeporomoka," amesema Cole Cameron kutoka wakfu wa Igazi, shirika la eneo la afya lisilo la kiserikali.