Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Halmashauri Kuu ya CCM yamchagua Hussein Mwinyi kugombea urais Zanzibar
Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Dkt Hussein Mwinyi amepitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama cha CCM kugombea urais wa Zanzibar.
Ni Mbunge wa jimbo la Kwahani, Zanzibar na Waziri wa Ulinzi katika serikali ya muungano. Huyu ni mtoto wa Rais mstaafu wa awamu ya pili ya serikali ya Jamhuri ya Mungaano wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Jina la Mwinyi sasa litapelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ili kumthibitisha rasmi kuwa mgombea wa CCM Zanzibar.
Dkt Mwinyi amepitishwa kwa kura 129 sawa na asilimia 78 ya kura zote.
Mwinyi alikuwa akikabiliana na upinzani kutoka kwa wanachama wenzake akiwemo Shamsi Vua Nahodha aliyepata kura 16 na Dkt Khalid Salim Mohammed aliyepata kura 19.
Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kura hizo Mwinyi aliwashukuru wajumbe wote kwa kuonesha imani kwake.
"Hizi ni kura nyingi sana...nikuahidini kuwa tutakuwa pamoja tukatafute ushindi wa Chama Cha Mapinduzi,"
Katika nyakati hizi zenye vijana wengi wanao hoji mara kwa mara maslahi ya Zanzibar katika Muungano na Tanganyika, Dkt. Mwinyi ambaye ni tabibu kitaaluma, anaonekana kuwa kichwa muhimu kuipeperusha bendera ya CCM Zanzibar, si kwa sababu tu ya siasa zake za utiifu, pia ni kwakuwa uhusiano wake kisiasa na kidamu uko pande zote mbili za muungano.
Yuko katika shughuli za kisiasa tangu mwaka 2000, hapa ni kusema sio mgeni katika uwanda wa siasa za Tanzania.
Ametumikia nafasi ya ubunge pande zote za Muungano, alikuwa Mbunge katika jimbo la Mkuranga, mkoa wa Pwani kabla ya kuwa Mbunge wa Kwahani.
Hii ina maana safari yake ya kisiasa inafanana na ya baba yake aliyetumikia nafasi ya urais pande zote za Muungano.
Rais wa sasa Dkt. Ali Mohamed Shein anamaliza miaka yake kumi ya kuiongoza Zanzibar, nchi ya visiwa na yenye mamlaka ya ndani pekee.
Magufuli apitishwa kuwania awamu ya pili
Kikao hicho pia kimempitisha kwa pamoja rais John Magufuli kuwania awamu ya pili ya urais wa Tanzania.
Magufuli hakuwa na mpinzani katika mchakato huo kwa kuwa hakukuwa na Mwananchi a mwengine wa CCM aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo.
"Niwaombe wote tukashirikiane kutafute ushindi...wakati mwengine kunakuwa na hali ya kujiamini. Tukijiamini hatutashiriki ipasavyo, tukafanye kazi kwa nguvu ili tukapate ushindi wa kishindo," alisema Magufuli baada ya kupitishwa.
Kama ilivyo kwa jina la Mwinyi, jina la Magufuli pia litapelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kesho Jumamosi ili lithibitishwe rasmi.