Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Madagascar yaweka amri ya kutotoka nje kufuatia ongezeko la corona
Madagascar imeuwekea mji wake mkuu Antananarivo amri ya kutotoka nje kufuatia ongezeko jipya la maambukizi ya virusi vya corona, miezi miwili baada ya masharti hayo kuondolewa, ametangaza rais.
Katika taarifa, eneo la Analamanga ambalo ndilo lenye mji mkuu linafungwa tena, rais alisema.
''Hakuna magari yatakayoruhusiwa kuingia ama kutoka katika eneo hilo kuanzia leo Jumatatu hadi Julai 20 na masharti makali yatawekewa wanaotoka''.
''Ni mtu mmoja mmoja katika kila familia atakayeruhusiwa kwenda barabarani kati ya saa kumi na mbili asubuhi na saa sita mchana'', ilisema taarifa hiyo.
Hatua hizo zimechukuliwa kutokana na kusambaa kwa mlipuko huo na kuongezeka kwa visa vya Covid-19, iliongezea.
Madagascar ilikuwa imezoea kuandikisha visa vichache kwa siku vya ugonjwa huo lakini sasa ,taifa hilo katika siku za hivi karibuni limwthibitisha idadi kubwa ya wagonjwa wa Covid 19 kila siku , ambapo wagonjwa 216 waliripotiwa siku ya Jumamosi baada ya watu 675 kupimwa.
Takriban watu 24,000 wamepimwa virusi hivyo kuafikia sasa.
Tangu virusi hivyo vilipogunduliwa katika kisiwa hicho Machi 20 , taifa hilo lilikuwa na jumla ya wagonjwa 2,728 ikiwemo watu 29 waliofariki kufikia siku ya Jumapili.
Usikilizaji wa kesi umeahirishwa na mikutano yote itafanyika kupitia kanda za video.
Aprili , rais Andry Rajaoelina alizindua dawa ya mitishamba ambayo alidai inazuia na kuponya virusi hivyo vya corona.
Rajoelina amekuwa akikuza dawa hiyo kwa lengo la kuiuza katika nchi za kigeni, akiitaja kuwa 'dhahabu ya kijani' itakayobadili historia ya taifa hilo.
Manufaa ya dawa hiyo ya Covid Organics, inayotokana na mmea wa pakanga - mmea unaotibu malaria pamoja na mitishamba mingine hayajathibitishwa na utafiti wa kisayansi.